Haaland atwaa tuza ya Golden Boy baada ya kutawazwa Chipukizi Bora wa Mwaka wa 2020
Na MASHIRIKA
FOWADI Erling Braut Haaland, 20, ametawazwa taji la Chipukizi Bora wa Mwaka almaarufu Golden Boy mnamo 2020 kwa kuwa mwanasoka bora zaidi aliye chini ya umri wa miaka 21 miongoni mwa mataifa ya Ligi Kuu katika bara Ulaya.
Nyota huyo raia wa Norway aliibuka mshindi baada ya kuwapiku Ansu Fati wa Barcelona na timu ya taifa ya Uhispania pamoja na beki wa kushoto Alphonso Davies wa Bayern Munich na timu ya taifa ya Canada.
Haaland alifungia Dortmund ya Ujerumani jumla ya mabao 27 kutokana na mechi 29 za mwaka huu wa 2020 kwenye kampeni za Bundesliga.
Fowadi wa Atletico Madrid, Joao Felix alitia kibindoni ubingwa wa taji hilo mnamo 2019.
Chipukizi wengine waliokuwa wakiwania tuzo hiyo mwaka huu ni kiungo Jadon Sancho anayecheza na Sancho kambini mwa Dortmund pamoja na fowadi wa Manchester United, Mason Greenwood.
Wanasoka wa zamani raia wa Uingereza waliowahi kunyakua taji la Golden Boy ni Wayne Rooney mnamo 2004 na Raheem Sterling mnamo 2014.
Mbali na Sancho na Greenwood, Waingereza wengine waliokuwa wakiwania taji la mwaka huu 2020 ni Callum Hudson-Odoi (Chelsea), Phil Foden (Man-City) na Bukayo Saka (Arsenal).
Walikabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa Vinicius Junior (Brazil na Real Madrid), Sergino Dest (Barcelona), Rodrygo Silva (Real Madrid), Jonathan David (Bayern Munich), Ferran Torres (Man-City), Fabio Silva (Wolves), Eduardo Camavinga (Rennes) Mitchel Bakker (PSG), Ryan Gravenberch (Ajax), Dejan Kulusevski (Juventus), Dominik Szoboszlai (Red Bull Salzburg) na Sandro Tonali (AC Milan).
Tuzo hiyo ambayo imekuwa ikidhaminiwa na Tuttosport kwa miaka 17 iliyopita, iko wazi kwa wanasoka wote waliozaliwa baada ya Januari 1, 2000 na ambao wanapigia klabu zinazoshiriki Ligi Kuu tano za bara Ulaya; yaani EPL (Uingereza), La Liga (Uhispania), Serie A (Italia), Ligue 1 (Ufaransa) na Bundesliga (Uhispania).
Wawaniaji wa tuzo hiyo hupigiwa kura na wanahabari 40 kutoka mataifa wanachama wa Shirikisho la Soka la bara Ulaya kutegemea matokeo ya wachezaji husika katika mwaka mzima.