Michezo

Uholanzi wakosa kufuzu kwa fainali za Nations League licha ya kupepeta Poland

November 19th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MASHIRIKA

LICHA ya kiungo Georginio Wijnaldum kufunga bao mwishoni mwa kipindi cha pili, ushindi wao 2-1 uliosajiliwa na Uholanzi dhidi ya Poland mnamo Novemba 18, 2020 haukuwezesha wanafainali hao wa mwaka wa 2019 kufuzu kwa fainali zijazo za UEFA Nations League mnamo Oktoba 2021.

Kamil Jozwiak aliwaweka Poland kifua mbele katika dakika ya tano kabla ya fowadi wa Olympique Lyon, Memphis Depay kusawazishia Uholanzi katika dakika ya 77 kupitia mkwaju wa penalti.

Wijnaldum ambaye kwa sasa huchezea Liverpool, alifunga bao la pili kwa upande wa Uholanzi mwishoni mwa kipindi cha pili na kuhakikisha kwamba wanaibuka washindi wa gozi hilo.

Hata hivyo, ushindi wa 2-0 ambao Italia walisajili dhidi ya Bosnia-Herzegovina uliwapa Azzurri fursa ya kukamilisha kampeni za Kundi A1 kileleni.

Mabao ya Italia yalifumwa wavuni kupitiwa kwa Andrea Belotti na Domenico Berardi na kuhakikisha kwamba kikosi chao kinaungana sasa na Ubelgiji, Ufaransa na Uhispania kwenye fainali zijazo za UEFA Nations League. Fainali hizo zitaandaliwa mnamo Oktoba 2021.

Japo Uholanzi walishindwa kusonga mbele kwenye kivumbi cha mwaka huu wa 2019, ushindi waliousajili dhidi ya Poland ulikuwa wao pili mfululizo chini ya mkufunzi mpya Frank de Boer aliyemrithi Ronald Koeman aliyeyoyomea Uhispania kudhibiti mikoba ya Barcelona mwishoni mwa msimu uliopita wa 2019-20.

Chini ya Boer, Uholanzi walishindwa kusajili ushindi wowote katika jumla ya mechi nne za kwanza zilizosimamiwa na mkufunzi huyo ambaye pia amewahi kudhibiti mikoba ya Ajax, Inter Milan, Crystal Palace na Atlanta United.