• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
MUTUA: Uhuru kama kiongozi astahili kutulia raia wanapomkebehi

MUTUA: Uhuru kama kiongozi astahili kutulia raia wanapomkebehi

Na DOUGLAS MUTUA

NILIWAHI kuandika kwenye safu hizi kwamba, wananchi wanapaswa kuruhusiwa watukane viongozi wao ikiwa msongo wa mawazo umewazidia, hasa wakiwa na nyakati ngumu kimaisha.

Niliandika hayo wabunge fulani walipolaumiwa na hata kukamatwa kwa madai kuwa walimtusi Rais Uhuru Kenyatta na mamake mzazi, Bi Ngina Kenyatta.

Sikupendekeza kuwe na utovu wa nidhamu katika jamii. La hasha! Wakati huo, nilihoji kuwa asiyevumilia kutukanwa au kupigwa vijembe na raia hapaswi kuthubutu kushiriki shughuli za umma au kuwa kiongozi. Hata sasa ninaamini hivyo.

Uongozi na maisha ya umma hutaka moyo wa chuma. Na bila shaka ukitaka kuandika sheria dhidi ya matusi, hutawahi kumaliza kazi hiyo kwa maana matusi mapya yanaibuka kila siku pamoja na sababu zake.

Sisi ni Waafrika, watu tunaoamini kwamba, adabu mtu hufunzwa na mamake tangu mwanzo, hivyo si rahisi jamii nzima iwe ya matusi matupu, eti hiyo iwe desturi.

Leo watakutusi wewe, kesho mwenzako, kesho-kutwa wajidhihaki au kujicheka wenyewe kwa sababu maisha ni gurudumu linalobingiria kufululiza, nayo mazingira yakibadilika.

Mbona nimerejelea mada hii? Haikosi unajiuliza. Kisa na maana ni kwamba, hivi majuzi Rais Kenyatta alipuuzilia mbali kwa jeuri na dharau mitandao ya kijamii.

Ilikuwa wakati wa uzinduzi wa shughuli ya ukusanyaji wa sahihi kwa minajili ya kujiandalia kura ya maamuzi kuhusu ripoti ya maridhiano (BBI).

Kiongozi wa nchi alisema aliondoka kwa vishindo kwenye mitandao hiyo kwa sababu kila kukicha akitukanwa na wananchi.

Aliashiria kuwa waliosalia humo wanapiga ubwete, au pengine wanafurahia utundu unaoendelea mle, kitu ambacho mwanzo kilinichekesha sana kisha nikatafakari: Nilijiuliza: kumbe Uhuru, mwana wa mwanzilishi wa taifa, hajajifunza chochote tangu iwe wazi kwamba hatakuwa na ukiritimba wa kuheshimiwa kama aliojaribisha kuwa nao babake?

Ukibarikiwa kuwa hai wakati huu ambapo teknolojia imerahisisha utandawazi, sharti ukubali kwamba huwezi kujifungia chumbani ukose uchangamano kwa kuogopa vijembe.

Huu ni wakati wa kupendeza; mchunga kondoo asiye na miaka 18 akiwa kijijini Kacheliba anaweza kujadiliana kitu na rais wa Amerika akiwa ndani ya Ikulu ya White House!

Wasipoelewana, kijana wa watu anaweza kutema tusi au aseme kitu kitakachochukuliwa kama kumkosea heshima kiongozi wa taifa tajiri na lenye nguvu za kijeshi zaidi duniani.

Hutarajii Rais huyo atume vifaru vya kivita na mizinga mizitomizito hadi kijijini Kacheliba kumsaka kijana mtundu wala kuondoka miandaoni kwa fujo!

Enzi hii ambapo mtu anaweza kukutusi kwa raha zake tu na ukose la kumfanyia, uwe rais au raia, siri ni kupiga moyo konde na kumpuuza. Kugura mtandaoni si dawa. Ni ishara ya woga na moyo mwepesi.

[email protected]

You can share this post!

WASONGA: Wanasiasa sasa wapunguze joto la kisiasa kuhusu BBI

FUNGUKA: ‘Nimezoea vya kunyonga…’