• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 11:13 AM
KAMAU: Kenya ijifunze kutatua shida kwa mataifa yaliyostawi

KAMAU: Kenya ijifunze kutatua shida kwa mataifa yaliyostawi

Na WANDERI KAMAU

NCHI nyingi ambazo zimekuwa zikifurahia uthabiti wa kisiasa duniani hazikufikia hatua hiyo kwa njia rahisi.

Nyingi zina historia ndefu, chungu na yenye simulizi za kutamausha.

Baadhi zilifikia hatua hiyo baada ya kukumbwa na maafa na umwagikaji damu wa kuogofya.

Mfano halisi Amerika, Urusi, Ujerumani, Rwanda kati ya mataifa mengine.

Simulizi ya Amerika inafanana na mtoto anayesoma kwa shida nyingi lakini anapata mafanikio kwenye maisha yake ya baadaye.

Licha ya kupata uhuru wake mnamo 1776 na kutazamwa kama mojawapo ya nchi zenye kiwango cha juu zaidi cha demokrasia, nusura uthabiti huo uvurugike kati ya 1861 na 1877, baada ya baadhi ya majimbo yake kutaka kujitenga.

Majimbo hayo ni yale yaliyo katika eneo la Kusini.

Ulikuwa wakati mgumu kwa Amerika. Ni hatua iliyomfanya Rais Abraham Lincoln kuwaruhusu Waamerika wenye asili ya Kiafrika kujiunga na jeshi la taifa hilo ili kuyakabili majimbo ambayo yalitaka kujitenga.

Licha ya vita hivyo, Amerika iliweza kusuluhisha tofauti zake kisiasa chini ya Mpango Mpya wa Ujenzi wa Taifa.

Mpango huo ulichochewa sana na hasara iliyosababishwa na vita hivyo.

Kwa sasa, Amerika ni baadhi ya mataifa yanayochukuliwa kuwa kielelezo chema cha demokrasia duniani, licha ya changamoto za hapa na pale ambazo zimekuwa zikiiandama.

Nchini Urusi, enzi ya Vita Baridi (1947-1990) ndio ilitoa nafasi kwa ustawi wake mkubwa kiuchumi na kisiasa.

Ujerumani nayo hurejelea kuanguka kwa Ukuta wa Berlin mnamo 1989 kama tukio lililoweka ukurasa mpya katika siasa zake.

Kwa muda mrefu, uwepo wa ukuta huo ulikuwa ishara ya mgawanyiko mkubwa kati ya Ujerumani Mashariki na Ujerumani Magharibi; kwani ziliegemea mifumo tofauti ya kisiasa.

Kama Amerika, Ujerumani ni baadhi ya nchi zenye uthabiti mkubwa zaidi kisiasa na kiuchumi duniani.

Urejeleo huu mrefu unafuatia mdahalo mpya ambao umeibuka nchini, kuhusu ikiwa ni vizuri kurejelea upya kesi za ghasia zilizotokea baada ya uchaguzi tata wa 2007/ 2008 au la.

Mdahalo huu unafuatia tangazo la Mkurugenzi wa Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI), Bw George Kinoti, Jumatatu, kwamba idara imepokea malalamishi kutoka kwa baadhi ya Wakenya kuwa wanatishiwa kuondoka wanakokaa na kurejea ‘makwao’ ielekeapo 2022.

Ni tangazo ambalo limezua hisia kali, hasa miongoni mwa wafuasi wa Naibu Rais William Ruto, wakisema mkakati huo ni “njama za kuzima nia yake kuwania urais 2022.”

Bila shaka, hizi si simulizi zinazopaswa kuwa vinywani mwetu wakati kama huu ambapo baadhi ya nchi zinajadiliana kuhusu mikakati ya kukita chumi zao kwa mfumo wa usasa duniani.

Imefikia wakati Kenya ijifunze kutoka kwa mataifa kama Rwanda, ambayo yamefanikiwa kusuluhisha tofauti zake zote za kisiasa.

Tulipaswa kusuluhisha tofauti hizi mara tu baada ya kesi za ghasia za 2007/2008 kukamilika katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).

Ingawa hili halimaanishi walioathiriwa wasipate haki, tunajirudisha nyuma kutumia tofauti za jadi kuamua mielekeo yetu kisiasa kila uchaguzi mkuu unapokaribia.

[email protected]

You can share this post!

DAISY: Tuzae watoto tunaoweza kumudu mahitaji yao ya...

Wabunge watoa ufafanuzi kuhusu tarehe ya mazishi ya Murunga