Habari

Waislamu nao wakataa BBI

November 23rd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CECIL ODONGO

BARAZA Kuu la Waislamu Nchini (Supkem ) limepinga ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI) na kudai yaliyomo ni kinyume cha yale waliotarajia.

Viongozi wa Supkem walisema ripoti ya BBI jinsi ilivyo kwa sasa ni hatari kwa ugatuzi na itarudisha nyuma zaidi hatua zilizopigwa chini ya katiba iliyopitishwa mnamo 2010.

Msimamo wao umeongeza orodha ya viongozi na makundi ya kijamii ambayo yamejitokeza kupinga kura ya maamuzi kama inavyopendekezwa na BBI.

Makundi mengine yaliyopinga awali ni baadhi ya viongozi wa makanisa, wanasiasa wanaoegemea mrengo wa Naibu Rais William Ruto na mashirika mbalimbali ya kijamii.

Wiki iliyopita, mpango wa kuzindua ukusanyaji wa sahihi milioni moja kuwezesha mswada wa marekebisho ya katiba ulisitishwa ghafla.

Hafla hiyo ilipangiwa kuongozwa na Rais Uhuru Kenyatta na mshirika wake wa handisheki, Raila Odinga ambaye ni kiongozi wa chama cha ODM.

Mwenyekiti wa Supkem, Hassan Ole Naado, alisema Jumapili ripoti ya BBI ikitekelezwa itarejesha utawala wa kiimla wa Urais na akisisitiza haifai kupitishwa jinsi ilivyo kwa kuwa ina mapungufu mengi kisheria.

Punde baada ya ripoti hiyo kutolewa, Supkem iliwateua wasomi wa kisheria na wa dini kuipiga darubini ndipo wakatoa pendekezo la kuipinga Jumapili.

“BBI inarejesha nyuma manufaa yaliyoletwa na katiba ya sasa na inapendekeza kurejeshwa kwa utawala wa kiimla wa Urais pamoja na kudhoofisha zaidi asasi mbalimbali za serikali ambazo utendakazi wao umekuwa mzuri chini ya katiba ya sasa. Kwa hivyo, tunaomba kamati ya BBI iangazie upya mapendekezo yaliyomo kwenye ripoti hiyo. Tunamwomba Rais kama kiongozi wa nchi kusimamisha mchakato wowote wa kupitishwa kwa BBI hadi mapendekezo hayo yaangaziwe upya,” akasema Bw Ole Naado kwenye kikao na wanahabari katika msikiti wa Hurlingham, jijini Nairobi.

Kulingana na Supkem, wananchi walikuwa na matumaini tele wakati Rais na Bw Odinga walipoweka mwafaka wa ushirikiano baada ya uchaguzi wa 2017, lakini matokeo ya BBI sasa yanafifisha matumaini hayo.

Hivi majuzi, Bw Odinga alipuuzilia mbali wanaopinga BBI akisema wanaeneza propaganda, kwani anaamini marekebisho ya katiba yatakuwa kwa manufaa ya nchi.

Aidha, Bw Ole Naado alilalamika kwamba lugha iliyotumika kwenye BBI ni ngumu na ya kitaalamu wala haitaeleweka na Wakenya wengi hata wakipokezwa ripoti hiyo waisome.

Alitaja pendekezo linalomhitaji Rais kumteua Waziri Mkuu kutoka kwa chama kinachojivunia wabunge wengi kama lisiloeleweka na linalokanganya zaidi.

“Iwapo Rais atapata idadi inayohitajika ya kura kisha akose wabunge wengi. Je, Waziri Mkuu atachaguliwa kutoka upinzani atakuwa sehemu ya serikali yake? Hii itakuwa kama uchaguzi wa 2007 ambapo Kibaki alikuwa Rais na idadi ya chini ya wabunge na Raila akawa Waziri Mkuu na wabunge wengi. Serikali hiyo ilijawa na mzozo wa mamlaka,” akaongeza.

Supkem pia inasisitiza kwamba, muundo wa serikali ya mseto unaopendekezwa ni kama ule wa Tanzania ambao hauwezi kutekelezeka nchini.

Kikao hicho kilihudhuriwa na maafisa wa mashirika ya Kiislamu ya NAMLEF, CIPK, NUKEM, KCIU na KIMYA.

Pia walitaja kuangaziwa upya kwa mipaka ya maeneobunge ambapo 27 ya sasa yataondolewa kama njama ya kuzipokonya jamii ndogo nafasi ya uwakilishi na kupendelea zile kubwa.

“Maeneo yatakayoathirika tayari yametengwa kihistoria. Kwa sasa maendeleo kiasi yanaonekana maeneo hayo kupitia hazina ya CDF. Ni wazi hapa nchini kwamba ukifuta eneobunge basi pia maendeleo yanapungua au kutoweka. Hata wadi zikiongezwa na kupewa hazina yao, maeneo pekee yatakayonufaika ni yale yenye watu wengi,” akasema.

Kuhusu IEBC, Supkem inapinga makamishina kuteuliwa kutoka kwa vyama vya kisiasa tena kwa mkataba wa miaka minne pekee. Baraza hilo lilisisitiza kuwa, makamishina hao watapigania tu matakwa ya wakuu wa vyama vyao kwenye Tume hiyo kisha kuondoka baada ya kuzua mgogoro zaidi kuhusu uwazi kwenye uchaguzi mkuu.

Baraza hilo pia linapinga mawaziri kuchaguliwa kutoka kwa wabunge wakisema hilo linazua suala la mgongano wa kimajukumu.