RIZIKI: Alipenda baiskeli utotoni, sasa ni fundi hodari wa baiskeli ukubwani
Na SAMMY WAWERU
LEONARD Musula ni fundi hodari katika kukarabati na kurekebisha baiskeli zilizoharibika na pia kuzirembesha.
Karakana yake ipo eneo la Toezz, katika mtaa wa Githurai, kiungani mwa jiji la Nairobi.
Jinsi alivyojipata katika gange hiyo, Musula anasema ni kupitia kwa yeye kupenda baiskeli tangu akiwa mdogo kiumri.
Akivuta mawazo yake nyuma, kana kwamba ilikuwa jana tu, barobaro huyu anasema alipenda kucheza na baiskeli, asiijue siku za usoni itaishia kuwa kitega uchumi chake.
Kulingana na Musula, akiwa mdogo matamanio yake yalikuwa kuwa mhandisi, na isemwavyo lenga mwezi, ukikosa kulenga shabaha utaangukia nyota, hatimaye aliishia kuwa mhandisi wa baiskeli.
Urekebishaji wa ‘vijigari vya magurudumu mawili’, ni gange inayomuingizia mapato ya kuridhisha na kumudu kukithi familia yake riziki na mahitaji mengine muhimu ya kimsingi.
“Utengenezaji na urekebishaji wa baiskeli hususan zile za kisasa na za hadhi ndio afisi yangu ya kila siku. Ninaamini mimi ni mhandisi, mhandisi wa baiskeli.
“Ndoto zangu za tangu nikiwa mdogo zilitimia na nina kila sababu ya kutabasamu na kumshukuru Mwenyezi Mungu,” Musula anasema.
Karakana yake huwa yenye shughuli chungu nzima, kufuatia jitihada zake kujituma kuhudumia wapenzi wa baiskeli.
Anasema safari ya kufika aliko sasa, ilianza 1998.
“Nilijinyima mengi na kuweka akiba ya Sh4,000 nilizotumia kama mtaji,” anafichua, akiongeza kwamba alifanya vibarua vya hapa na pale kukusanya pesa hizo.
Anasema alitumia Sh3,000 kununua vipuri vya baiskeli na zana za kazi kama vile komeo, nyundo kati ya vifaa vinginevyo.
Wakati huo, kodi ya nyumba haikuwa ghali, na anadokeza kwamba fedha zilizosalia alitumia kukodi chumba.
Anasimulia kwamba utangulizi safari hiyo haikuwa rahisi, akitaja ukosefu wa vipuri na vilivyopatikana kuwa bei ghali kama miongoni mwa changamoto zilizomzingira.
Mchumia juani hulia kivulini, kauli hii ilimpa motisha, akaendelea kujikaza ‘ipo siku mambo yatakuwa mteremko’.
Kuanzia mwaka wa 2006, Musula anasema kazi ilianza kuimarika.
Kwa sasa huduma zake zimeboreka kiasi cha kupata idadi kubwa ya wateja.
Anasema ada ya kukarabati baiskeli inalingana na hitilafu, leba ya chini ikiwa Sh100.
Musula pia hurembesha baiskeli, kwa mujibu wa matakwa ya mmiliki.
Hali kadhalika, karakana yake hununua na kuuza baiskeli, akidokeza kwamba bei yake ya mauzo huwa kati ya Sh4, 000 – 20, 000.
“Kuna basikeli zingine, hasa zile mpya na kulingana na muundo hugharimu zaidi ya Sh20,000,” akasema wakati wa mahojiano.
Hununua na kuuza basikeli za aina tofauti kama vile za mashindano, watoto na pia zenye uwezo kusafiri masafa marefu.
Alipoulizwa ikiwa anaweza kuacha gange hiyo ili kuajiriwa kwingine, alijibu: “Mshahara ninaopata kupitia kazi ya kutengeneza, kukarabati baiskeli na kuziuza, sidhani kuna mwajiri katika sekta ya baiskeli anayeweza kunilipa kiasi cha pesa ninazounda.”
Musula, 40, anaridhia talanta yake katika uhandisi wa basikeli, akihimiza vijana kupalilia na kuthamini vipaji walivyojaaliwa na Mola.
“Kuna waliobarikiwa kuchora, kuigiza, uandishi, soka, riadha, kati ya vipaji vinginevyo, wavipalilie na wavitumie ipasavyo vitawaimarisha,” anashauri, akisisizia haja ya uvumilivu licha ya pandashuka zinazoibuka.