Michezo

Mtihani mgumu kwa Gor katika CAF baada ya kuzamishwa 2-1 na APR katika mkondo wa kwanza

November 28th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

MABINGWA watetezi na washindi mara 19 wa Ligi Kuu ya Kenya, Gor Mahia, sasa wana kibarua kigumu cha kusonga mbele katika kampeni za CAF Champions League msimu huu wa 2020-21.

Hii ni baada ya kikosi hicho kuanza vibaya kampeni zao za kuwania taji hilo la Klabu Bingwa Afrika kwa kichapo cha 2-1 kutoka kwa Armee Patriotique Rwandaise Football Club (APR) ya Rwanda mnamo Novemba 28, 2020.

Gor Mahia almaarufu K’Ogalo sasa wanahitaji ushindi wa angalau bao moja kwa nunge dhidi ya APR katika mechi ya marudiano mnamo Disemba 5, 2020 ili kufuzu kwa mechi za raundi pili jijini Nairobi kwa kanuni ya bao la ugenini.

Mshindi wa michuano hiyo ya mikondo miwili atakutana ama na El Nasr ya Libya au mabingwa wa Algeria, CR Belouizdad.

Wenyeji APR walitangulia kuona lango la Gor Mahia katika dakika ya 10 mnamo Novemba 28 kupitia kwa Sefu Niyonzima kabla ya Gor Mahia kusawazisha mambo kupitia kwa beki Charles Momanyi dakika 18 baadaye.

Bao la Gor Mahia liliwapa APR motisha ya kurejelea kampeni za kipindi cha pili kwa matao ya juu na presha ambayo walielekezea wageni wao ilizaa matunda katika dakika ya 60 baada ya beki Andrew Juma kujifunga.

K’Ogalo walisimamiwa jijini Kigali na mkufunzi wa Posta Rangers, Sammy ‘Pamzo’ Omollo katika mechi hiyo kwa sababu

Kocha mkuu wa Gor Mahia, Roberto Oliveira kutoka Brazil alipigwa marufuku na Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) kusimamia michuano ya kimataifa inayoendeshwa na shirikisho hilo.

Kiini cha marufuku hayo ni kuwa Oliveira hana cheti cha leseni ya kiwango cha CAF A au Uefo Pro ambacho ni cha msingi kwa mkufunzi yeyote anayeongoza kikosi kwenye michuano ya CAF Champions League.

Katika kipindi cha pili, timu hizo zilikuwa sawa na sasa zote bado zina nafasi ya kufuzu raundi ya kwanza kutegemea matokeo ya mechi ijayo.

Matumaini Gor Mahia kusonga mbele katika CAF Champions League mnamo 2019 yalizimwa na USM Alger ya Algeria iliyowabandua kwa jumla ya mabao 6-1 baada ya kichapo cha 4-1 ugenini na 2-0 ugani MISC Kasarani kwenye mchuano wa mkondo wa pili mnamo Septemba.

Gor Mahia walichuana na APR kwa mara ya mwisho mnamo 2014 kwenye hatua ya makundi ya kipute cha Cecafa Kagame Cup na kuambulia sare ya 2-2 nchini Rwanda.

Mechi ya Novemba 28 kati ya Gor Mahia na APR ilikutanisha miamba hao wa Kenya na fowadi wao wa zamani, Jacques Tuyisenge aliyesajiliwa na APR mnamo Septemba 2020 kutoka Petro de Luanda ya Angola.

Hadi alipoyoyomea Angola mnamo Agosti 2019, Tuyisenge alikuwa amevalia jezi za Gor kwa misimu mitatu na kuwaongoza kutwaa mataji matatu ya Ligi Kuu ya Kenya.

Gor Mahia ambao waliagana na wanasoka 15 walipania kutegemea pakubwa huduma za sajili wapya 16 waliojiunga nao muhula huu kwa minajili ya kampeni hizo za CAF.

Kubanduliwa mapema kwa Gor Mahia katika mchujo wa CAF Champions League msimu wa 2019-20 kuliwashusha ngazi hadi CAF Confederation Cup ambao walidenguliwa na DC Motema Pembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa magoli 3-2.

Gor Mahia walinyanyua taji la kimataifa la Afrika mnamo 1987 walipocharaza Esperance Sportive de Tunis ya Tunisia na kutwaa ubingwa wa Mandela Cup. Walitinga robo-fainali za Caf Confederation Cup kwa mara ya kwanza mnamo 2018.

KIKOSI CHA GOR MAHIA:

Makipa: Bonface Oluoch, Gad Mathews.

Mabeki: Geoffrey Ochieng, Michael Apudo, Philemon Otieno, Kelvin Wesonga, Charles Momanyi, Joachim Oluoch, Andrew Juma.

Viungo: Ernest Wendo, Bertrand Konfor, Kenneth Muguna, Bernard Ondiek, Cliffton Miheso, John Macharia, Samuel Onyango.

Wavamizi: Nicholas Kipkirui, Tito Okello