ODONGO: BBI: Tukumbatie maoni tofauti bila kuvuruga nchi
Na CECIL ODONGO
NI dhahiri kwamba huenda mchakato wa kutia saini stakabadhi za ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI) unaoendelea, ukazua mgawanyiko zaidi nchini kati ya mirengo pinzani.
Gavana wa Nandi, Bw Stephen Sang tayari amewasha moto kuhusu suala hilo, akiwataka wanaoendeleza mchakato wa kupata saini za Wakenya, wasifike katika Kaunti yake, akisema hakuna anayeunga mkono shughuli hiyo.
Isitoshe, Bw Sang ambaye ni mwandani wa Naibu Rais Dkt William Ruto, aliapa kuwa atasambaratisha hafla za ukusanyaji wa saini za raia katika Kaunti hiyo kwa kuwa wakazi wanapinga BBI.
Matamshi kama haya hata hivyo hayafai kutoka kwa viongozi wa hadhi ya Bw Sang enzi hizi ambapo Kenya imepiga hatua kidemokrasia na maoni kinzani yanakubaliwa kuhusu masuala mbalimbali kwenye mawanda ya kisiasa.
Ni kweli kwamba viongozi wanaopinga ripoti hiyo pamoja na makundi mbalimbali ya kidini kama Baraza la Waislamu Nchini (Supkem) wana hoja zenye mashiko ambazo hazifai kupuuzwa vivi hivi.
Kati ya hoja ambazo zimekuwa zikitajwa sana ni kuongezwa kwa maeneobunge 70 na Kenya kuwa na wajumbe zaidi ya 400 iwapo BBI itapitishwa. Idadi hii kwa kweli ni ya juu mno na itamgharimu mlipa ushuru hela nyingi kukimu mishahara ya viongozi hao.
Japo kupinga si kosa na ni haki ya kila mmoja kidemokrasia, matamshi kama aliyoyatoa Gavana Sang huenda yakachangia visa vya ghasia hasa kati ya wafuasi wa mirengo miwili.
Kwa upande mwingine, wanaovumisha ripoti ya BBI nayo hawafai kuwasawiri wanaoipinga kama wasiotambua handisheki kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Kinara wa ODM, Bw Raila Odinga.
Kuungwa mkono kwa ripoti hiyo na vigogo wa kisiasa kama Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi (ANC) na Moses Wetang’ula wa Ford Kenya, haimaanishi kwa ripoti ya BBI ndiyo itamaliza matatizo yote hapa Kenya.
Huenda hata viongozi hawa ambao wametangaza watakuwa debeni tayari wanaotea nyadhifa zingine kama za uwaziri mkuu, manaibu wake wawili na kile cha makamu wa Rais.
Isitoshe, si siri kwamba wakati wa hafla ya uzinduzi wa BBI yenyewe mrengo wa Dkt Ruto ulitengwa na kuzua maswali iwapo wanaohusika wana makinikia kuwaunganisha Wakenya jinsi wanavyodai.
Wadadisi wa kisiasa mara nyingi wamewakumbusha Wakenya kwamba matokeo ya kura ya maamuzi ya 2005 kwa namna moja au nyingine yalichangia vurugu kutokea kwenye ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007.
Hii ni kwa sababu mrengo wa ‘NO’ ulioangusha rasimu ya Katiba iliyopendekezwa ulishirikiana hata kwenye uchaguzi huo ukiwa na imani haungeshindwa ndiposa kukatokea ghasia baada kuyakataa matokeo.
Kwa hivyo, huenda hata ukusanyaji wa saini na kura ya maoni inayonukia ikatumiwa na vigogo wa kisiasa kupima umaarufu wao na matokeo yake kuwapa imani ya kushinda kura ya 2022.
Kila mwanasiasa aruhusiwe kuuza ajenda zake wala shughuli za ukusanyaji wa saini isitumike kugawanya baadhi ya maeneo.