• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 5:41 PM
Obiri atamalaki mbio za nyika mjini Machakos

Obiri atamalaki mbio za nyika mjini Machakos

Na CHRIS ADUNGO

BINGWA wa dunia katika mbio za nyika, Hellen Obiri alianza kampeni zake za msimu huu kwa matao ya juu baada ya kuibuka mshindi wa mbio za kilomita 10 katika duru ya kwanza ya Riadha za Nyika zilizoandaliwa na Shirikisho la Riadha la Kenya (AK) mjini Machakos mnamo Novemba 28, 2020.

Obiri ambaye pia ni bingwa wa dunia katika mbio za mita 5,000 alichukua uongozi wa mapema baada ya kilomita tatu pekee. Hii ni baada ya kumpiku Beatrice Chepkoech ambaye ni bingwa wa dunia katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na vidimbwi vya maji na kuibuka mshindi kwa dakika 32:29.2.

Baada ya Chepkoech ambaye pia ni mshikilizi wa rekodi ya dunia katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji kujiondoa baada ya kilomita sita pekee, Caroline Nyaga wa Kenya Ploce aliambulia nafasi ya pili baada ya dakika 32:46.8.

Mkenya raia wa Bahrain, Winfred Mutile ambaye pia hushiriki fani ya kilomita 3,000 kuruka viunzi na vidimbwi vya maji, aliridhika na nafasi ya tatu baada ya dakika 32:47.5.

“Barabara ilikuwa telezi baada ya mvua kubwa kunyesha majira ya asubuhi. Hata hivyo, huu ulikuwa mwanzo mzuri kwa kampeni za msimu huu hasa ikizingatiwa kwamba najiandaa pia kwa Michezo ya Olimpiki jijini Tokyo, Japan,” akasema Obiri.

Obiri ambaye aliibuka mshindi wa nishani ya fedha katika mbio za mita 5,000 kwenye Olimpiki za 2016 jijini Rio, Brazil, amesema kwamba ataamua iwapo atashiriki fani zote mbili za mita 5,000 na mita 10,000 kwa sambamba jijini Tokyo, Japan. Michezo hiyo ya Olimpiki itaandaliwa kati ya Julai 23 na Agosti 8, 2021.

“Kwa kuwa mbio za Nyika za Dunia za 2022 zimeahirishwa, sasa nitapania zaidi kujiandaa kwa Olimpiki,” akasema Obiri.

You can share this post!

Pigo Everton baada ya beki tegemeo Digne kupata jeraha la...

Liverpool wadandia kilele cha jedwali la EPL kwa kutoka...