Siasa

Joho apiga kampeni vijijini Msambweni

November 19th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na FADHILI FREDRICK

GAVANA wa Mombasa Ali Hassan Joho ameanza kampeni za nyumba kwa nyumba, katika juhudi za kuhakikisha mwaniaji wa ODM katika uchaguzi mdogo wa eneobunge la Msambweni, ataibuka mshindi.

Bw Joho anaongoza kampeni za Bw Omar Boga kwenye kinyang’anyiro hicho kitakachokamilika kwa uchaguzi hapo Desemba 15.

Kiti hicho kiliachwa wazi baada ya kifo cha mbunge Suleiman Dori mwezi Machi.

Uchaguzi huo umevutia wagombeaji kadhaa miongoni mwao Bw Feisal Bader, ambaye anaonekana kuipa ODM ushindani mkali.

Bw Bader ni mpwa wa Bw Dori, na anagombea kama mwaniaji huru. Aidha, anaungwa mkono na Naibu Rais William Ruto.

Amekuwa akifanyiwa kampeni na washirika wa Dkt Ruto kama vile maseneta wa zamani Hassan Omar (Mombasa), Johnstone Muthama (Machakos) na Dkt Boni Khalwale (Kakamega).

Kinyang’anyiro hicho sasa kinaonekana kuwa ushindani wa kisiasa kati ya Dkt Ruto (mrengo wa Tangatanga) na kinara wa ODM Raila Odinga (mrengo wa Kieleweke).

Akihutubu kwenye mikutano kadhaa kumpigia debe Bw Boga, Bw Joho aliwalaumu wapinzani wao kwa kutumia ukabila kupiga kampeni.

Alionya kwamba Tangatanga ‘wanawachezea’ wenyeji wa Msambweni.

“Msichezee shere maisha ya watu. Wanakumbwa na changamoto nyingi kama kukosa ajira na mizozo ya ardhi,” Bw Joho aliwaambia wakazi.

“Haya yanaweza tu kusuluhishwa kwa kumchagua kiongozi muungwana anayejali maslahi yenu,” aliongeza na kusisitiza kuwa Bw Boga ndiye anafaa zaidi kuwaunganisha watu na kuwaletea maendeleo.

Akaendelea: “Msimpigie kura mwaniaji ambaye hana chama. Je, atapata usaidizi wapi akipatwa na shida? Ikiwa hali hiyo itamkumba Bw Boga atapata usaidizi kutoka kwa Rais Kenyatta, Bw Odinga na maafisa wengine serikalini.”

Naye Bw Boga akijipia debe kama mwaniaji anayefaa zaidi, alisema kuwa kama kiongozi mwenye uzoefu mkubwa ataelekeza juhudi zake katika kuimarisha utalii na uvuvi ili kuboresha maisha ya wenyeji.

“Eneobunge letu limejaaliwa raslimali nyingi. Hivyo, linahitaji kiongozi mwenye maono ambaye atawawezesha nyinyi kuboresha maisha ilio kupiga teke umaskini,” akasema.

Aliahidi kushirikiana na serikali kusaidia wenyeji kwa uwezo wake wote.

ODM inapoendeleza kampeni zake, wawaniaji wengine pia wanaweka kila juhudi kujipigia debe ili kuvutia wapigakura zaidi ya 68,000 wa eneo hilo.

Wawaniaji huru wengine kwenye kinyang’anyiro ni Mansury Kubaka na Bw Charles Bilali.

Walio na vyama ji pamoja na Shee Abdulrahman (Wiper), Marere Wamwachai (NVP), Hassan Mwakulonda (PED na Khamis Mwakaonje (UGM).