• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 12:15 PM
Familia ya Safari Rally yaomboleza kifo cha Nagin Chouhan

Familia ya Safari Rally yaomboleza kifo cha Nagin Chouhan

Na ABDUL SIDI

MRATIBU wa zamani wa mbio za magari za kifahari za Safari Rally, Nagin Chouhan atapewa heshima za mwisho Jumamosi.

Mwenyeji huyo wa mji wa Nanyuki atachomwa moto katika makaburi ya Kariokor baada ya kuaga dunia Novemba 24 akiwa na umri wa miaka 85.

Kabla ya kifo chake, Nagia alisumbuliwa na matatizo ya kiafya uzeeni mwake yaliyofanya alazwe katika hospitali ya Aga Khan alikokuwa kwa majuma kadhaa.

Mwanaye wa kiume Hitesh Chouhan, ambaye ni mkazi wa London nchini Uingereza, anatarajiwa kufika Nairobi kwa shughuli hiyo muhimu.

Akizungumza kutoka London, Hitesh alisema, “Nasikitika kupoteza babangu. Alilazwa kwa muda mrefu katika hospitali ya Aga Khan ambako nilikuwa nimemtembelea majuzi tu. Nasubiri kupata cheti cha kuonyesha sina virusi vya corona kabla ya nisafiri,” aliambia mwandishi huyu kwa njia ya simu.

Hitesh mwenyewe aliwahi kuhusika katika mashindano mengi ya mbio za magari za kitaifa za Kenya (KNRC) kama mwelekezi pamoja na katika mbio za magari za Pearl of Africa nchini Uganda, ambazo ni moja ya duru zinazowaniwa kwenye Mbio za Magari za Afrika.

Nagin alifanya kazi miaka mingi na mkuu wa zamani wa Safari Rally, Bharat Bhardwaj kuimarisha fani hiyo aliyoipenda sana.

Mbali na Safari Rally, Nagin pia alikuwa anapenda sana kukusanya miundo mbalimbali ya magari ya zamani. Alitambuliwa na mashindano ya urembo ya magari ya zamani na pikipiki almaarufu Concours d’Elegance, ambayo huvutia maelfu ya watu kila mwaka katika uwanja wa Ngong Racecourse.

Nagin pia alifanyia kazi Idara ya Wanyapori Kenya (KWS) na Kamati ya Kodi ya Mapato baada ya kuteuliwa katika wadhifa huo na Rais wa pili wa Kenya, Daniel Toroitich arap Moi.

Alifanya kazi pia katika benki ya Barclays na alikuwa muhimu katika benki hiyo kufungua matawi kadhaa kaskazini mwa nchi kabla ya kujitosa kwenye biashara miaka ya mwisho ya ‘70. Nagin pia alipenda kucheza mpira wa gofu.

Kupitia ushauri wake, Nanyuki ilianza kuandaa mbio za magari za Clubman kabla ya kupandishwa ngazi na kuwa moja ya duru za KNRC.

Nanyuki Rally (awali Mount Kenya Rally) ilifanyika chini ya klabu ya michezo ya Nanyuki ikisimamiwa na Nagin Chouhan kama mwenyekiti wa eneo la Mlima Mkenya wa Safari Rally iliyokuwa kwenye ratiba ya dunia (WRC).

Kati ya 1986 na 1997, mbio za magari za Nanyuki zilikuwa katika daraja ya pili ya Clubman. Zilijumuishwa katika KNRC kwa mara ya kwanza kabisa mnamo Agosti 29, 1998 wakati Jonathan Toroitich “JT” (mtoto wa Rais Moi) aliibuka mshindi akiendesha gari la aina ya Toyota Celica.

Familia ya Chouhan ilichangia pakubwa katika ukuaji wa mbio za magari katika eneo la Laikipia. Mwanawe wa kike Sonal aliwahi kutumikia Nanyuki Rally kama afisa wa uhusiano mwema naye Hitesh alikuwa mshiriki na pia mwandalizi.

Nagin alianza kujishughulisha na mbio za magari za Safari Rally za Afrika Mashariki ikielekea miaka ya mwisho ya ‘50, miaka michache baada ya Safari kutawazwa.

Aliyekuwa rais wa Kenya Mwai Kibaki alimpa Nagin tuzo ya heshima ya OGW kwa kazi yake ya wema na uhifadhi wa mazingira katika eneo la Laikipia.

Imetafsiriwa na Geoffrey Anene 

  • Tags

You can share this post!

Moto wateketeza mali ya thamani kubwa Githurai

TAHARIRI: FKF isaidie klabu kupata udhamini