• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Wanasoka 10 ghali zaidi duniani ambao watakosa fainali zijazo za Euro 2021

Wanasoka 10 ghali zaidi duniani ambao watakosa fainali zijazo za Euro 2021

Na CHRIS ADUNGO

FAINALI zijazo za Euro zilizoahirishwa kutoka mwaka wa 2020 hadi 2021 zitakosa baadhi ya wanasoka chipukizi wa haiba kubwa na masogora wazoefu katika ulingo wa kabumbu.

Hapa tunawaangazia baadhi ya wachezaji ghali zaidi duniani ambao hawatakuwa sehemu ya kampeni hizo baada ya vikosi vyao kukosa kujikatia tiketi za fainali za Euro 2021.

1 – Jan Oblak – Slovenia – Sh11.2 bilioni

Iwapo Oblak angalikuwa mchezaji wa Uingereza au Uhispania, basi angalikuwa kwa sasa kipa bora zaidi duniani akijivunia kuwajibishwa ndani ya jezi za timu ya taifa mara nyingi zaidi.

Lakini kwa bahati mbaya mlinda-lango huyo ni raia wa Slovenia ambao hawajawahi kufuzu kwa fainali za kipute chochote cha haiba kubwa tangu Oblak ayoyomee Uhispania kuwadakika Atletico Madrid baada ya kuagana na Inter Milan alikokuwa kipa chaguo la pili baada ya Samir Handanovic.

2 – Erling Haaland – Norway – Sh10 bilioni

Chipukizi huyu raia wa Norway na fowadi wa Borussia Dortmund bado ana muda mwingi wa kudhihirisha ukubwa wa uwezo wake katika ulingo wa soka ya kimataifa.

Kufikia sasa, Halaand anajivunia jumla ya mabao sita kutokana na mechi saba ambazo amechezea Norway ambao watakosa kunogesha fainali zijazo za Euro 2021 baada ya kuzidiwa maarifa na Serbia kwenye mchujo.

3 – Sergej Milinkovic-Savic – Serbia – Sh8.1 bilioni

Kiungo huyu wa Lazio anahusishwa na uwezekano mkubwa wa kuondoka katika Ligi Kuu ya Italia (Serie A) na kutua Uingereza kuvalia jezi za Manchester United na Chelsea katika Ligi Kuu ya EPL.

Nafasi ya Milinkovic-Savic kudhihirishia dunia utajiri wa kipaji alichonacho akivalia jezi za Serbia kwenye fainali zijazo za Euro ilipotea baada ya timu yake ya taifa kuzamishwa na Scotland kwenye mchujo ambapo mshindi aliamuliwa kupitia mikwaju ya penalti.

4 – Miralem Pjanic – Bosnia – Sh6.3 bilioni

Wachache sana wanafahamu kwamba Pjanic aliwahi kuwakilisha Luxembourg katika kiwango cha wanasoka chipukizi kabla ya kupata uraia wa Bosnia mnamo 2008. Baada ya kuwakilisha Bosnia kwenye fainali zilizopita za Kombe la Dunia za 2018 nchini Urusi, kiungo huyu wa Barcelona atakosa kunogesha kivumbi cha Euro baada ya Bosnia kubanduliwa na Northern Ireland kwenye mchujo.

5 – Martin Odegaard – Norway – Sh5.6 bilioni

Wakijivunia huduma za Haaland na Odegaard, Norway ni miongoni mwa vikosi ambavyo vingepigiwa upatu kutamba zaidi katika fainali zijazo za Euro.

Hata hivyo, 2021 ni mapema sana kwa Odegaard ambaye kwa sasa yuko katika msimu wake wa kwanza kambini mwa Real Madrid, Uhispania kudhihirisha ukwasi wa kipaji chake kwenye ngazi ya kimataifa akiwa sehemu ya kikosi cha Norway.

6 – Filip Kostic – Serbia – Sh3.9 bilioni

Serbia ndilo taifa linalojivunia idadi kubwa ya wanasoka kwenye orodha hii baada ya kupigiwa upatu wa kutawala kampeni zao za mchujo na kujikatia tiketi ya moja kwa moja ya kushiriki Euro.

Kostic ambaye ni fowadi wa Eintracht Frankfurt nchini Ujerumani atakosa kunogesha fainali zijazo za Euro licha ya kutamba na kuishia kuwa tegemeo la Frankfurt kwenye kampeni za Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) hadi kufikia sasa.

6 – Kostas Manolas – Greece – Sh3.9 bilioni

Kikosi cha sasa cha Ugiriki ni cha kiwango cha chini sana kikilinganishwa na kile kilichojitwalia ubingwa wa taji la Euro 2004. Miamba hao waliokuwa wenyeji wa fainali zilizopita za Kombe la Dunia mnamo 2018 waliambulia nafasi ya tatu kwenye Kundi J nyuma ya viongozi Finland kwenye hatua ya makundi, matokeo ambayo yatamnyima beki Manolas wa Napoli fursa ya kushiriki fainali za Euro kwa mara ya kwanza.

8 – Nikola Milenkovic – Serbia – Sh3.5 bilioni

Serbia walishindwa kuhimili ukali wa viwango vya ushindani katika Kundi B la kufuzu kwa fainali za Euro 2021 baada ya kuzidiwa ujanja na Ukraine, Ureno na Scotland waliowabandua kupitia mikwaju ya penalti.

Beki wa Fiorentina, Milenkovic, 23, ni miongoni mwa chipukizi waliopigiwa upatu wa kutamba zaidi katika fainali zijazo za Euro na kuwapa Juventus kila sababu ya kumsajili mwishoni mwa kipute hicho.

9 – Marash Kumbulla – Albania – Sh3.0 bilioni

Albania walishiriki mchuano wa kwanza wa haiba kubwa walipofuzu kwa fainali za Euro 2016 nchini Ufaransa yapata miaka minne iliyopita baada ya kupepeta Romania na kuwalazimishia wenyeji sare kwenye hatua ya makundi.

Beki chipukizi wa AS Roma, Marash Kumbulla, 20, angalikuwa miongoni mwa makinda ambao wangalisisimua zaidi fainali zijazo za Euro iwapo Albania wangalifuzu kwa kivumbi hicho.

10 – Luka Jovic – Serbia – Sh3.0 bilioni

Jovic aliduwaza Scotland baada ya kufunga bao la kusawazisha katika dakika za mwisho na kusababisha mchuano wao wa mchujo kuingia katika muda wa ziada wa vipindi viwili vya jumla ya dakika 30.

Hata hivyo, Serbia walizidiwa maarifa kwenye gozi hilo la kufa-kupona na Jovic ambaye ni kiungo wa Real Madrid nchini Uhispania akakosa fursa ya kuibua msisimko kwenye fainali zijazo za Euro.

You can share this post!

BBI: Kimya chao chazua hofu

Raila atuliza maswali kuhusu alikokwenda baada ya kufichua...