Michezo

Salim Babu apokezwa mikoba ya Kisumu All Stars baada ya kutemwa Wazito FC

November 19th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na CHRIS ADUNGO

ALIYEKUWA kocha mkuu wa Western Stima, Salim Babu, amepokezwa mikoba ya kikosi cha Kisumu All Stars kwa mkataba wa mwaka mmoja na kubwa zaidi katika majukumu yake ni kurejesha kikosi hicho hadi Ligi Kuu ya Kenya mwishoni mwa msimu wa 2020-21.

Kuajiriwa kwa Babu kunajiri siku chache baada ya kutimuliwa na mabwanyenye wa Ligi Kuu ya FKF-PL, Wazito FC alikokuwa kocha msaidizi.

Aliagana na kikosi hicho kinachomilikiwa na mfanyabiashara Ricardo Badoer baada ya kufurushwa kwa pamoja na kocha mkuu Fred Ambani na aliyekuwa kocha wa makipa, Elias Otieno.

“Sasa nitakuwa kocha rasmi wa All Stars kwa kipindi cha mwaka mmoja ujao. Nimepewa majukumu ya kurejesha All Stars katika Ligi Kuu ya FKF-PL mnamo 2021-22,” akasema Babu.

“Lengo langu kuu ni kushinda idadi kubwa ya mechi zijazo na kurejesha kikosi kinakostahili kuwa. Timu inajivunia wachezaji wazuri na tutazidi kuimarisha kila idara,” akaongeza.

All Stars waliteremshwa ngazi hadi kwenye Ligi ya Kitaifa ya Supa (NSL) majuma machache yaliyopita baada ya kupokezwa kichapo cha 5-3 na Vihiga United kwenye mchujo wa kufuzu kwa Ligi Kuu ya FKF-PL.

Kuteuliwa kwa Babu kudhibiti mikoba ya All Stars ni pigo kubwa kwa Andrew Aroka ambaye amekuwa akiwatia makali vijana wa All Stars tangu Februari 2020.

Aroka ni miongoni mwa makocha waliotuma maombi ya kazi kwa minajili ya kupokezwa mikoba ya All Stars waliotangaza nafasi ya kazi hiyo mnamo Agosti 2020.

Ratiba

Kwa mujibu wa ratiba mpya ya NSL, All Stars wamepangwa kuvaana na Kibera Black Stars mnamo Novemba 28 katika mechi yao ya ufunguzi wa msimu mpya wa 2020-21.

“Tulipokea idadi nzuri ya barua za maombi kutoka kwa wakufunzi wazawa wa humu nchini na wengine kutoka mataifa ya nje. Bodi ya Usimamizi ya All Stars ilipitia barua hizo kabla ya kuwatathmini walioziwasilisha. Hata hivyo, usimamizi uliamua kumteua Babu,” akasema Nicholas Ochieng ambaye ni Afisa Mkuu Mtendaji wa All Stars.

All Stars almaarufu ‘Blue Eagles’ wanadhaminiwa na Serikali ya Kaunti ya Kisumu. Mbali na kocha mkuu, kikosi hicho kilikuwa kikisaka kocha msaidizi, kocha wa viungo vya mwili na kocha wa makipa. Ni matumaini ya Aroka kwamba sasa atapokezwa mojawapo ya nafasi hizo baada ya Babu kuteuliwa kocha mkuu.

Ochieng amesema kwamba tayari wameanza maandalizi kwa minajili ya msimu ujao na wanasoka wake wana matumaini ya kuibuka washindi wa taji la NSL baada ya kukosa kuhifadhi nafasi yao kwenye Ligi Kuu ya FKF-PL msimu ujao.

“Ingawa wanasoka wetu wamekuwa katika likizo ndefu tangu ujio wa corona, kila mmoja wao amekuwa akishiriki mazoezi kivyake. Tutatumia wiki chache zijazo kujiandaa vilivyo kwa kibarua kilichopo mbele yetu na tuna kila sababu ya kutamba,” akaeleza Ochieng.

Kuvunjiliwa mbali kwa kikosi cha Chemelil Sugar baada ya kuteremshwa ngazi kwa pamoja na SoNy Sugar na All Stars sasa kunasaza Western Stima wakiwa wawakilishi wa pekee wa eneo la Nyanza kwenye FKF-PL msimu ujao wa 2020-21.

Stima waliagana na wanasoka 11 tangu kampuni ya umeme ya Kenya Power iliyokuwa ikiwadhamini isitishe ufadhili. Wengi wa wachezaji hao waliobanduka Stima walisajiliwa na Wazito FC na mabingwa mara 19 wa Ligi Kuu ya KPL, Gor Mahia.

All Stars waliagana rasmi na Jeff Odongo (kocha wa viungo vya mwili) na Fredrick Onyango (kocha wa makipa) walioteuliwa kuhudumu katika benchi ya kiufundi mnamo Februari 2020.

Aroka ndiye afisa aliyewahi kuhudumu kambini mwa kikosi hicho kinachodhaminiwa na Serikali ya Kaunti ya Kisumu kwa muda mrefu zaidi na ndiye aliyechangia kupandishwa ngazi kwa kikosi hicho kushiriki soka ya Ligi Kuu mwanzoni mwa msimu huu wa 2019-20.

Mnamo Januari 2020, All Stars walimtimua aliyekuwa kocha wao wa muda mrefu, marehemu Henry Omino kwa pamoja na aliyekuwa msaidizi wake, Aroka na kocha wa makipa Joseph Ongoro kwa sababu ya matokeo duni ya kikosi.

Hata hivyo, Aroka alirejea baadaye kambini mwa klabu hiyo baada ya Arthur Opiyo aliyeteuliwa kushikilia mikoba ya kikosi hicho kwa muda kurejea Ujerumani kwa mafunzo zaidi ya ukocha.

Mbali na Aroka, wengine ambao walituma upya maombi ya kazi kambini mwa All Stars ni Odongo na Onyango.

“Walikuwa wametia saini mikataba ya miezi michache iliyokatika. Waliwasilisha upya maombi ya kazi kwa minajili ya kuendelea kuhudumu nasi katika benchi mpya ya kiufundi ambayo tunapania kuifichua rasmi mwishoni mwa wiki moja,” akasema Ochieng kwa kusisitiza kwamba walikuwa wakimtafuta kocha mkuu aliye na leseni ya kiwango cha C kutoka kwa Shirikisho la Soka la Afrika (CAF).