• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 1:29 PM
ODONGO: Ubinafsi wa ODM kubana hela za vyama vya kisiasa

ODONGO: Ubinafsi wa ODM kubana hela za vyama vya kisiasa

Na CECIL ODONGO

HATUA ya chama cha ODM kukataa kumegea vyama tanzu kwenye Muungano wa NASA fedha za vyama vya kisiasa haifai ikizingatiwa ushirikiano uliokuwepo kati yao kwenye uchaguzi wa 2017.

Hii ni kwa sababu Ford Kenya, Amani National Congress na Wiper zilichangia pakubwa zaidi ya kura milioni 6.8 alizopata Kinara wa ODM Raila Odinga kwenye duru ya kwanza ya uchaguzi wa urais mwaka huo.

Wiki jana, Msajili wa vyama vya kisiasa Anne Nderitu alieleza kamati ya Bunge kwamba vyama hivyo tanzu haviwezi kupata mgao wowote wa Sh4 bilioni kutoka kwa serikali, pesa zote zikielekezwa katika hazina ya ODM. Sehemu ya fedha hizo ni za miaka ya 2016 na 2017 ambapo ODM hazikuzipokea na ikawasilisha kesi kortini.

Wakati huo vyama hivyo vilikuwa kwenye muungano wa CORD.

Bi Nderitu alisisitiza kuwa ingawa hoja inayosema vyama hivyo vingenufaika na mgao wa ODM ipo kwenye makubaliano ya muungano huo, ufafanuzi haukutolewa jinsi pesa hizo zingegawiwa kati ya vyama vyote vinne.

ODM nayo imekuwa ikishikilia kwamba hataitoa hata senti kwa vyama vingine vya NASA, ikisisitiza kuwa umaarufu wake ndio ulihakikisha inanufaikia hela hizo.

Uchoyo huu wa ODM hata hivyo unafaa kuwa kifungua macho kwa chama chochote kinachoingia kwenye muungano na kingine kabla au hata baada ya uchaguzi. Chama hicho kinafaa kuhakikisha mfumo wa mgao wa fedha za vyama vya kisiasa zinazotolewa na serikali unabainishwa

Lau viongozi wa Ford Kenya, ANC na Wiper wangemakinikia hilo, hawangekuwa wakililia pesa hizo ambazo sasa ni bayana hawatazipata.

Kwanza, si siri kwamba ODM imedhihirisha kiburi na inatumia mwanya uliopo kwenye makubaliano ya muungano kuvinyima vyama hivi vitatu haki ya kunufaikia hela hizo.

Pili, ni bayana kuwa vyama hivyo hasa Wiper katika ngome zake ilipigia Bw Odinga kura nyingi zaidi ikilinganishwa na alizopokea kutoka kwa ngome za Ford Kenya na ANC

Ingekuwa vyema iwapo muungano huo ungeafikiana kuwa ODM itenge hata asilimia 30 za fedha hizo na kuzigawia kwa Wiper, ANC na Ford Kenya kisha isalie na asilimia 70 badala ya kuziacha mikono mitupu.

Vyama hivyo vitatu navyo vinafaa vijikakamue kwenye uchaguzi wa 2022 ili vishinde idadi kubwa ya viti vya ubunge ndipi vihitimu kupokea mgao wao wa fedha za vyama kutoka kwa serikali kuu.

Katika mwaka huu wa kifedha ni ODM na Jubilee ambazo zimetengewa Sh240 milioni na Sh515 milioni kwa kuwa vilishinda viti 76 na 140 mtawalia vya ubunge mnamo 2017.

Wiper (19), Ford Kenya (10) na ANC (12) vote vilishinda viti vya jumla 41 vya ubunge pekee.

La mno ni kwamba vyama hivi vianze kuweka mikakati ya kuvishinda Citi vingi kwenye uchaguzi wa 2022 ili vifaulu kupata mgao wa fedha za vyama vya kisiasa.

Kwa upande mwingine ODM, imeonyesha kwamba si mshirika mwema na chama chochote kinachoshirikiana nao kabla ya uchaguzi, kinafaa kuwa makini kisije kikarukwa baada ya kura.

Kwa upande mwingine inashangaza kuwa Wiper, Ford Kenya na ANC haviwezi kupata viti 20 vya ubunge, vitatu vya useneta na ugavana na madiwani 40 ili vinufaikie fedha hizo moja kwa moja badala ya kusumbua ODM inayoamini inakula jasho lake.

Hii ni licha ya viongozi wao Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi na Moses Wetang’ula kudai kila mara kwamba vyama hivyo ni vikubwa na tayari hata wametangaza azma ya kuwania Urais mnamo 2022.

You can share this post!

Lukaku na Sanchez wasaidia Inter Milan kutoka nyuma na...

Biden kutaja baraza lake la mawaziri Jumanne