Rekodi ya Gor Mahia katika CAF Champions League kabla ya kuvaana na APR ya Rwanda
Na CHRIS ADUNGO
GOR Mahia wanatarajiwa Jumamosi kushuka dimbani kuvaana na APR ya Rwanda kwenye mchujo wa gozi la Klabu Bingwa Afrika (CAF Champions League) katika uwanja wa Amahoro jijini Kigali.
Miamba hao wa soka ya humu nchini watakuwa wakipania kusajili matokeo yatakayowawezesha kutinga hatua ya makundi ya kipute hicho kwa mara ya kwanza chini ya kipindi cha misimu mitano iliyopita.
Matumaini yao ya kusonga mbele mwaka jana yalizimwa na USM Alger ya Algeria iliyowabandua kwa jumla ya mabao 6-1 baada ya kichapo cha 4-1 ugenini na 2-0 ugani MISC Kasarani kwenye mchuano wa mkondo wa pili mnamo Septemba 2019.
Gor Mahia walirejea kwa soka ya CAF mnamo Februari 2017 ambapo walipangwa kuvaana na Leones Vegetarianos ya Equatorial Guinea katika raundi ya kwanza ya mchujo. Waliambulia sare ya 1-1 ugenini kabla ya kusajili ushindi wa 2-0 nyumbani.
Ufanisi huo uliwapa tiketi ya kuchuana na Esperance ya Tunisia mnamo Machi 2018 ambapo walibanduliwa kwa bao 1-0 baada ya kuambulia sare tasa katika mkondo wa kwanza jijini Nairobi.
Kichapo hicho kiliwafanya kushushwa ngazi kushiriki michuano ya Kombe la Mashirikisho (CAF Confederations Cup) ambapo walipangwa kukutana na SuperSport United ya Afrika Kusini kwenye mchujo.
Walifuzu kwa hatua ya makundi kwa kanuni ya wingi wa mabao ya ugenini (2-2) baada ya kusajili ushindi wa 1-0 nyumbani kabla ya chombo chao kuzamishwa kwa kichapo cha 2-1 ugenini katika uwanja wa Lucas Moripe.
Walitiwa baadaye katika Kundi D kwa pamoja na Yanga SC ya Tanzania, USM Alger ya Algeria na Rayon Sports ya Rwanda. Gor Mahia ambao ni mabingwa mara 19 wa Ligi Kuu ya Kenya, waliambulia sare ya 1-1 dhidi ya Rayon Sports, wakapoteza 2-1 dhidi ya USM Alger kabla ya kupepeta Yanga 3-2.
Hata hivyo, kichapo cha 2-1 dhidi ya Rayon waliokuwa wakinolewa na kocha Roberto Oliveira ambaye kwa sasa anawafunza Gor Mahia, kilizamisha matumaini ya miamba hao wa Kenya kusonga mbele kwa hatua ya robo-fainali. Hii ni baada ya Rayon Sports kujizolea alama moja muhimu dhidi ya USM Alger ugenini na kusonga mbele kutoka Kundi D.
Safari ya Gor Mahia kwenye CAF Champions League mnamo 2018 ilianza kwa ushindi dhidi ya Nyasa Big Bullets ya Malawi. Katika mkondo wa kwanza, walisajili ushindi wa 1-0 uwanjani Kasarani kabla ya Big Bullets kusajili matokeo sawa na hayo wakati wa marudiano. Mshindi wa mechi hiyo aliamuliwa kwa mikwaju ya penalti ambapo kipa Boniface Oluoch alipangua makombora mawili na kusaidia Gor Mahia kuibuka na ushindi wa 4-3.
Matumaini ya Gor Mahia kusonga mbele kwenye Champions League mnamo Disemba 2018 yalizimwa ghafla na Lobi Stars ya Nigeria waliowapiga 2-0 kwenye mchuano wa raundi ya pili ya mchujo.
Austin Ogunye na Alimi Sikiru walifungia Lobi Stars katika mechi ya marudiano baada ya Gor Mahia kusajili ushindi wa 3-1 nyumbani wakati wa mechi ya mkondo wa kwanza.
Kwa mara nyingine, Gor Mahia walishuka ngazi hadi mechi za Confederation Cup na wakapangwa pamoja na New Star de Doula ya Cameroon kwenye mchujo.
Baada ya kushinda 2-1 nyumbani, walilazimisha sare tasa jijini Doula na wakafuzu kwa hatua ya makundi. Katika Kundi D, walipigwa 2-1 ugenini na Petro Atletico ya Angola, 1-0 na NA Hussein Dey ya Algeria na 4-0 dhidi ya SC Zamalek ya Misri.
Hata hivyo, walifaulu kufuzu kwa robo-fainali baada ya kupepeta Zamalek 4-2, Hussein Dey 2-0 na Petro Atletico 1-0 nyumbani. Licha ya kusonga mbele, Gor Mahia walipokezwa kichapo cha mabao 5-1 ugenini na Renaissance Sportive de Berkane ya Morocco wlaiowacharaza 2-0 nyumbani.
Mnamo 2019-20, Gor Mahia waliwapepeta Aigle Noir ya Burundi 5-1 nyumbani baada ya kuambulia sare tasa ugenini jijini Bujumbura.