Makala

KINA CHA FIKIRA: Ukitenda wema utalipwa wema hapa duniani

December 2nd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na WALLAH BIN WALLAH

MATENDO mema ya mwanadamu ndiyo yanayojenga utu wa mwanadamu.

Na matendo maovu ya mtu ndiyo yanayobomoa utu wa mtu! Wakati mwingine binadamu huwa mwema kwa kuchagua tu kuwa mwema ama huwa mwovu kwa kuchagua tu kuwa mwovu! Lakini tujue kwamba kila kitendo kina chanzo chake, matokeo yake na malipo yake. Chanzo cha maovu ni watu waovu!

Chanzo cha mema ni watu wema! Matendo ni tabia za mtu! Ila tuzingatie kwamba matendo mema hulipwa kwa mema na matendo maovu hulipwa kwa maovu! Jitahidi uchague kutenda mema uwe mwema ulipwe wema!

Kasonge alikuwa mwanafunzi katika shule ya upili Kijiweni kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne. Amesomea Kijiweni kwa shida kubwa! Wazazi wake waliishi katika ufukara wakila na kuvaa kwa kufanya kazi za mikono kuwalimia watu, kuwafulia nguo na kuwachungia mifugo. Kasonge alipoenda nyumbani likizoni au kwa kufukuziwa karo alijiunga na wazazi wake kufanya kazi za mikono ndipo wapate chakula na pesa kidogo za kurudi shuleni! Lakini Kasonge alikuwa na bidii sana masomoni. Pia alikuwa mwema mtiifu mwenye nidhamu zaidi! Alipenda shule kwa nia ya kusoma afaulu maishani. Labda umaskini na hali duni nyumbani kwao ndiyo iliyomchochea kufanya bidii ili aje alete maisha mema kwa familia yake siku zijazo! Lakini watoto wangapi wanaojua hivyo??

Shule ilipofunguliwa muhula wa tatu wanafunzi wa kidato cha nne pekee ndio waliorudi wafanye mtihani wa mwisho wa taifa! Kasonge alirejea na wenzake akiwa mikono mitupu bila chochote! Na alipokuwa nyumbani mara nyingi walilala njaa na kushinda njaa! Hali ilikuwa mbaya bila kibarua chochote! Halafu alidaiwa limbikizo la karo shilingi elfu arubaini ambazo bila ya kuzilipa asingefanya mtihani!

Saa kumi na moja jioni Mwalimu wa zamu Bwana Mtajua alipogonga kengele ili wanafunzi wakusanyike gwarideni, Kasonge alibaki ndani ya bweni akipangapanga vitabu katika mkoba wake aondoke arudi nyumbani badala ya kungojea kufurushwa! Baada ya wanafunzi kuitwa majina, Mwalimu Mtajua aliuliza, “Kasonge yuko wapi?” Wenzake walijibu, “Amebaki bwenini!” Mwalimu alienda mwenyewe kumtafuta! Alimkuta Kasonge amesongwa na mawazo moyoni! Akamwambia, “Kasonge, utasoma mpaka umalize masomo yako!” Kasonge alidhani alikuwa ndotoni! Hakika alisoma akafaulu vizuri akaingia chuo kikuu!

Miaka kumi na mitano baadaye Mwalimu Mtajua akiwa mgonjwa mahututi maradhi ya moyo na mapafu yametoboka alilala akingojea kukata roho kwa kukosa shilingi milioni ishirini za kumsafirisha ng’ambo kutibiwa, alishangaa kumwona mwanafunzi wake Daktari Kasonge ndiye aliyekuja kumtibu mpaka akapona!

Ndugu wapenzi, ukitenda wema utalipwa wema hapa hapa duniani!

[email protected]