• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 2:08 PM
Rugby Africa kugawia mataifa 11 Kenya ikiwemo Sh36 milioni kuanza raga 2021

Rugby Africa kugawia mataifa 11 Kenya ikiwemo Sh36 milioni kuanza raga 2021

Na GEOFFREY ANENE

KENYA itanufaika na msaada wa Sh36.9 milioni utakaotolewa na Shirikisho la Raga barani Afrika (Rugby Africa) kwa mataifa 11.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari Jumatano, Rugby Africa imeorodhesha Kenya pamoja na Namibia, Uganda, Tunisia, Zimbabwe, Algeria, Zambia, Madagascar, Ivory Coast, Senegal na Ghana kupokea fedha kati ya Sh5.8 milioni na Sh671,247 kwa sababu ya hatua kubwa za kimaendeleo nchi hizo zimepiga kwenye raga.

Isitoshe, Rugby Africa ilisema kuwa mataifa yatakayopokea hela hizo yamekuwa yakishiriki mashindano yake na pia kuandikisha matokeo mazuri katika mashindano hayo ambayo ni Kombe la Afrika la wachezaji 15 kila upande na Kombe la Afrika la wachezaji saba kila upande pamoja na Kombe la Afrika la wachezaji walio chini ya umri wa miaka 20 almaarufu kama Barthes Trophy.

Maendeleo ya mwanachama na uthabiti wa raga yake yalichangia asilimia 40 nayo ushiriki wake kwenye mashindano ya Rugby Africa ulichangia asilimia 60.

Rugby Africa imesema kuwa fedha inazotoa kwa mataifa hayo 11 ni za kuzisaidia kufanikisha kurejea kwa raga kwa njia ya salama mwaka 2021 baada ya msimu 2020 kuvurugwa na janga la virusi vya corona.

“Tuna mataifa 39 wanachama wa Rugby Africa, lakini tulichagua 11 ili kuhakikisha fedha zinazotolewa zinaelekezwa katika mataifa ambayo yatazalisha matunda makubwa na yatakayoonekana kwa haraka. Hii inaonyesha kuwa kuna faida kubwa kwa washiriki wa mashindano ya Rugby Africa,” shirikisho hilo linaloongozwa na Khaled Babbou lilisema na kuongeza kuwa fedha hizo ni tofauti na zilizotolewa hapo awali za kusaidia wanachama wake kukabiliana na makali ya janga la corona. Kenya ilipokea Sh644,111 mwezi Septemba wakati Rugby Africa iliwapa wanachama wake wote kiasi tofauti cha fedha kukabiliana na janga la corona.

  • Tags

You can share this post!

Ruto, wandani wake wasikitika baadhi ya mapendekezo ya BBI...

Jinsi ya kutengeneza shake ya vanilla na maziwa