Michezo

Monaco watoka nyuma na kuzamisha chombo cha PSG ligini

November 21st, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MASHIRIKA

AS Monaco walitoka nyuma kwa mabao mawili na kusajili ushindi wa 3-2 uliokomesha rekodi nzuri ya kutoshindwa kwa Paris Saint-Germain (PSG) katika msururu wa mechi nane mfululizo kwenye kampeni za Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) mnamo Novemba 20, 2020.

Mabao yote mawili ya PSG yalifumwa wavuni na fowadi chipukizi Kylian Mbappe aliyekuwa akirejea ugani baada ya kuwa nje kwa kipindi kirefu kutokana na jeraha.

Mbappe aliwafungulia waajiri wake ukurasa wa mabao katika dakika ya 25 kabla ya kufunga la pili dakika 12 baadaye.

Licha ya kuwa chini kwa mabao mawili kufikia mwisho wa kipindi cha kwanza, Monaco walirejea katika kipindi cha pili kwa matao ya juu. Walifungiwa mabao mawili ya haraka kupitia kwa Kevin Volland aliyemwacha hoi kipa Keylor Navas katika dakika za 52 na 65.

Kiungo wa zamani wa Arsenal, Barcelona na Chelsea, Cesc Fabregas alizamisha kabisa chombo cha PSG katika dakika ya 84 kupitia penalti iliyosababishwa na Abdou Diallo aliyeonyeshwa kadi nyekundu.

PSG walitamalaki mchuano huo katika kipindi cha kwanza kilichowashuhudia wakimiliki asilimia kubwa ya mpira huku mabao yao mawili yalifumwa wavuni na Moise Kean na Mbappe yakikataliwa na refa kwa madai kwamba walikuwa wameotea.

Hata hivyo, ujio wa Fabregas katika kipindi cha pili ulibadilisha mkondo wa mechi na Monaco wakajivunia ubunifu na kasi zaidi kwenye safu ya kati na idara ya mbele.

Hadi walipojibwaga ugani kwa gozi hilo la Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1), PSG walikuwa wamefungwa bao moja pekee kutokana na mechi nane za awali. Ingawa hivyo, walishindwa kuhimili ubabe wa Monaco waliotawazwa mabingwa wa Ligue 1 mnamo 2016-17.

Bila ya huduma za nahodha Wissam Ben Yedder anayeuguza Covid-19, Monaco walijipata katika ulazima wa kutegemea kikosi cha chipukizi wengi, wanane kati ya waliounga kikosi chao cha kwanza wakiwa wachezaji wenye umri wa chini ya miaka 23.