• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 10:06 AM
WASONGA: Kenya iombe msamaha wa madeni ili ijifufue kiuchumi

WASONGA: Kenya iombe msamaha wa madeni ili ijifufue kiuchumi

Na CHARLES WASONGA

WIKI jana kwa mara nyingine, taifa hili liliwapoteza madaktari wawili wenye haiba kubwa, Profesa Anthony Were Omollo na Dkt Nira Patel waliofariki kutokana na ugonjwa wa Covid-19.

Hawa ni miongoni mwa zaidi ya wahudumu wa afya 30 ambao wameuawa na homa hiyo huku wengine zaidi ya 2,000 wakiambukizwa virusi vya corona tangu Machi 13 maka huu.

Inakera kuwa miongoni mwa sababu zinazochangia visa vya wahudumu wa afya kuambukizwa ni ukosefu wa vifaa vya kijikinga (PPEs) vyenye ubora hitajika katika hospitali za umma, miongoni mwa mahitaji mengine, walivyosema viongozi wa vyama vya kutetea masilahi ya wahudumu hao.

Mwenyekiti wa Baraza la Magavana (CoG) Wycliffe Oparanya wiki jana alifichua ongezeko la visa vya maambukizi miongoni mwa wahudumu wa afya linachangiwa na sababu kwamba serikali za kaunti hazina fedha za kununua PPEs.

Hii ni kwa sababu Hazina ya Kitaifa haijasambaza fedha kwa kaunti tangu mwezi wa Septemba licha ya kusuluhishwa na mvutano miongoni mwa maseneta kuhusu mfumo wa ugavi wa fedha kwa kaunti.

Kinaya ni wiki jana, Waziri wa Fedha alikana ripoti kwamba Serikali ya Kenya imefilisika na kwamba inahitaji msamaha wa ulipaji wa madeni ya kima cha Sh75.5 bilioni kutoka kwa mataifa 20 tajiri ulimwenguni (G20).

Sikubaliani kabisa na kauli ya Waziri Yatani. Ikiwa serikali imeshindwa kusambaza sehemu ya mgao wa fedha kwa kaunti katika miezi ya Septemba, Oktoba na Novemba, mtawalia basi imefilisika. Ikiwa serikali haiwezi kununua PPEs na kugharimia bima ya afya kwa wahudumu wa afya katika ngazi za kitaifa na kaunti, basi sio makosa kusema kuwa imefilisika.

Kenya itapoteza madaktari na wahudumu wa afya wangapi ndipo serikali ipambazukiwe na ukweli kwamba imekuwa filisi na inapasa kuomba msaada kutoka na mataifa tajiri na mashirika ya kifedha ulimwenguni?

Nafahamu fika kwa Waziri Yatani amefahama athari za kuungama kwake kwamba Kenya imefilisika kwa kutokana na athari za kiuchumi ambazo tangazo kama hizo litasababisha. Athari za kwanza zitakuwa kudorora kwa thamani ya sarafu ya Kenya dhidi ya zile za kimataifa na hatari ya mali ya nchi kama vile Bandari na Viwanja vya Ndege na Mashirika ya Serikali kutwaliwa na wadeni wetu kama vile China.

Kwa hivyo, Serikali inapasa kupiga moyo konde na kuwasilisha ombi kwa mataifa wanachama wa G20 ili ulipaji wa madeni ya kima cha Sh75.5 bilioni uahirishwe hadi pale uchumi utaanza kuimarika baada ya kudhibitiwa kwa janga la corona

Serikali pia iwasilishe ombi kama hilo kwa nchi zinazoidai kama vile China na mashirika ya kimataifa ya kifedha kama vile Benki ya Dunia (WB).

You can share this post!

KAMAU: Vijana wazinduke sasa kuzikomboa jamii zao

Matokeo mseto kwa wanasoka wa Kenya wanaocheza ligi za...