Mapenzi au utumwa?
NA BENSON MATHEKA
Kwa miaka saba, Jane amekuwa akimkwamilia Patrick akidai kwamba anampenda ingawa mwanamume huyo hawajibiki kamwe.
“Nampenda tu,” anasema.Mwanadada huyu amekuwa akipambana kivyake na hata kumsaidia Patrick akiwa na shida.“Nimeshindwa kumuacha ingawa hawajibiki.
Ninampenda sana hivi kwamba sidhani ninaweza kuwa au kuishi na mwanamume mwingine katika maisha yangu,” asema.Lakini licha ya kumkwamilia mwanamume huyo, maisha yake yanazidi kuwa magumu mno.
Patrick hajali kamwe na huwa anajigamba kwamba ana mpenzi anayemjali na asiyemsumbua kwa mahitaji ya hapa na pale kama wanavyofanya wanawake wengine.
Tabia ya Jane ni sawa na wanawake wengine wanaokubali kuwa watumwa kwa kuishi na wanaume wasiowajibika wakisingizia mapenzi. Kulingana na wanasaikolojia, wanawake wanaowavumilia wanaume wa aina hii huwa wanajiweka katika shida. “Ikiwa mwanamume hawajibiki, hata kwa masuala madogo, hatoshi mboga.
Kukwama kwa mwanamume kama huyo ni kujipalilia makaa,” asema Dinah Wangui Kamau, mtaalamu wa masuala ya mapenzi wa shirika la Love Care, jijini Nairobi.
Anasema uhusiano wa mapenzi haufai kulemea upande mmoja. “Uhusiano wa kimapenzi na maisha ya ndoa yaliyokolea mahaba hayafai kulemea upande mmoja na hasa mwanamume anafaa kuwajibika kwa mtu wake. Ikiwa hafanyi hivyo au ukiona dalili kwamba mtu wako hana nia ya kufanya hivyo, jinusuru mapema,” asema.
Ivy Kamene, mwanadada mwenye umri wa miaka 28 asema kwamba alipoteza miaka mitatu katika uhusiano na mwanamume ambaye alikuwa kama kupe kwake.
“Nilimpenda lakini hakutambua kwamba kuna mahitaji ya mwanamke ambayo mwanaume anafaa kutimiza bali na burudani chumbani. Hakuwahi kunionyesha dalili za kujiimarisha maishani. Niliamua kumuacha baada ya juhudi za kumshauri abadilike kugonga mwamba,” asema Kamene.Wangui anasema wanaumewasio wajibika, huwa na maneno matamu na vitendo vichache.
“Ninamaanisha wale ambao wana uwezo wa kutimiza majukumu yao na hawafanyi hivyo. Wanapenda raha na starehe lakini hawajali wapenzi wao na hata watoto wao. Huwa ninashauri wanawake kutowavumilia wanaume kama hao hata kama ni magwiji wa kuwapandisha mizuka chumbani,” aeleza Wangui.
Upofu wa mapezi
Kulingana na Dkt Silas Oponyi, mwanasaikolojia wa kituo cha Big Hearts, jijini Nairobi, mwanamume asiyewajibika kwa mpenzi wake au familia yake akiwa na uwezo wa kufanya hivyo, ni hatari mwanamke kumkwamilia akidai anampenda.
“Mapenzi ya aina hii ni upofu wa kiwango cha juu. Ni hatari, yanaweza kuathiri maisha ya mwanamke na kumkosesha raha. Unawezaje kuvumilia mwanamume asiyejali mwonekano wako kwa kukupa pesa za saluni, kununua nguo na chakula? Utavumiliaje mwanamume asiyejali maisha yako ya siku zijazo na watoto wako?” auliza Dkt Oponyi.
Wangui na Dkt Oponyi wanaonya wanawake dhidi ya kusukuma wanaume wapenzi wao kuwajibika kwa mambo yanayopita uwezo wao.
“Kumsukuma au kutarajia mchumba wako akufanyie mambo yanayopita uwezo wake si sawa. Kunaweza kumsababishia mateso ya kisaikolojia na kuvuruga mambo zaidi,” asema Oponyi.
“Uwajibikaji katika uhusiano wa kimapenzi una mipaka kwa kutegemea uwezo wa mhusika. Makosa ambayo baadhi ya watu hufanya ni kuiga wanavyofanyiwa watu wengine na wachumba wao na kulaumu wapenzi wao kwa kutowajibika ilhali hawana uwezo wa kufanya hivyo,” aongeza Wangui.
Wataalamu hawa wanakubaliana kwamba ni jukumu la mwanamume kuonyesha mchumba wake mwelekeo na kuwa na maono ya siku zijazo.
“Hakuna mwanamke anayefaa kuvumilia mwanamume asiye na maono. Hata hivyo, maono yakikosa kutimizwa kwa sababu zisizoweza kuepukika, haimaanishi amekosa kuwajibika,” asema.
Washauri wa masuala ya mapenzi wanakosoa wanawake wanaowatema wanaume uwezo wao wa kuwajibika unapopungua. “Ikiwa mwanamume amepoteza kazi au mapato yake yakipungua, hawezi kufananishwa na bwege asiyetosha mboga,” asema Wangui.