• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
Mfanyakazi wa zamani wa shirika lisilo la kiserikali aeleza anavyopenda kuimarisha jamii

Mfanyakazi wa zamani wa shirika lisilo la kiserikali aeleza anavyopenda kuimarisha jamii

Na SAMMY WAWERU

BI Elizabeth Mutuku alihudumu katika Shirika moja lisilo la kiserikali (NGO) kati ya mwaka wa 2003 hadi 2018, ambapo anakiri alitekeleza miradi mingi ya maendeleo.

Jitegemee Children’s Program, ni Shirika lenye afisi zake Machakos na linalojituma kuangazia changamoto zinazokumba mayatima na wasiojiweza katika jamii.

Katika kipindi cha muda wa miaka 15 mfululizo aliyohudumu katika shirika hilo, Elizabeth ambaye ni mama wa watoto watatu anajivunia jitihada zake kuimarisha jamii, hasa familia zilizokuwa zimelemewa na ufukara na kupitia bidii alizotia chini ya ufadhili wa Jitegemee Children’s Program, nyingi yazo zimeweza kujiimarisha.

“Ni fahari ya mama kuona familia inaishi maisha bora. Ninapokutana na niliosaidia kujiimarisha, hushukuru Mungu niliokoa maisha, si ya mtu mmoja au wawili, ila familia nzima,” asema Elizabeth.

Kando na kuhamasisha jamii miradi muhimu kuwekeza kwa njia ya mafunzo bila malipo, Elizabeth anasema shirika hilo pia lilipiga jeki walioonekana kutokuwa na uwezo kifedha.

Aidha, Programu ya Jitegemee inalenga maeneo ya Mashariki mwa Kenya, mengi yakiwa ni yanayolemewa na makali ya ukame na kiangazi.

Kuna hiki kisa cha familia ya watu 10, 8 wakiwa watoto, ambacho kingali kibichi katika kumbukumbu za Elizabeth Mutuku.

“Ulikuwa mwaka wa 2016, katika mojawapo ya majukumu yetu. Kijiji cha Misakwani, Kaunti ya Machakos, tulisaidia kuimarisha familia hiyo iliyokuwa imekata tamaa na kupoteza matumaini maishani,” anaelezea mama huyo mcheshi na mkwasi wa utu.

Kulingana na Elizabeth, baba na wavulana wake wanne walikuwa mateka wa pombe, dawa za kulevya na mihadarati.

Binti mmoja alipata ujauzito akiwa angali mchanga kiumri, na kwa bahati mbaya mimba ikaharibika (miscarriage).

Kulingana na Elizabeth, mahangaiko hayo yalichangiwa na umaskini uliotawala familia hiyo, mama akiwa ndiye tegemeo pekee kuikithi riziki na mahitaji mengine muhimu ya kimsingi.

“Baada ya kutathmini hali, ufukara ndio ulichochea. Baba alikuwa mlevi kupindukia kiasi cha kutogundua bintiye alipata mimba, na kijusi akafa,” anafafanua.

Endapo familia hiyo ingehamasishwa kuhusu miradi bora kuingilia, ili ijitegemee kupitia hela kidogo waathirika walikuwa wakielekeza kwa mgema, changamoto ilizopitia zingeepukika.

Ni kisa kilichogusa moyo wa Elizabeth na kuhisi wajibu aliompa Mwenyezi Mungu kuimarisha jamii, ulihitajika kwa hali na mali katika familia hiyo.

“Kama mama niliona ikiwa mama huyo angekuwa na shughuli inayomuingizia mapato, angesimamia familia yake,” anasema.

Elizabeth anadokeza kwamba chini ya ufadhili wa Jitegmee Children’s Program, mama huyo alisajiliwa katika programu inayohamasisha miradi bora ya maendeleo, na ambapo alichagua ufugaji wa kuku.

Mmoja wa wavulana wake, naye akapelekwa katika kituo cha maadili na kurekebisha tabia. “Kilele kikawa kuwanunulia kuku na baada ya muda mfupi, ufugaji huo ukageuka kuwa chanzo cha mapato,” Elizabeth anasimulia, akithibitisha kuwa mama na mvulana wake walisaidia kunusuru baba na waliotekwa kwenye minyororo ya pombe na dawa za kulevya.

“Familia hiyo sasa ni kielelezo katika kijiji cha Misakwani,” anaeleza.

Kabla kuamua kuacha kazi kwa hiari katika shirika hilo lisilo la kiserikali mnamo 2018, ili kufanya kikamilifu ufugaji wa kuku, Elizabeth, 43, alikuwa amezuru nchi jirani ya Uganda kupitia semina, na anasema kinachofanya taifa hilo kuwa la kipekee katika ubora wa ufugaji kuku ni mikakati iliyowekwa na serikali na jitihada za mashirika yasiyo ya kiserikali kuinua wakulima.

“Kenya tuna uwezo na raslimali za kutosha, na tunahitaji mkono wa serikali na mashirika hususan yasiyo ya kiserikali kuinua jamii ili tuondoe umaskini,” anahimiza mama huyo, ambaye hutumia mradi wake wa kuku kupiga jeki vijana na kina mama.

Serikali imezindua utoaji wa mikopo kwa vijana na kina mama ili kujiendeleza kimaisha, ila taratibu na mikakati iliyowekwa kuipata ni kibarua.

“Kupata mikopo inayodaiwa kusambazwa na serikali kwa vijana na kina mama si rahisi. Nimejaribu mara kadhaa bila mafanikio,” analalamika Peter Irungu, mfanyabiashara.

Mkondo wa Jitegemee Children’s Program ukiigwa na serikali na mashirika mengine yasiyo ya kiserikali, sawa na mwigo wa Elizabeth Mutuku baada ya kuacha kazi kwa hiari, huenda suala la ukosefu wa kazi na mdahalo wa kuondoa ufukara katika jamii ukaangaziwa.

 

You can share this post!

Gor Mahia yateua kocha Sammy ‘Pamzo’ Omollo wa...

Dereva wa lori lililoanguka Viwandani aokolewa