Makala

TALANTA: Mwanadada aliyezamia katika muziki, uchezaji densi, uanamitindo na uigizaji

November 23rd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na WANDERI KAMAU

JE, unajua kwamba talanta ni nguzo kuu inayoweza kumfikisha mtu mbali akiamua kuipalilia tangu mwanzoni?

Naam, hiyo ndiyo simulizi ya mwanadada Syniniah Bosibori kutoka Kaunti ya Nyamira, ambaye anatamba kwa sasa katika fani za uanamitindo, uchezaji densi, uimbaji na uigizaji sinema.

Mwanadada huyo, ambaye ana umri wa miaka 22 pekee, anavuma kwa kibao ‘Nakubaliana’ ambacho kilitungwa mwanzo na mwanamuziki maarufu Gloria Muliro.

Anasema aliamua kuachilia kibao hicho kwanza kama “jaribio” la kuona vile mashabiki wake wangempokea.

“Nina nyimbo nyingi ambazo tayari nimezirekodi na natarajia kuziachilia siku kadhaa zijazo. Ingawa mimi bado ni mwanamuziki anayechipukia, nawaahidi mashabiki wangu kutegea uhondo kamili,” akasema mwanadada huyo kwenye mahojiano na ‘Taifa Dijitali.’

Akiwa mzaliwa wa Kaunti ya Nyamira, Syniviah alisomea katika Shule ya Msingi ya Nyaimao, ambapo baadaye alielekea katika Shule ya Upili ya Gisage.

Baada ya hapo, aliendeleza masomo yake katika Taasisi ya Elgonview, katika Kaunti ya Kisii, alikosomea masuala ya Utalii na Uhusiano Mwema.

Utotoni mwake, alikuwa akivutiwa sana na uchezaji densi, jambo alilotamani kulifanya sana ukubwani mwake.

“Nilianza uchezaji densi kitambo sana; nikiwa katika shule ya msingi. Niliendelea hata baada ya kujiunga na shule ya upili. Hapo ndipo niligundua kwamba ni talanta niliyokuwa nayo,” akasema.

Hata hivyo, alijitosa kwenye tasnia hiyo kirasmi mwaka 2020.

“Nimeitwa katika hafla kadhaa za kuwatumbuiza watu na kushiriki kwenye video za wanamuziki ijapokuwa bado ninajikakamua kupenya zaidi. Si rahisi kwa mabinti kufaulu katika tasnia ya burudani bila kujituma. Inahitaji bidii, nidhamu na kujituma kwa kiwango cha juu,” asema.

Katika tasnia ya muziki, amekuwa akitazama mwanamuziki King Sande, ambaye hutumbuiza kwa lugha ya Kikisii, anayemtaja kuwa miongoni mwa watu waliomkuza sana kwenye safari ya kupalilia talanta zake.

“Ni muhimu sana kuwa na mtu unayemtazama na anayekupa mwongozo kuhusu njia utakayofuata katika tasnia hii ya burudani. Mwanamuziki huyo amekuwa nguzo kubwa kwangu kwani ana tajriba ya miaka mingi kwenye sekta hii,” akasema.

Majuzi, mwanadada alishiriki kwenye mashindano ya kumtafuta mwigizaji na mwanamitindo bora, yaliyoandaliwa na kampuni ya Glightlakes jijini Nairobi.

Kampuni hiyo huhusika katika kuwatafuta na kuwakuza wanamitindo, waigizaji na waandishi wa michezo ya kuigiza.

“Kwenye shindano hilo, washiriki walihitajika kuwarai mashabiki wao kuwapigia kura ili kuibuka washindi. Ingawa sikuibuka mshindi, niliorodheshwa kuwa miongoni mwa washiriki kumi bora,” asema.

Anaeleza hilo limemfungulia nafasi, kwani ameitwa kushiriki kwenye senema kadhaa.

Katika safari yake changa, changamoto kuu ambazo amekumbana nazo ni ukosefu wa fedha za kutosha. Anasema kuwa wakati mwingine, mtu anaweza kuitwa kushiriki kwenye hafla fulani lakini akakosa kufika kwa kukosa njia za usafiri.

Anasema taratibu za kuandaa video pia hugharimu fedha nyingi, hali ambayo huwa changamoto kwake ikizingatiwa bado hajapata ajira rasmi.

Licha ya changamoto hizo, lengo lake kuu ni kuikuza fani ya burudani nchini, kwa kubuni jukwaa ambalo litawakuza wanamuziki, wachezaji densi na wanamitindo wanaochipukia.

“Nchi yetu ina vijana wengi waliojaaliwa vipawa vingi ila huwa wanakosa nafasi za kujikuza. Lengo langu kuu ni kubuni kampuni ambayo jukumu lake kuu litakuwa kuwatambua na kuwakuza wasanii wanaochipukia,” akasema.

Anawashauri wasanii chipukizi kujituma, kumweka Mungu mbele na kutoangalia nyuma kwenye safari zao katika usanii, kwani hiyo ndiyo njia pekee watakavyotimiza ndoto zao.