Michezo

Watambue baadhi ya Waganda waliowahi kusakatia K'Ogalo

November 14th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na JOHN KIMWERE

ERISSA SSEKISAMBU, SHAFIK BATAMBUZE

GOR Mahia FC ni klabu kongwe, kubwa pia ina wafuasi wengi tu sawa na mahasimu wao AFC Leopards maarufu Ingwe. K’Ogalo inajivunia kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL) mara 19.

Licha ya kwamba ni klabu ya kijamii imekuwa ikisajili wachezaji kutoka mataifa ya nje kama Rwanda, Uganda na Ghana kati ya mengine. Katika mpango mzima Gor Mahia inajivunia kusajili jumla ya wanasoka 13 kutoka Uganda ambao waliwahi kushiriki soka kwa faida ya klabu hiyo.

TITO OKELLO

Katika kipindi cha usajili Gor Mahia ambayo imepata pigo la kupoteza takribani wachezaji saba imetwaa huduma za mshambuliaji matata, Tito Okello mzawa wa Uganda ambaye pia huchezea timu ya taifa ya Cranes. Mchana nyavu huyo ni miongoni mwa wachezaji 14 waliosajiliwa na klabu hiyo tayari kuionegesha kwenye kampeni za muhula ujao.

Mpigagozi huyo anayepania kutambisha klabu hiyo kwa kuifungia mabao mengi msimu ujao alitia wino kandarasi ya miaka mitatu. Anajivunia kuchezea timu za Ligi Kuu nchini Uganda kama KCCA FC, Vipers FC bila kuweka katika kaburi la sahau BUL FC. Katika taifa jirani la Tanzania amewahi kuchezea Mbeya City, African Lyon.

Katika klabu za ughaibuni amewahi kupigia Benfica Macau ya Hong Kong. ”Kiukweli nina furaha tele kujiunga na Gor Mahia FC ambayo imejizolea umaarufu sio hapa Kenya pekee bali pia Afrika Mashariki kwa jumla.

Nimepania kuitumikia kwa moyo wangu wote nikilenga kuifungia mabao mengi ndani ya kipindi nitaichezea,” alisema na kuongeza kwamba ana imani atafanya kweli kusaidia katika ligi pia michuano ya Klabu Bingwa Afrika (CAF).

GEOFREY WALUSIMBI

Beki huyu alikuwa kati ya wachezaji muhimu wa K’Ogalo waliosaidia kuinogesha na kubeba taji la KPL msimu wa 2014, 2015, 2017 bila sahau mwaka 2018.

Mchezaji huyo aliibuka muhimu aliposaidia Gor Mahia kupiga hatua katika mashindano ya Afrika Mashariki na Kati mwaka 2015 licha ya kunyukwa mabao 2-0 na Azam FC ya Tanzania. Pia kwa ujuzi wake na huduma zake aliisaidia kutinga mechi za makundi katika shindano la CAF Confederation Cup 2018.

HASHIM SEMPALA

Kiungo huyo ambaye ni mali ya Tusker FC alishiriki soka la humu nchini kwa faida ya Gor Mahia kwenye kampeni za Ligi Kuu ya Kenya (KPL) mwaka 2019 akitokea Tusker FC. Sempala alikuwa mchezaji wa pili kujiunga na K’Ogalo akitokea Tukser baada ya Khalid Aucho.

Mchezaji huyo alihamia Tusker kutoka BUL FC ya Uganda ambapo kando na klabu hiyo pia anajivunia kuchezea Uganda Revenue Authority na Express FC. Akichezea K’Ogalo kocha wake kipindi hicho, Hassan Oktay alimsifia kwa mchezo wake na kumtaja kuwa kati ya wanasoka bora katika Ligi Kuu ya Kenya.

“Nilipendezwa na mchezo wa Sempala ni mchezaji mwenye kipaji cha kusakata boli ambapo anaweza kukabili mpinzani yeyote na kumnyang’anya mpira,” Hassan alinukuliwa akisema.

JUMA BALINYA

MSHAMBULIAJI huyu aliyesepa katika kipindi hiki cha corona na kufuata nyayo za wachana nyavu wengine kutoka Gor Mahia alirejea kwao nchini Uganda alikojiunga na Kampala Capital City Authority (KCCA). Alihama kama wenzake akiwamo Joash Onyango (Simba FC), mnyakaji David Mapigano (Azam FC), winga Dickson Ambundo (Dodoma Jiji) za Tanzania pia Boniface Omondi na kipa Peter Odhiambo wote Wazito FC ya Kenya.

Balinya alijiunga na K’Ogalo mwanzo wa mechi za mkondo wa pili msimu uliyopita huku akipigiwa upatu kutesa na kusaidia klabu hiyo kufanya kweli lakini janga la corona lilisitishwa shughuli za michezo na kuvuruga mpango wake. Balinya ni kati ya mafundi wa magoli katika kanda ya Afrika Mashariki na Kati. Balinya aliwahi kuchezea Police FC ya Uganda na Yanga SC ya Tanzania.

Akisakatia Police msimu wa 2018/19 alifanya kweli alipoibuka mfungaji bora baada ya kucheka na nyavu mara 17. Akipigia K’Ogalo katika mechi tano alizocheza alifunga mabao mawili kwenye mechi ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Nzoia Sugar.

DAN SSERUNKUMA

FOWADI huyu aliibuka kati ya wanasoka wazuri nchini alipojiunga na K’Ogalo akitokea Nairobi City Stars. Aliisaidia Gor Mahia pakubwa hasa kubeba taji la ligi kuu mwaka 2013 na kumaliza ukame wa kulisaka kwa miaka 13. Pia aliibeba kiana ilipohifadhi ubingwa huo kwenye kampeni za muhula wa 2014.

Ndani ya misimu miwili (2013 na 2014) Sserunkuma ambaye huchezea Vipers ya nyumbani kwao alifanikiwa kutikisa nyavu mara 49 baada ya kushiriki mechi 73. Akiwa mali ya K’Ogalo alibahatika kubeba tuzo ya mfungaji bora mara mbili kabla ya kuyoyomea nchini Tanzania kupigia Simba SC.

Katika mpango mzima orodha ya wapigagozi wa Uganda waliowahi kuchezea K’Ogalo pia inajumuisha: Khalid Aucho, Erissa Ssekisambu bila kuweka katika kaburi la sahau Shafik Batambuze kati ya wengine.