WHO: Vita dhidi ya malaria visipuuzwe kipindi hiki cha janga la Covid-19
Na MASHIRIKA
GENEVA, Uswisi
IDADI ya vifo vinavyotokana na ugonjwa wa malaria baada ya kuvurugwa kwa huduma za kupambana nao, inazidi idadi ya wale waliofariki kutokana na Covid-19 barani Afrika, Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) limesema.
Zaidi ya watu 409,000 ulimwenguni, wengi wao wakiwa watoto katika nchi kadha maskini Afrika, walifariki kutokana na malaria mwaka 2019, WHO ilisema katika ripoti yake ya hivi punde.
Shirika hilo linasema kuwa janga la Covid-19 litafanya idadi ya vifo kutokana na malaria kuwa juu zaidi mwaka huu wa 2020.
“Ukadiriaji wetu ni kwamba kwa kutegemea kiwango wa kuvurugwa kwa mipango na mikakati ya kupambana na malaria hasa kufuatia mlipuko wa corona, kuna uwezekano mkubwa kwamba ugonjwa wa malaria uliua zaidi ya watu 100,000 barani Afrika, wengi wao wakiwa watoto,” Pedro Alsonso, Mkurugenzi wa Mpango wa Malaria katika WHO, akawaambia wanahabari jijini Geneva, Uswisi.
“Kuna uwezekano mkubwa kwamba vifo kutokana na malaria ni vingi kuliko vile ambavyo vilisababishwa na Covid-19, moja kwa moja,” akaongeza.
Kulingana na ripoti hiyo ya WHO jumla ya visa 229 milioni vya malaria viliripotiwa kote ulimwenguni mnamo 2019.
Hata hivyo, inasema kuwa licha ya changamoto zilizosababishwa na Covid-19 mataifa mengi duniani yamekuwa yakiendeleza vita dhidi ya malaria.
“Lakini ufanisi katika kuzima kabisa malaria ulimwenguni bado hautapatikana,” ikaongeza ikiongeza kuwa “hii ni licha ya juhudi ambazo zimefanywa katika vita dhidi ya ugonjwa huu tangu mwaka wa 2016.”
Kwa kuwa malaria – yanayosababishwa na Plasmodium; viini vinavyobebwa na aina fulani ya mbu, ripoti hiyo inaeleza, takriban nusu ya idadi ya watu ulimwenguni wanakabiliwa na hatari ya kuambukizwa ugonjwa huo.
“Malaria huua mtoto mmoja kila baada ya dakika mbili,” WHO inakariri.
Licha ya hali hii, ufadhili wa ulimwenguni umeelekezwa kwa ugonjwa wa Covid-19, hali inayofifisha matumaini ya kupungua kwa idadi ya vifo kutokana na malaria.
Mkurugenzi wa Hazina ya Ulimwengu (Global Fund) kupambana na Ukimwi na HIV, ugonjwa wa mapafu (TB) na malaria, Bw Peter Sands alisema matokeo kwenye ripoti ya WHO yamejiri “wakati ufaao”.
“Huduma za kiafya ulimwenguni, vyombo vya habari na siasa zimejikita katika Covid-19 ilhali tunapuuza ugonjwa wa malaria ambao huua zaidi ya watu 400,000 kila mwaka, haswa watoto,” akawaambia wanahabari katika kikao hicho.
“Na niwakumbushe kwamba huu (Covid-19) ni ugonjwa ambao hatujui jinsi ya kupambana nao,” akasema Dkt Sands.
Kulingana na takwimu kutoka kwa Wizara ya Afya ya Kenya, takriban watu 40,000 walifariki kutokana na ugonjwa wa malaria nchini Kenya mnamo 2019.