Michezo

Sababu za Zarika kubatilisha maamuzi ya kustaafu ndondi na kurejea ulingoni

November 20th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na CHRIS ADUNGO

KABLA ya bondia Fatuma ‘Iron Fist’ Zarika kukubali kuchapana na Yamileth ‘Yeimi’ Mercado wa Mexico katika vita vya kuwania taji la dunia la WBC super bantamweight kwa wanawake, mwanamasumbwi huyo alitekeleza kifungu cha marudiano ya mechi kwenye mkataba wao.

Zarika alikuwa amevaana na Mercado kwenye mchapano wa kwanza mnamo Septemba 8, 2018 jijini Nairobi kabla ya kurudiana mnamo Novemba 16, 2019 mjini Chihuahua, Mexico.

Tangu Zarika apoteze mchuano huo, juhudi zake za kurudiana na bondia huyo wa Mexico hazijazaa matunda.

Zarika, 35, aliyepata kibali cha kushiriki mazoezi katika ukumbi wa Round 10 Boxing Gymnasium jijini Dubai alikokuwa mwelekezi, alikuwa mwingi wa matumaini kwamba fursa hiyo ingalimpa nafasi ya kujiandaa vilivyo kwa marudiano dhidi ya Mercado baada ya kuambulia pakavu nchini Mexico.

Kubisha kwa janga la Covid-19 kulimweka Zarika katika ulazima wa kutafuta makazi Dubai ili amakinikie kazi yake ya kuajiriwa, jambo ambalo lingalimweka nje ya ulingo wa ndondi.

“Juhudi za kupata fursa ya kurudiana na Mercado ziliambulia pakavu baada ya kuzungushwa kwa kipindi kirefu. Isitoshe, ujio wa corona ulitatiza hali,” akasema Zarika ambaye aliamulia kuangika glavu zake ndondi ili amakinikie kazi yake ya kuajiriwa,” akasema Zarika kwa kusisitiza kwamba alifikia mahali ambapo hakutaka hata kidogo kusikia mpango wa kurejea ulingoni kwa minali ya mchezo wa ndondi.

Hata hivyo, ilimchukua Mtanzania Kelvin Twissa ambaye ni mkurugenzi wa Jackson Group zaidi ya mwezi mmoja uliopita kumshawishi Zarika kubatilisha maamuzi yake ya kustaafu na arejee ulingoni kuendelea kushiriki mchezo wa ndondi. Twissa aliwahi kuwa mkuu wa kitengo cha mauzo katika kampuni ya SportPesa jijini Nairobi.

SportPesa waliwahi kudhamini na kusimamia mchuano mkali kati ya Zarika na Mercado, na Twissa akamshawishi Zarika kushiriki ndondi za Dar Night Fight mnamo Novemba 12, 2020 jijini Dar es Salaam, Tanzania.

Awali, mchapano wa uzani wa featherweight kati ya Zarika na Patience Mastara kutoka Zimbabwe ulikuwa usiwe wa kuwania taji lolote na ulistahili kuwa wa raundi nane.

Hata hivyo, Howard Goldberg ambaye ni rais wa Shirikisho la Ndondi Duniani aliidhinisha shindano hilo kuwa la kuwania taji la kimataifa baada ya mshikilizi wa zamani kutolitetea na badala yake kuzamia mapambano ya uzani mwingine tofauti.

Zarika aliibuka mshindi wa mchapano huo uliomkutanisha na Mastara kwa wingi wa pointi kutoka kwa waamuzi.

“Ilichukua muda mrefu kumshawishi Zarika kurejea ulingoni kwa mara nyingine. Nilishangaa sana aliponieleza kwamba alikuwa ameanza kumakinikia masuala mengine tofauti kabisa na ndondi Dubai,” akasema Twissa.

Twissa alisema alimshauri Zarika kufikiria upya kuhusu maamuzi yake ya kustaafu kwenye ulingo wa masumbwi na kumwaminisha kwamba bado ana fursa kubwa ya kurejea kuwa bingwa wa dunia.

“Nilimweleza kuwa hiyo ilikuwa fursa nzuri kwake kurejea ulingoni na atawaliwe zaidi na mawazo ya ushindi badala ya kuongozwa na tama ya pesa,” akasema Twissa kwa kusisitiza kwamba hakuna bondia mwingine anayeorodheshwa kwa kiwango cha juu zaidi barani Afrika kwa sasa kwa upande wa wanawake kuliko Zarika.

Kwa mujibu wa Twissa, Zarika amekuwa kielelezo kwa wasichana wengi barani Afrika tangu aweke rekodi ya kuwa mwanamke wa kwanza kutwaa taji la dunia la WBC na kulitetea mara tatu.

“Zarika bado yuko katika hali shwari ya kimwili, kisaikolojia na kiakili. Angali na miaka mingi ya kutamba ulingoni na kutwaa mataji ya haiba kubwa katika mchezo wa ndondi duniani,” akaongeza Twissa.

Katika mchapano wake na Mastara, Zarika alikuwa akirejea katika ulingo wa masumbwi takriban miezi 12 baada ya kuzidiwa ujanja na Mercado wa Mexico aliyempokonya ubingwa wa taji la dunia la WBC.

Zarika anayejivunia rekodi ya ushindi mara 33 (Knock-out 17) na sare mbili, amewahi kupoteza jumla ya mashindano 13 pekee.

Kwa mujibu wa Franklin ‘Kuja’ Imbenzi ambaye ni Katibu wa Kamati ya Kitaifa ya Wanamasumbwi Wataalamu (KPBC), ndondi hizo za Dar Night Fight zilikuwa zimedhaminiwa na Jackson Group Sports (JGS).

“Shindano la Dar Night Fight lilikuwa la haiba kubwa ambalo lilijumuisha michapano minne tofauti ya kimataifa. Kulikuwa na kategoria mbili za ndondi za wanawake kwenye masumbwi hayo yaliyoleta pamoja mataifa matano tofauti – Argentina, Kenya, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Zimbabwe na wenyeji Tanzania,” akasema Imbenzi katika mahojiano yake na Taifa Leo.

Huku Zarika na Mastara wakishiriki pigano kuu la kitengo cha wanawake, Mtanzania Zulfa ‘Macho’ Yusufu na Alice Mbewe wa Zimbabwe walivaana kwenye mchapano wa raundi sita wa kiwango cha flyweight.

Kwa upande wa wanaume, Abdallah ‘Dulla Mbale’ Pazzy wa Tanzania alipimana ubabe na Alex Kabangu wa DR Congo kwenye pigano la raundi 10 la uzani wa super middleweight.

Mtanzania Hassan Mwakinyo alimenyana na Jose Carlos Paz wa Argentina katika mchuano wa raundi 12 uliowakutanisha mabondia wawili bora zaidi duniani katika uzani wa super-welterweight.

Kelvin Twissa ambaye ni mkurugenzi wa JGS, alisema kwenye mtandao wake wa Twitter: “Tajriba yetu katika masuala ya mauzo na michezo ilitupa jukwaa maridhawa zaidi la kuandaa mojawapo ya mapigano ya haiba kubwa zaidi duniani jijini Dar es Salaam. Mashindano hayo yalifuatiliwa sana nchini Tanzania, Zambia, Zimbabwe, Kenya, DRC na Argentina.”