Habari

Mkondo mbaya Kenya watoto 44 wakinaswa mtaani Mountain View wakishiriki ulevi, ngono

November 23rd, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

MWANAMKE Millicent Muthoni Kithinji aliyekamatwa mtaani Mountain View ambapo matineja 44 walikuwa wakishiriki anasa nyumbani kwake wikendi, Jumatatu amewasilishwa katika Mahakama ya Milimani na maafisa wa Idara ya Uchunguzi wa Makosa ya Jinai (DCI) wakitaka yeye na washirika wake watatu wazuiliwe kwa siku saba.

Watoto 44 ambao ni wanafunzi wa shule walikamatwa usiku wa kuamkia Jumapili katika mtaa huo wakibugia pombe na kuvuta bangi.

Maafisa wa DCI walisema 26 kati yao walikuwa wavulana na 18 wakiwa wasichana. Wote ni wenye umri wa kati ya miaka 14 na 17 wakiwa wanafunzi wa shule za msingi na upili.

“Mwanamke ambaye aliwaalika watoto hao katika nyumba hiyo pia amekamatwa,” DCI ilisema kupitia Twitter.

Idara hiyo ilisema uchunguzi unaendelea kubaini sababu iliyopelekea mwanamke huyo kuwaalika watoto nyumbani kwake.

“Kwa mara nyingine, DCI inawaomba wazazi kufuatilia kwa makini mienendo ya watoto wao nyumbani na katika mitandao ya kijamii. Adhabu kali itachukuliwa dhidi ya watu wazima ambao hudhulumu watoto,” DCI ikaonya.

Kukamatwa kwa watoto hao kunajiri baada ya DCI kufichua kuwa kuna genge la majambazi ambao hutumia mitandao ya kijamii kuwavutia wasichana na kuwaalika katika aina mbalimbali za karamu.

Katika kisa kingine, wapelelezi wa kitengo cha kupambana na wahalifu sugu (SCU) Jumamosi, Novemba 21, 2020, waliwakamatwa maafisa wawili wa polisi wa utawala ambao wamekuwa wakiwapunja watu pesa wakijifanya kuwa maafisa kutoka Mamlaka ya Kusimamia Mazingira (NEMA) na ile ya kusimamia sekta ya kawi (EPRA).

Wawili hao, Benson Njoroge Mburu na Justus Mwangi Macharia pamoja na mwanamume mmoja kwa jina Duncan Njogu Mukono walikamatwa baada ya kukusanya kiasi kisichojulikana cha pesa kutoka kwa watu wasio na habari.

Maafisa hao wanahudumu katika afisi za kaunti ndogo za Kiambu na Modagashe, mtawalia.

Walifaa kufikishwa mahakamani leo Jumatatu na kufunguliwa mashtaka kwa mujibu wa sehemu 382 ya sheria ya uhalifu.