• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
OMAUYA: Kitumbua cha Sonko kimeingia mchanga, itakuwaje?

OMAUYA: Kitumbua cha Sonko kimeingia mchanga, itakuwaje?

Na MAUYA OMAUYA

GHAFLA bin vuu! Kumetokea maandiko kwenye ukuta wa siasa wa Mfalme wa Nairobi, Gavana Mike Sonko, “Mene Mene Tekeli na Peresi.”

Maandiko kama hayo yalipomjia Mfalme Belshsaza wa Biblia, aliambulia katika kaburi la sahau. Tafakari.

Miungu wakiamua kukuumbua na kukuangamiza, kwanza wanakugeuza kichaa. Hayo ndio yamempata Gavana wa Nairobi Mike Mbuvi Sonko kufuatia hoja ya kumng’oa mamlakani juma hili.

Katika hali hiyo, amekuwa haambiliki. Kila hatua yake hivi karibuni imekuwa ya kutapatapa kutoka kikaangoni kwelekea motoni.

Kitumbua chake kimeingia mchanga na badala ya masikitiko, masaibu yake yanaibua mchanganyiko wa hisia kuwa huu ni mwiba wa kujidunga, hauambiwi pole. Mashaka yanayomkabili Sonko yanatokana hasa na udogo wa hekima katika utendakazi wake.

Historia ya Sonko kwenye siasa ni kitendawili na kichekesho. Nyota ya jaha imeangaza mkondo wake tangua alipojitwalia madaraka ya eneo bunge la Makadara.

Kwa mienendo, mitindo ya mavazi na mabunda ya manoti alifaulu kuteka nyoyo na mawazo ya wapiga kura hasa vijana na baada ya Makadara wakamteua kuwa Seneta na hatimaye Gavana wa jiji kuu. Alipanda ngazi ya ukuu kwa kasi iliyoshangaza wengi.

Vivyo hivyo, uongozi wake ukazidi kwa sarakasi, kashfa na mizengwe iliyodunisha mno hadhi ya cheo chake katika jamii. Aliongoza jiji la Nairobi kama kioski chake binafsi. Miradi mingi aliyozindua ilitekelezwa sio kufuatana na mikakati sahihi ya ustawi wa mji bali kulingana na mvuto wa hisia zake na maelekezo ya kundi lake la Sonko Rescue Team.

Wakati mwingi amejitambulisha na hohehahe wa mabanda akiwapa mahitaji muhimu kama vyakula na maji, kuwalipia huduma za afya, kuwasaidia katika shughuli za mazishi ya wapendwa na kadhalika. Haya yote anasema ni kutoka kwa mfuko wake binafsi na wingi wake wa ukarimu.

Tatizo kuu ni kuwa huwezi kuongoza jiji la watu zaidi ya milioni tano ambao wengi ni maskini kwa ukarimu wa aina hii.Huwezi kuwafaidi wavuvi kwa kuwapatia samaki nao hawaoni bahari. Wanajua kuvua, wapeleke ziwani au baharini.

Taswira ya kipenzi cha maskini na ukarimu wa Sonko unakera hisia zaidi ukizingatia ameshtakiwa kwa ufisadi, ubadhirifu na ufujaji wa raslimali za umma. Ufisadi ndio chanzo kikuu cha umaskini nchini.

Licha ya hitilafu alizokuwa nazo katika usimamizi wa jiji, Sonko alipata afueni kwa muda mrefu kwa sababu alifahamu pa kukimbilia kisiasa. Amekuwa mwandani wa Rais Uhuru Kenyatta na ushabiki wake umemwepusha mawimbi makali ya siasa.

Hata hivyo, hivi majuzi, ujeuri wa kinywa chake umemfika hata Rais. Mawimbi yamegeuka. Yaelekea Uhuru amechoka kutetea mtoto mkaidi ambaye pindi tu akishiba mlo, anatapika kwenye sinia.

[email protected]

You can share this post!

TAHARIRI: Watumiao barabara wawe waangalifu

ODONGO: BBI: Tukumbatie maoni tofauti bila kuvuruga nchi