Kifo cha kitambulisho chaja Huduma Namba ikinukia
MARY WAMBUI na WANDERI KAMAU
MUDA wa matumizi ya vitambulisho vya kitaifa miongoni mwa Wakenya utaisha rasmi Desemba 2021, baada ya serikali Jumatano kuzindua utoaji wa kadi ya Huduma Namba.
Akiongoza uzinduzi wa kadi hizo katika Kaunti ya Machakos jana, Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i alisema kuwa mchakato wa kusambaza kadi hizo utaendelea kwa mwaka mmoja, kwa mujibu wa taratibu zilizo kwenye sheria.
Uzinduzi huo pia uliendeshwa sambamba na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia (ICT), Joe Mucheru katika Kaunti ya Kiambu.
Ili kupata kadi hizo mpya, Wakenya watafahamishwa kwa kutumiwa ujumbe mfupi kwenye simu zao kuhusu mahali ambapo wataenda kuzichukua.
Wakenya wataanza kuchukua kadi hizo Desemba 1, 2020.
Waziri alisema kuwa utaratibu huo ni kuhakikisha watu wengi hawakusanyiki katika mahali pamoja, ili kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.
Kwa mujibu wa kanuni hizo, kila Mkenya atakuwa na muda wa mwezi mmoja kuchukua kadi yake baada ya kupokea ujumbe unaomwelekeza atakakoichukua.
Kinyume na vitambulisho vya kitaifa, ambavyo havikuorodheshwa kwa namna yoyote, kadi hizo zitakuwa za aina nne.
Kulingana na Dkt Matiang’i, aina ya kwanza ya kadi hizo itakuwa ya watoto waliofikisha umri wa miaka sita. Aina ya pili itapewa watu wazima, waliofikisha umri wa miaka 18 na zaidi. Aina ya tatu ya kadi hizo itapewa raia wa kigeni huku ya nne ikipewa wakimbizi.
Waziri alisema wanalenga kusajili Wakenya milioni 10 zaidi kwenye duru ya pili, ya usajili huo, iliyopangiwa kuanza Aprili 2021.
“Uzinduzi wa leo Jumatano ni mwanzo wa utaratibu wa kuwafikia Wakenya milioni 10 ambao hawakujisajili katika awamu ya kwanza,” akasema.
Uzinduzi wa jana unajiri wiki mbili baada ya kuapishwa kwa Bi Immaculate Kasssait, kama Kamishna wa Kwanza wa Kusimamia Data.
Jukumu kuu la Bi Kassait litakuwa pia kusimamia Mpango wa Kitaifa wa Kuhifadhi na Kusimamia Maelezo ya Wakenya (Nemis).
Rais Uhuru Kenyatta na mkewe, Bi Margaret Kenyatta ndio waliokuwa Wakenya wa kwanza kupokea kadi hizo wakati wa sherehe za Sikukuu ya Mashujaa katika Kaunti ya Kisii mnamo Oktoba 20.
Rais Kenyatta amekuwa akisisitiza kuwa kadi hizo zitaashiria mwanzo mpya katika maisha ya Wakenya kwa kurahisisha mfumo wa utoaji huduma muhimu, hasa katika afisi za serikali.