Makala

AKILIMALI: Kibao-mbuzi ni aina mpya ya mbuzi ambayo inaweza kutumika kwa urahisi hata na watu wenye ulemavu

December 1st, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na DIANA MUTHEU

JAPOKUWA alizaliwa katika familia ya maseremala, George Mulatya Mutinda, 30, hakuchagua kufanya kazi ya useremala kabisa.

Kwa miaka mingi amekuwa akijipatia riziki kutokana na kazi zingine, akiwa miongoni mwa machale – wacheshi – tajika mjini Mombasa akitambulika kwa jina la matani la Sharobaro Katana.

Hata hivyo, anasema janga la corona lilimlazimu kurejelea useremala, ujuzi aliojifunza kutoka kwa babake, ili kujisitiri na makali ya madhara yaliyoletwa na kuwepo kwa virusi vya corona humu nchini.

George anasema kuwa mnamo Aprili, alianza kutengeneza mbuzi za kukunia nazi ambazo zina viti vyake, ili kuwasaidia wakunaji kustareheka wanapotengeneza tui.

“Mbuzi ni kifaa ambacho kinatumika pakubwa eneo la Pwani. Wazo langu lilikuwa ni kuvumbua mbuzi ambayo inaweza kuwarahisishia kina mama kazi ya kukuna nazi, au mtu yeyote ambaye anafanya kazi hiyo kama biashara,” akasema George alipokuwa akizungumza na Akilimali, huku akiongeza kuwa kwa ushirikiano na ndugu yake, Bw Stephen Musyoki Mutinda, wameweza kufanikisha wazo hilo kwa kuwa wanapenda vitu vya kipekee.

Katika sehemu yao ya kufanyia kazi za useremala maarufu PM Workshop, iliyoko eneo la Karama-Kongowea, Kaunti ya Mombasa, utawapata George na Stephen wakitengeneza mbuzi hizo pamoja na bidhaa zingine za nyumba kama vile makabati, vitanda, meza na viti.

Wikendi iliyopita, walikuwa wanajitahidi kutengeneza mbuzi 20 za aina hiyo walizoagizwa na wateja wao.

George Mulatya, 30, na nduguye Stephen Musyoki wakionyesha kibao-mbuzi ambacho wametengeneza. Picha/ Diana Mutheu

George anaelezea kuwa kibao-mbuzi kinahusisha kiti kifupi kwa jina kibao kinachounganishwa na meno ya kifaa cha kukunia nazi ambacho kimepigiliwa katika kipande cha mbao.

“Mbuzi hii imeshikana na kibao. Baada ya kukuna nazi yako, utaondoa mbuzi hiyo kisha uendelee kuketi kwa kile kibao na kukamilisha mapishi yako au kazi za pale jikoni, bila kulazimika kutafuta kiti kingine,” akasema George.

Akaeleza: “Tunaelewa kuwa miili yetu ni tofauti, kuna watu wembamba na wengine wanene. Mbuzi zetu ni za aina tatu ikiwemo; ndogo, ya wastani na pana zaidi ambayo inaweza kukaliwa na mtu mwenye unene wa aina yoyote.”

George anaongeza kuwa katika harakati ya kuvumbua kibao-mbuzi, walizingatia swala la kuwa kuna watu wenye ulemavu ambao hutumia kifaa hicho.

“Kina mama wenye ulemavu wa miguu wanaweza kutumia kibao-mbuzi, na baada ya kukamilisha shughuli za kukuna nazi, watahitajika kuitoa mbuzi, kisha wakaendelea kuketi katika kibao na kufanya kazi zao,” akasema mvumbuzi huyo ambaye pia ni mwandishi wa filamu za mtaani za ucheshi na tayari ameweza kuuza baadhi ya kazi zake katika fani hiyo.

Kulingana na George, kibao-mbuzi ndogo huuzwa kwa Sh600, wastani Sh800 na kubwa zaidi Sh1,200.

“Nimeweza kuuza mbuzi hizo zaidi ya 80. Katika miezi ya kwanza, sikuweza kuuza vibao nyingi manake nilikuwa natumia muda mwingi kuipigia debe bidhaa yenyewe na kuchukua maoni kutoka kwa watu tofauti. Hata hivyo, ninashukuru Kibao Mbuzi imeanza kukubalika kote,” akasema.

George anaelezea kuwa ameweza kufanikisha uvumbuzi wake kwa kuwa tayari alikuwa amefunzwa useremala na baba yake mzazi.

“Najua kutafuta mbao bora, nikazikata, nikazipiga msasa na kuziunganisha kutumia misumari. Zaidi, mashine au ‘meno’ ya kukunia nazi, ni chuma ninazoweza kutengeneza nikitumia msumeno,” akasema George huku akibainisha kuwa chuma kimoja hunuliwa kwa Sh50.

Zaidi, anaongeza kuwa mbao anazotumia hulingana na mahitaji ya wateja wake.

“Naweza kutengeneza kibao-mbuzi nikitumia mbao nyepesi au nzito kulingana na mahitaji ya mteja wangu. Hata hivyo, bei huwa tofauti kulingana mbao ambazo nimetumia,” akasema.

George alielezea kuwa amepata baadhi ya changamoto ikiwemo kukosa pesa za kununua rasilimali za kutosha kutengeneza mbuzi hizo.

Hata hivyo, ana matumaini kuwa kibao-mbuzi itajulikana kote ili aweze kuwa na soko kubwa.

“Nikipata wateja wengi, nitaweza kuwaajiri vijana ili wanisaidie kutengeneza mbuzi hizo,” akasema huku akitoa wosia kwa vijana wenzake wakome kulalamika kuwa hawana kazi, bali ajitume, na hata zaidi wajifunze ujuzi tofauti ili wenyewe wajianzishie biashara zao.

“Kila mtu ana uwezo wa kuvumbua. Tusiwe wavivu wa akili kila mara tukilia kuwa hakuna kazi, mara tunasubiri kuajiriwa ofisini na sababu zingine ambazo kama vijana tumezoea,” akasema.