Habari

Reggae kuvuma vifo vikizidi

November 16th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

VALENTINE OBARA na RUSHDIE OUDIA

VIONGOZI katika serikali ya Rais Uhuru Kenyatta kwa ushirikiano na Kiongozi wa chama cha ODM, Bw Raila Odinga, wamepuuza wito wa baadhi ya wananchi kuwa mchakato wa mageuzi ya katiba usitishwe ili taifa hili limakinikie vita dhidi ya janga la corona.

Bw Odinga mnamo Jumapili aliongoza mkutano na magavana wa eneo la Magharibi akiandamana na mawaziri Dkt Fred Matiang’i (Usalama wa Nchi) na Eugene Wamalwa (Ugatuzi), ambapo ishara zote zilionyesha kuwa hakuna mpango wa kusitisha ‘ngoma’ ya kurekebisha katiba, almaarufu ‘reggae’.

Hii ni licha ya kuwa, kwa takriban mwezi mmoja sasa, idadi ya maambukizi na vifo vinavyosababishwa na virusi vya corona imeongezeka mno.

Kufikia Jumapili, idadi ya vifo ilifika 1,269 baada ya watu 20 wengine kufariki huku maambukizi yakifika 70,245. Wagonjwa 59 wamelazwa katika vyumba vya walio hali mahututi (ICU) na kuekewa vifaa vya kuwasaidia kupumua.

Baadhi ya viongozi na wananchi wanaamini huu si wakati mwafaka wa kupigia debe marekebisho ya katiba kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI), ikizingatiwa kuwa kuna changamoto tele ambazo zimesababishwa na janga la corona ambazo zinafaa kutatuliwa kwa dharura.

Miongoni mwa changamoto hizo ni lalama kutoka kwa wahudumu wa afya kuhusu ukosefu wa mazingira bora ya kufanyia kazi ambapo wamekuwa wakijiweka katika hatari ya kuambukizwa corona, na ukosefu wa bima inayoweza kutumiwa na raia kugharimia matibabu ya Covid-19 wanapoambukizwa.

Chama cha Wahudumu wa Afya, Wanafamasia na Madaktari wa Meno (KMPDU) tayari kimetoa ilani ya siku 21 kutaka malalamishi yao yashughulikiwe la sivyo waitishe mgomo.

Changamoto nyingine zilizosababishwa na janga la corona ni kama vile pigo kwa uchumi wa kitaifa.

Wakili mtajika, Dkt John Khaminwa, ameonya kuwa marekebisho ya katiba yanayopiganiwa huenda hata yasipite kwa sababu za kisheria, na hivyo basi itakuwa busara kama vigogo wa siasa nchini watashughulikia majanga yanayokumba taifa kwa sasa.

“Kurekebisha katiba ya 2010 si jambo rahisi inavyodhaniwa. Ni heri pesa za BBI zitumiwe kwa masuala mengine ambayo yanaathiri taifa letu. Lazima tukome kuzungumzia suala la BBI,” akasema wakili huyo mkongwe.

Katika kikao na wanahabari mjini Kisumu baada ya kukutana na magavana wa eneo la Magharibi, Bw Odinga alisisitiza kuwa mipango ya kurekebisha katiba itaendelea mbele.

Kulingana naye, ukusanyaji sahihi za wananchi kuunga mkono mapendekezo ya ripoti ya BBI utazinduliwa wiki ijayo. Sahihi milioni moja za wapiga-kura zitahitajika. Inatarajiwa kampeni za kupigia debe marekebisho ya katiba zitafanywa ukumbini, kwa kuzingatia kanuni za kuepusha maambukizi ya virusi vya corona.

Bw Odinga alipuuzilia mbali wanaopinga BBI akiwakashifu kwa kueneza propaganda.

“Ukweli utajulikana wakati wa kampeni. Tutaenda kila pembe ya nchi. Wananchi watatia sahihi kwa hiari yao wenyewe,” akasema. Alieleza kuwa baadaye, stakabadhi zote pamoja na sahihi zitawasilishwa kwa Tume Huru ya Mipaka na Uchaguzi (IEBC), kisha zitumwe kwa mabunge ya kaunti na baadaye bunge la taifa na seneti ikiwa ripoti itapitishwa na mabunge 24 ya kaunti.

“Itakuwa shughuli ya kidemokrasia. Wale walio na malalamishi tukutane uwanjani na Wakenya wataamua. Naamini watafanya uamuzi bora,” akasema. Kaimu Katibu Mkuu wa KMPDU, Dkt Chibanzi Mwachonda, alieleza masikitiko kwamba wahudumu wapatao 30 wa afya ni miongoni mwa watu ambao wamefariki kwa Covid-19 ilhali serikali haionekani kutilia maanani hali hiyo.

Dkt Mwachonda alisema, kwa miezi minane iliyopita tangu janga la corona lilipoingia nchini, wameshauriana kwa mapana na wadau wote serikalini lakini wameendelea kupuuzwa.

“Covid-19 ni janga la kiafya nchini ambalo limesababishia wahudumu wa afya hali ngumu. Wanachama wetu wametoa huduma zao katika hali hatari hadi wengine wao wakafariki,” akasema Jumapili.

Madaktari wanataka serikali ipeleke mavazi ya kuwaepushia maambukizi (PPE) katika kila hospitali nchini, bima kamilifu ya afya, marupurupu, kuajiriwa kwa madaktari 2,000 na kutenga hospitali maalumu za kuwahudumia katika kila kaunti.

Misimamo ya madaktari iliungwa mkono na shirika la kijamii la Kongamano La Mageuzi (KLM) ambalo lilikashifu serikali ya Rais Kenyatta kwa kukosa mwelekeo madhubuti katika vita dhidi ya Covid-19.

“Hospitali za umma zimegeuka mitego ya maafa, si kwa wagonjwa pekee bali pia kwa madaktari,” shirika hilo likasema katika kikao cha wanahabari Nairobi.