Rosebell Owiti: Anawasaidia wasanii wenzake msimu wa corona
Na DIANA MUTHEU
UNAPOINGIA katika lango la Studio BelaBela ambalo liko umbali wa karibia mita mia mbili kutoka kwa duka kuu la Naivas, Bamburi, utakaribishwa na bango kubwa lililotengenezwa kwa ustadi wa kiwango cha juu.
Kando ya bango hilo kuna bustani ndogo iliyo na aina tofauti ya maua yanayoninginia, mengine ni ya kutambaa na zimepandwa katika vifaa vya kawaida kama chupa za plastiki zilizokatwa, mikebe ya rangi, magurudumu kuukuu- yote kuashiria kwamba eneo hilo ni la sanaa.
Ndani ya jengo hilo la sanaa, bidhaa nyingi zimetengenezwa kwa njia ya ubunifu ikiwemo magogo y miti yaliyounganishwa na vyuma kutengeneza stuli, magurudumu yaliyorembeshwa kwa kupakwa rangi na kugeuzwa kuwa meaza, miongoni mwa vifaa vingine.
Tangu mwezi Mei mwaka huu, jengo hilo limekuwa kimbilio la wasanii wengi katika kaunti za Mombasa, Kilifi na hata Kwale.
Wasanii wa aina mbalimbali kama vile: waimbaji, wachoraji, wale wa kubuni mitindo ya nguo na viatu (designers), wapiga picha, wanaorekodi video, malenga na wengine wengi wameweza kupata nafasi ya kukuza talanta zao ndani ya jengo hilo, licha ya kukosa nafasi zingine, jambo lililosababishwa na janga la corona.
Rosebell Owiti, 33, ambaye ni msanii na mmiliki wa jengo hilo anasema kuwa janga la corona liliathiri pakubwa maisha ya wasanii hapo mwanzoni, na aliamua kutenga sehemu ya jengo lake, ili kuwapa wasanii haswa vijana nafasi mbadala ya kujitafutia riziki.
Anasema kisa cha kwanza cha mgonjwa wa corona kilipotangazwa nchini, mambo mengi yalibadilika.
“Maeneo ya burudani yalifungwa, kumaanisha kuwa waimbaji, malenga, wapiga picha, wanaochukua video, wapambaji, wapishi, DJs pamoja na wasanii wengine katika sekta hiyo hawangeendelea na kazi zao. Pia, katika eneo la Pwani, hoteli nyingi zilifungwa na zaidi mikutano ikapigwa marufuku. Kafyu nayo ilitangazwa kuanzia saa moja. Wasanii waliokuwa wanajichumia riziki kwa njia hiyo walibaki bila kazi,” akasema Bi Owiti huku akisema kuwa hali hiyo ilimhuzunisha ndipo akaamua kutengea wasanii nafasi katika studio yake, ili watafute njia mbadala ya kutafuta hela.
Akizungumza na Taifa Leo Dijitali, Bi Owiti alisema kuwa mnamo Mei, alishirikiana na baadhi ya wasanii kutengeneza video moja ya kuwajulisha wasanii tofauti kuwa wanaweza kufanyia kazi zao katika majengo ya Studio BelaBela.
Katika video hiyo, mtangazaji anaanza kwa kuwaalika wasanii wote katika studio hiyo, kisha video za wasanii tofauti waliokuwa tayari wameanza kufanya kazi zao pale zinaonyeshwa kwa ustadi.
Kwa mfano, binti mmoja mwenye tajriba ya kubuni mitindo ya nguo anayejulikana kama Jojo Dena ama Denah Fashions anaonekana akimvalisha sketi moja la kuvutia mtangazaji huyo.
Pia, kijana mmoja kwa jina Justine Rotah ambaye anatengeneza video na picha katika mtandao wa Youtube anaonekana akipigia debe biashara yake ya kuuza suti.
Video hiyo iliwekwa katika mitandao tofauti ya kijamii kama vile Youtube, Facebook, Instagram na WhatsApp.
“Wasanii wengi walinipigia simu na hata kunitumia jumbe wakitaka maelezo kuhusu nafasi hizo nilizotaja. Hata hivyo, hakuna ada yoyote walitoa kujiunga na sisi,” akasema msanii huyo ambaye amebobea katika uchoraji na pia kutoa mafunzo katika fani hiyo.
Alielezea kuwa ili kuwe na umoja na uwiiano katika utendakazi wao, wametengeneza chama katika mtandao wa Whatsapp ambapo wasanii wote katika jengo hilo huwa wanajadiliana maswala yao.
“Jambo la kwanza, msanii anayejiunga na sisi anafaa kuhisi kuwa hapa ni ‘nyumbani’. Pili, anafaa kufanya kazi yake kwa uendelevu na asife moyo, zaidi awe na imani kuwa kuna siku kazi yake itatambulika, na atavuna kipato cha kuridhisha,” akasema.
Bi Owiti alisema kuwa msaada ambao wamepeana baina yao ni jambo la kufurahikiwa.
“Jambo la maana ambalo naweza kusema tumefaidi sana kupitia mpango huu ni kuwa tumeweza kutoa huduma zetu kwa wenzetu, ambao walikuwa wanahitaji huduma zetu pia. Pia, wasanii wengi wameweza kujiuza kupitia mitandao tofauti ya kijamii na kupata wateja ,” akasema.
Bi Owiti anasema kuwa changamoto kubwa kwake kama msanii msimu huu wa janga hili ni kuwa, biashara ilididimia.
“Nilisitisha kutoa mafunzo ya uchoraji na sanaa ya kutumia uzi kutengeneza bidhaa mbalimbali kwa watoto ili kuwaepusha na maambukizi ya maradhi ya Covid-19. Pia, kwa jumla wateja wa bidhaa zangu zingine kama vile herini, mapambo na upigaji picha walipungua,” akasema Bi Owiti.
Alisema kuwa kwa jumla, wasanii wengi wamepatwa na msongamano wa mawazo msimu huu wa corona, kwa sababu asilimia kubwa kazi zao huwa sawia na vibarua- unapata leo, kesho unakosa.
Aliiomba jamii iwaelewe wasanii na kuwachukulia kama binadamu walio na shida zao pia.
“Zaidi, umaarufu una taabu yake pia. Baadhi ya wasanii wamekumbwa na matatizo msimu huu wa corona na mtindo wao wa maisha ukaathiriwa pakubwa na janga hili. La kuhuzunisha zaidi ni kuwa watu wengi huwasuta na kuwadharau, jambo ambalo hupelekea wawe na msongamano wa mawazo,” akasema Bi Owiti.
Mawaidha yake kwa wasanii mbalimbali ni kuwa wasivunjike moyo na wasiache kubuni. “Zaidi, watumie mitandao tofauti ya kijamii kujipigia debe,” akasema.
Kwa sasa, msanii huyo ameanzisha mradi wa kutengeneza vyungu vya kupandia maua, na anakuza maua pamoja na mimea ya viungo, ambayo huwauzia wateja tofauti.
Zaidi, ameanza kukarabati nafasi katika studio hiyo ambayo wachoraji watano watakuwa wanafanyia kazi zao.