• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 5:55 AM
Uwanja wa Kamukunji kukarabatiwa baada ya Wenyeji United kutawazwa mabingwa

Uwanja wa Kamukunji kukarabatiwa baada ya Wenyeji United kutawazwa mabingwa

Na JOHN KIMWERE

WANASOKA wa Wenyeji United wametawazwa mabingwa wa taji la Kamukunji Cup kwenye mashindano yaliyoandaliwa katika Uwanja wa Godown Kamukunji, Nairobi.

Wenyeji United chini ya nahodha, Salim Ochola ilituzwa ubingwa wa taji hilo ilipokomoa Lebanon FC kwa magoli 5-3 katika fainali kupitia mipigo ya matuta baada ya kutoka sare tasa katika muda wa kawaida.

Kwenye nusu fainali Wenyeji United ilichapa Bale Stars mabao 8-7 kupitia mikwanju ya penalti baada ya kutoka sare tasa. Nayo Lebanon FC iliandikisha ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Allstars. Katika matokeo ya robo fainali, Lebanon ilichapa Wenyeji Youth mabao 5-3, Allstars ililaza Kinyago United magoli 3-1, Chemchendas ilinyukwa mabao 2-1 na Wenyeji United nayo Blue Stars ilikomoa Bale FC mabao 2-1.

”Nashukuru wachezaji wangu kwa kuonyesha mechi safi tangu mwanzo hadi mwisho wa kipute cha Kamukunji Cup ambapo waliibuka mabingwa,” alisema kocha wa Wenyeji United, Lazaraus Mbithi na kuongeza kuwa ngarambe hiyo ilisaidia wachezaji wote kwa jumla hasa kipindi hiki mlipuko wa virusi hatari vya corona umesitisha shughuli za michezo kote nchini.

Mashindano hayo yaliandaliwa na makocha wa timu za eneo hilo kwa ajili ya kushurutisha viongozi wa eneo hilo akiwamo mbunge Yusuf Hassan na kamati ya CDF kufanya hima kukarabati Uwanja wa Kamukunji.

“Tuna furaha tele maana tayari mbunge wa eneo hilo ameanza kushughulika maana Uwanja huo umeanza kulainishwa ili kutoa nafasi kwa wanasoka kuanza kuutumia,” alisema kocha wa Fearl FC, Jonah Makau na kuongeza kuwa ni matumaini yao shughuli hizo zitakamilika vizuri hasa Uwanja kuwa katika hali nzuri ya kuchezea.

”Soka limesaidia vijana wengi nchini ambapo ni muhimu pia kutoa nafasi kwa wanasoka wa eneo letu kukuza talanta zao na kujiepusha dhidi ya kushiriki matendo maovu mitaani kama matumizi ya mihadarati na kujiunga na uhalifu.” akasema.

Mashindano hayo yalivutia zaidi ya timu 32 lakini baada ya kushiriki mechi za mchujo zilibakia klabu 20 ambazo zimepangwa katika makundi manne. Kundi A: Wenyeji Youth, Cum Cheddas, Soccer Stars, Istanbul F.A na Eastleigh Stars.

Kundi B: Young Elephant, Kinyago United, Fearless, Uprising na Blue Stars. Kundi C. Chipukizi, Amazon, Fanabache, Base FC na Blue Boys. Kundi D; Wenyeji FC, Green Rhino, Lebanon FC, Tico United na Toronto FC.

You can share this post!

Raha kwa Bundes FC kuwanyamazisha Gogo Boys

LILA NYOKABI: Serikali isaidie kuinua vipaji kutoka familia...