NMK yakemea wakazi Lamu kwa kuvamia ardhi za turathi
Na KALUME KAZUNGU
HALMASHAURI ya Makavazi na Turathi nchini (NMK) imeonya wakazi wa Lamu dhidi ya kuvamia ardhi za makavazi na kuzigeuza makazi yao.
Naibu Mkurugenzi wa NMK Ukanda wa Pwani, Athman Hussein, anasema baadhi ya wakazi wamekuwa wakinyakua ardhi za makavazi na kuzikalia, hatua ambayo huenda ikachangia kupotea kwa maeneo hayo muhimu.
Katika mahojiano na Taifa Leo, Bw Hussein alitaja makavazi ya Pate, Siyu, Manda na Takwa kuwa sehemu ambazo ziko kwenye hatari ya kunyakuliwa.
Alisema NMK iko kwenye mazungumzo na serikali ya kaunti na ile ya kitaifa ili kuwepo na uwezekano wa kutolewa kwa hatimiliki kwa sehemu za makavazi ambazo hazijakuwa na veti hivyo.
Bw Hussein alisema ni kupitia kuwepo kwa hatimiliki ambapo ardhi za makavazi zitalindwa dhidi ya wanyakuzi.
Aidha aliwaonya wakazi dhidi ya kukalia ardhi hizo, akisisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wavamizi wa ardhi za makavazi.
“NMK haina fedha za kutumika kufurushia watu wanaovamia ardhi za makavazi. Hivyo ni muhimu kwa wananchi kuepuka kukaa kwa ardhi hizo,” akasema Bw Hussein.
Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Lamu, Mohamed Mbwana aidha aliilumu NMK kwa kutowajumuisha wazee katika kuzitambua na kuziorodhesha ardhi za makavazi eneo hilo.
Bw Mbwana alisema wazee eneo hilo wako na ufahamu mkubwa kuhusiana na ardhi zote ambazo ni za zamani na ambazo baadhi yazo tayari zienyakuliwa na umma.
“Sisi tunao ufahamu wa ardhi zipi za makavazi ambazo tayari zimenyakuliwa na ni zipi ziko salama. Cha ajabu ni kwamba NMK yenyewe haijatuhusisha katika suala hilo,” akasema Bw Mbwana.
Mwaka 2019, NMK ilitangaza kwamba ilihitaji angalau Sh200 milioni ili kushughulikia masuala ya turathi na makavazi Kaunti ya Lamu.