• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 6:50 AM
MATHEKA: Serikali haijaonyesha nia ya kuzima uagizaji sukari

MATHEKA: Serikali haijaonyesha nia ya kuzima uagizaji sukari

Na BENSON MATHEKA

RIPOTI kwamba serikali imeruhusu wafanyabiashara kuingiza nchini sukari kwa wingi licha ya marufuku iliyotangaza Julai, zinaonyesha kuwa hakuna nia njema katika kufufua sekta ya sukari nchini.

Ripoti hizi zinajiri wakati serikali inasisitiza kuwa inaweka mikakati ya kulinda wakulima wa miwa nchini ambao uchumi wao umedorora baada ya viwanda walivyotegemea kufilisika kwa sababu ya kutohimili ushindani sukari ya bei rahisi inapoingizwa nchini.

Serikali pia imetangaza kuwa itabinafsisha viwanda vitano vya sukari nchini hatua ambayo inasema ni miongoni mwa mikakati ya kufufua sekta hiyo.

Hata hivyo, kwa kutohakikisha kwamba marufuku iliyotangazwa na waziri wa kilimo ya kutoingiza sukari nchini, juhudi hizi huenda hazitanufaisha wakulima wa miwa kamwe.

Hii ni kwa sababu ikiwa serikali inashindwa kutekeleza marufuku iliyotangaza wakati viwanda hivyo viko chini ya usimamizi wake, itawezaje kuvidhibiti vikimilikiwa na wawekezaji wa kibinafsi?

Kuna uwezekano mkubwa kwamba wamiliki wa kibinafsi wataweza kuingiza sukari nchini na kuipakia kama iliyotengenezewa nchini au kuendelea kununua miwa kutoka nchi jirani wakulima wa humu nchini wakiendelea kuteseka.

Linalojitokeza hapa ni kuwa serikali haijawahi kuwa na nia ya kufufua, kulinda na kusaidia wakulima wa miwa nchini licha ya ahadi za kila mara. Hii ni kwa sababu wanaohusika na biashara ya kuingiza sukari nchini kutoka nje ni watu wenye ushawishi mkubwa serikalini.

Kwa sababu ya donge wanalovuna, hawawezi kuunga juhudi zozote za kufufua sekta hiyo humu nchini. Hii ndiyo inafanya viongozi kugawanyika kila wakati mapendekezo yanayolenga kunufaisha mkulima yanapotolewa ilivyofanyika wakati ilipopendekezwa viwanda vya sukari viundwe.

Kuna wale waliotaka viwekwe chini ya serikali za kaunti kwa kuwa kilimo ni jukumu lililogatuliwa hatua ambayo ingewafaa wakulima zaidi kuliko vikiuziwa wawekezaji wa kibinafsi huku wengine wakiunga hatua ya serikali viuzwe.

Hali ilivyo kwa sasa ni kuwa wakulima wa miwa, sawa na wa kahawa, majani chai, mahindi, pareto na ngano, mazao ambayo miaka ya awali yalikuwa tegemeo kwa uchumi wa maeneo mbali mbali nchini, wataendelea kuzama katika umaskini kwa kuwa serikali haiwajali.

Yanayoendelea katika sekta hii ni kinyume kabisa na ahadi ya serikali ya kuimarisha kilimo kwa jumla ili nchi iweze kujitosheleza kwa chakula. Sio kwamba Kenya imekosa wataalamu wa kufanikisha ajenda hii mbali ni ukosefu wa nia njema katika utekelezaji wa mikakati wanayobuni.

Haiwezi kusahaulika kwamba msimu wa uchaguzi mkuu wa 2022 umenukia na wanasiasa ambao wamekuwa wakitumia mapato kutoka biashara ya kuuza sukari ya magendo kufadhili kampeni zao, miongoni mwao wanaohudumu wanajiandaa.

Si ajabu basi wakawa miongoni mwa watu wanaoendelea kuingiza sukari licha ya marufuku ya serikali. Ni vigumu kwa mtu asiye na ushawishi wa kisiasa kuingiza sukari nchini bila kukamatwa.

Miaka miwili iliyopita, maelfu ya magunia ya sukari iliyodaiwa kuwa ya magendo yalinaswa maeneo tofauti nchini dhihirisho kwamba kukiwa na nia njema, biashara hii inaweza kukomeshwa na wakulima wa miwa nchini kulindwa.

You can share this post!

Nandwa pazuri kubwaga Shikanda, Odipo na kuwa kocha mpya wa...

GWIJI WA WIKI: Emily Gatwiri