Mbio za AK kuandaliwa Naivasha
Na CHRIS ADUNGO
MJI wa Naivasha utakuwa mwenyeji wa makala ya pili ya mbio za Shirikisho la Riadha la Kenya (AK) za Mountain Running Championships mnamo Novemba 22, 2020.
Mbio hizo zitaanza katika shule ya Cornerstone Preparatory Academy iliyoko kwenye Barabara ya Naivasha-Mai Mahiu na kukamilikia katika eneo la Fly-Over.
“Mbio za milimani sasa ni sehemu ya mashindano rasmi katika kalenda yetu. Tunapania kutumia mashindano haya kuwaandaa wanariadha wetu kwa mapambano yajayo ya dunia ya kukimbia katika sehemu za milima. Tunawasihi pia wanariadha wetu wa haiba kubwa kutumia mbio hizo kujinolea kwa vipute mbalimbali vya msimu ujao,” akasema Naibu Rais wa AK, Paul Mutwii ambaye pia ni mkurugenzi wa mashindano katika shirikisho hilo.
Kwa mujibu wa kinara huyo, kukimbia katika maeneo ya milima huwapa wanariadha stamina na ustahimilivu ambao huhitajika zaidi kwenye mbio za masafa marefu au katika hatua za mwisho za mbio.
Mashindano ya mwaka huu ambayo yatafanyika kwa siku moja yatafanyika karibu na Mlima Longonot na yatakuwa huru kwa wanariadha wa haiba na yeyote anayepania kushiriki ila kwa ada ya Sh200.
“Mbio za mwaka huu zitakuwa katika kategoria tatu: kilomita nane kwa wanaume chipukizi, kilomita nane kwa wanawake wazima na kilomita 10 kwa wanaume wazima. Mashindano hayo yatafanyika katika eneo tambarare na kwenye sehemu za kupanda mlima mrefu (mita 930) na kushuka mabonde (mita 330),” ikasema sehemu ya taarifa ya AK.
Mbali na sehemu ya kukimbilia kuwa na mabonde na milima, pia kuna mawe na mwinuko mkubwa wenye urefu wa hadi mita 2,685 juu ya usawa wa bahari katika eneo la Kenton.
Washindi wa mbio hizo watajizolea zawadi kemkem zikiwemo pesa na medali. Ni matumaini ya AK kwamba mashindano hayo ya Mountain Running yatatoajukwaa mwafaka kwa wanariadha kujiandaa kwa mbio za nyika zitakazofungua rasmi kampeni za msimu huu wa 2020 mnamo Novemba 28 mjini Machakos.
Haya yatakuwa makala ya pili ya mbio za milimani baada ya kivumbi cha ‘Challenging the Heights’ kilichoandaliwa mnamo 2019 katika Kaunti ya Meru. AK imethibitisha kwamba mbio za Challenging the Heights yatafanyika tena katika Kaunti ya Meru mnamo Februari 20, 2021.
Mutwii ameshikilia kwamba AK inapania sasa kuvumisha fani ya mbio za Mountain Climbing katika kiwango cha kitaifa na mabara.
“Tunaazimia pia kutuma wanariadha watakaowakilisha Kenya kwenye mashindano mbalimbali ya haiba ya kukimbia milimani mwaka ujao wa 2021,” akasema Mutwii.
Kati ya mapambano hayo ni yale ya Trail & Nordic Walking Championships nchini Italia (Mei 28-30), Pilancones Tunte Trail nchini Uhispania (Januari 16), World Masters Mountain Running Championships nchini Australia (Septemba 3-5), na International U-18 Mountain Running Cup nchini Uingereza (Julai 24).
Mkenya Lucy Wambui Murigi, 35, amewahi kuibuka bingwa wa dunia katika mbio za Mountain Running mara mbili. Alitawazwa mshindi nchini Australia mnamo 2017 kabla ya kuhifadhi ubingwa huo mnamo 2018 nchini Andorra.