Siasa

Weta aanza kukabili waasi katika Ford-K

December 2nd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na RUTH MBULA

KIONGOZI wa chama cha Ford-Kenya, Bw Moses Wetang’ula, ameanza harakati kuwakabili maafisa wa chama hicho ambao wamekuwa wakipinga uongozi wake.

Hili ni kwenye juhudi za kudhihirisha udhibiti wake kwenye chama ambacho kimekuwa kikikumbwa na mizozo.

Mnamo Jumapili, Bw Wetang’ula, ambaye pia ni Seneta wa Bungoma, alianza kufanya ziara kote nchini, hatua inayoonekana kama juhudi za kulainisha usimamizi wa chama kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Hii ni licha ya baadhi ya wapinzani wake chamani kupuuzilia mbali juhudi zake.

Hatua ya kwanza ilikuwa kubadilisha uongozi wa chama katika eneo la Kisii, kwa kuwaondoa wanachama wanaomuunga mkono mbunge Wafula Wamunyinyi (Kanduyi) kama kiongozi.

Kufuatia mabadiliko hayo, Dkt Timothy Arege atakuwa Kaimu Mwenyekiti. Alichukua mahali pa Bw Job Nyakenyanya. Bw Nyakenyanya amekuwa akiunga mkono mrengo wa Bw Wamunyinyi, ambao umekuwa ukifanya juhudi kumwondoa Bw Wetang’ula kama mwenyekiti wa chama.

Kwenye kikao hicho kilichowashirikisha wabunge wake kutoka kaunti za Kisii na Nyamira, Seneta alisema chama kitaendelea kujipigia debe kote nchini kabla ya uchaguzi huo.

“Tutaendelea kuimarisha juhudi zetu hata tunapoendelea kuunga mkono Mpango wa Maridhiano (BBI),” akasema Bw Wetang’ula.

Mapema mwaka 2020 Bw Wamunyinyi aliongoza kundi ambalo lilitangaza kumwondoa Bw Wetang’ula kama kiongozi wa chama.

Hata hivyo, Bw Wetang’ula alipata afueni baada ya mahakama kubatilisha hatua hiyo.

Licha ya mabadiliko hayo katika eneo la Kisii, makabiliano kati ya kambi husika bado yanaendelea, huku kila mrengo ukipigania kupata utambuzi maalum.

Mapema mwezi huu, Bw Wamunyinyi alikutana na baadhi ya wajumbe wa chama ili kuimarisha uungwaji mkono wake ielekeapo 2022.

Kabla ya ziara yake, Katibu Mkuu wa chama hicho, Dkt Eseli Simiyu alifanya ziara katika kaunti za Kisii na Nyamira ambapo alikutana na baadhi ya viongozi wake.

Mnamo Agosti, Kiongozi wa Kitaifa wa Vijana chamani, Bw Fred Asila, alisema walikuwa wakiendesha kampeni kote nchini kukivumisha chini ya uongozi wa Bw Wamunyinyi na Dkt Simiyu.

Bw Asila alisema kuwa uongozi mpya unalenga kuimarisha mipango ya baadaye ya chama.

Alisema waliunga mkono kuondolewa kwa Bw Wetang’ula kama kiongozi wao.

Kama Bw Wetang’ula, Dkt Simiyu alisema viongozi wa chama wameanza kukivumisha katika maeneo ya mashinani kwenye kaunti mbalimbali.

Kuhusu BBI, Bw Wetang’ula alisema lengo lake kuu la mchakato huo ni kuleta umoja nchini kuliko ilivyokuwa awali.

Miongoni mwa waliokuwepo kwenye hafla hiyo ni wabunge Richard Onyonka (Kitutu Chache) na Vincent Kemosi (Mugirango Magharibi).