• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 5:23 PM
ONYANGO: Serikali ilinde wazee dhidi ya corona msimu wa sikukuu

ONYANGO: Serikali ilinde wazee dhidi ya corona msimu wa sikukuu

Na LEONARD ONYANGO

VIFO vinavyotokana na ugonjwa wa corona huenda vikaongezeka humu nchini wakati wa msimu wa sherehe za Krismasi na Mwaka Mpya iwapo serikali haitachukua hatua mawafaka kuwalinda wazee.

Kwa kawaida, mwezi wa Desemba hutoa fursa kwa watu wengi wanaoishi katika maeneo ya mijini kama vile Nairobi na Mombasa kurejea nyumbani kujumuika na familia zao kwa ajili ya sherehe ya Krismasi na kukaribisha mwaka mpya.

Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha kuwa japo idadi kubwa ya watu walioambukizwa virusi vya corona ni vijana wa kati ya umri wa miaka 25 na 39, idadi kubwa ya wanaofariki ni wazee wa miaka 65 na zaidi.

Kwa mujibu wa WHO, asilimia 75 ya vifo milioni 1.5 vya corona ambavyo vimethibitishwa kote duniani kufikia sasa, ni wazee wa umri wa miaka 65 na zaidi.

Takwimu za wizara ya Afya pia zinaonyesha kuwa asilimia kubwa ya waliofariki kutokana na virusi vya corona ni watu wa kuanzia umri wa miaka 60.

Tafiti zinaonyesha kuwa wazee hulemewa zaidi na virusi vya corona kwa kuwa kingamwili zao ni dhaifu. Aidha, wengi walio na maradhi kama vile kisukari, shinikizo la damu, ugonjwa wa moyo na mapafu nakadhalika huwa ni watu wa kuanzia umri wa miaka 65 na zaidi.

Hivyo, serikali ina jukumu la kuwalinda wazee na watu wanaougua maradhi hayo hatari wakati huu wa msimu wa sherehe za Krismasi.

Serikali inafaa kuanzisha kampeni ya kuhamasiaha vijana kuhusu jinsi ya kutangamana na wazee bila kuwaambukiza virusi vya corona wakati huu wa msimu wa sherehe za Krismasi na Mwaka Mpya.

Huku visa vya maambukizi ya corona vinavyothibitishwa kwa siku vikiongezeka kila uchao humu nchini, serikali pia haina budi kuweka mikakati ya kuwalinda watu walio na maradhi hatari kama vile kisukari.

Serikali iwalinde wazee kwa kuwapa barakoa na dawa ya kuua viini vya corona bila malipo kote nchini.

Huu ndio wakati kwa wanasiasa kusambaza barakoa na sanitaiza za bure kama ilivyoshuhudiwa mara tu baada ya kisa cha kwanza cha mwathiriwa wa virusi vya corona kuthibitishwa humu nchini mnamo Machi.

Kampeni za kupigia debe mswada wa Mpango wa Maridhiano (BBI) zisitishwe mwezi huu na badala yake serikali na wanasiasa waelekeze juhudi zao katika kampeni za kuwalinda wazee na wagonjwa wa maradhi hatari kama vile kisukari, shinikizo la damu na mengineyo dhidi ya kuambukizwa virusi vya corona.

You can share this post!

RIZIKI: Alipenda baiskeli utotoni, sasa ni fundi hodari wa...

KAMAU: Wanawake waungane kukabili tamaduni duni