• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
NGILA: Nchi za Afrika ziungane kufaidika kiteknolojia

NGILA: Nchi za Afrika ziungane kufaidika kiteknolojia

Na FAUSTINE NGILA

RIPOTI mpya iliyochapishwa majuzi na kampuni ya Google ikishirikiana na Shirika la Ufadhili wa Kimataifa (IFC) kuhusu uchumi wa kidijitali wa Afrika imefichua kuwa bara hili lina uwezo mkubwa kufaidika kiteknolojia.

Ripoti hiyo imeonyesha kuwa katika miaka mitano ijayo, utajiri wa Afrika kutokana na teknolojia utagonga Sh19.5 trilioni na hata Sh77.5 trilioni kufikia mwaka 2050.

Huku bei ya intaneti ikiendelea kupungua katika mataifa kadha barani na kufikia asilimia 40 ya Waafrika wote wapatao bilioni 1.3, bado baadhi ya mataifa yanaonekana kusalia nyuma katika makuzi ya uchumi wa kidijitali.

Kutoka Afrika Kusini hadi Eritrea, Kenya hadi Benin, Tunisia hadi Malawi na Misri hadi Lesotho, mataifa ya Afrika yako katika viwango tofauti vya maendeleo ya kiteknolojia, hali ambayo isipochukuliwa hatua itaongezea mwanya unaoshuhudiwa katika matumizi ya teknolojia.

Huu ni wakati wa mataifa kuungana na kuunda soko moja la mataifa 55 ili kupata ushawishi katika soko la dunia la uchumi wa dijitali. China kwa mfano, ni soko la watu bilioni 1.2, India ni watu bilioni 1.3 huku Amerika, ambayo inaongoza dunia kwa kampuni zenye faida mno ina soko la watu milioni 300.

Ni wazi kuwa mataifa yanayojigamba kuwa na usemi mkubwa kiteknolojia kama Afrika Kusini, Nigeria, Kenya, Ghana au Misri hayawezi kupata ushawishi wa maana duniani iwapo yataingia sokoni kama taifa binafsi.

Dunia ya sasa imewekeza mno katika teknolojia za kisasa ambapo kampuni kama Apple, Amazon na Facebook zinaongoza duniani kwa orodha ya kampuni zenye faida kubwa duniani, hiyo ikiwa ishara kuwa uchumi wa mwongo huu utategemea ubunifu.

Hapa barani, kampuni zote zinafaa kuungana kuunda soko la pamoja ikizingatiwa kwa sasa watu milioni 520 wanapata intaneti ya kasi ya juu, huku ikitazamiwa matumizi ya data kwa kila Mwafrika yataongezeka kutoka GB 1.3 hadi GB 7.3 kufikia 2024.

Ikumbukwe kuwa licha ya kuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kukuza matrilioni ya hela, Afrika badi imesalia chini mno katika soko la kimataifa kutokana na ukosefu wa umoja na ufunguzi wa mipaka kwa biashara baina ya mataifa yake.

Kwa mfano, katika soko la kimataifa la teknolojia za kiotomatiki (AI) ambalo lina thamani ya Sh1.8 kwadrilioni, China na Amerika tayari zinamiliki asilimia 70 ya soko hilo.

Afrika inafaa kujizatiti kupata angalau asilimia 10 ya asilimia 30 iliyobakia, kwa kubuni teknolojia zake za kisasa na kuziuza katika mabara mengine.

Ingawa Umoja wa Afrika (AU) umeanza kutekeleza soko la pamoja kwa jina AfCFTA, ambalo linalenga kuondoa ushuru kwa asilimia 90 katika bidhaa zinazouzwa baina ya mataifa ya Afrika, baadhi ya mataifa kama Tanzania, Afrika Kusini, Libya na Burundi yamesalia kikwazo, yakidinda kufungulia mataifa mengine mipaka au kuwaruhusu watu kutoka mataifa mengine kufanya kazi katika uchumi wao.

Hiki ni kisiki kikuu katika utekelezaji wa mpango huo, ikizingatiwa bara hili lina watumizi wengi zaidi wa teknolojia za kutuma na kupokea hela kwa simu, ambao wanafaa kuunda soko moja dhabiti linaloheshimiwa duniani.

[email protected]

You can share this post!

TAHARIRI: Utata wa Huduma Namba utatuliwe

AWINO: Kilimo cha parachichi kimevutia pato bora kwa...