Michezo

Pigo Everton baada ya beki tegemeo Digne kupata jeraha la kumweka nje kwa miezi mitatu ijayo

November 28th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MASHIRIKA

BEKI matata wa Everton, Lucas Digne, atasalia nje ya uwanja kwa kipindi cha miezi miwili au mitatu ijayo baada ya kupata jeraha baya la kifundo cha mguu akishiriki mazoezi uwanjani Goodison Park mnamo Novemba 27, 2020.

Mfaransa huyo mwenye umri wa miaka 27 anatarajiwa kufanyiwa upasuaji mnamo Novemba 30, 2020.

Kocha mkuu wa Everton, Carlo Ancelotti amesema kuumia kwa Digne ni pigo kubwa kwa kampeni za Everton ambao ni “miongoni mwa wagombezi halisi wa taji la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu wa 2020-21.”

“Ni mchezaji wa haiba kubwa ambaye ni miongoni mwa mabeki bora zaidi wa kushoto duniani. Jeraha alilolipata litatulemaza na kutikisa uthabiti wetu katika safu ya ulinzi,” akasema mkufunzi huyo raia wa Italia.

Everton kwa sasa wanashikilia nafasi ya sita kwenye msimamo wa jedwali la EPL kwa alama 16, nne zaidi nyuma ya viongozi Tottenham Hotspur na Liverpool.

Kutokuwepo kwa Digne kutampisha sasa chipukizi Niels Nkounkou, 20, aliyetua ugani Goodison Park mnamo Julai 2020 baada ya kuagana na kikosi cha Olympique Marseille nchini Ufaransa.

Mtihani mkubwa zaidi kwa Nkounkou ni kutekeleza majukumu makubwa ya kudhibiti safu ya nyuma ya Everton katika michuano mikali ijayo dhidi ya Chelsea, Arsenal, Manchester City na Leicester City kwenye EPL kisha robo-fainali ya Carabao Cup dhidi ya Manchester United.