• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 9:50 AM
Giroud afunga mabao manne na kuongoza Chelsea kudhalilisha Sevilla katika UEFA

Giroud afunga mabao manne na kuongoza Chelsea kudhalilisha Sevilla katika UEFA

Na MASHIRIKA

OLIVIER Giroud alifunga mabao manne katika ushindi wa 4-0 uliosajiliwa na Chelsea dhidi ya Sevilla kwenye mchuano wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Disemba 2, 2020.

Ushindi huo uliosajiliwa na Chelsea ugenini uliwapa uhakika wa kukamilisha kampeni za hatua ya makundi kileleni Kundi E.

Giroud alifunga mabao mawili katika kipindi cha kwanza baada ya kushirikiana vilivyo na Kai Havertz na Matteo Kovacic.

Alifumwa nyavu za wenyeji wao kwa mara ya tatu kupitia mpira wa kichwa katika dakika ya 74 kabla ya kufunga penalti ya dakika ya 88 alipochezewa visivyo ndani ya eneo la hatari.

Chelsea walioshuka dimbani kwa minajili ya mchuano huo wakiwa tayari wamefuzu kwa hatua ya 16-bora, walifanyia kikosi kilichoambulia sare tasa dhidi ya Tottenham Hotspur katika gozi la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Novemba 29, 2020 mabadiliko tisa.

Havertz na Christian Pulisic waliokuwa mkekani kwa muda mrefu kuuguza majeraha, walipangwa katika kikosi cha kwanza cha Chelsea almaarufu ‘The Blues’ kwa mara ya kwanza tangu Oktoba 2020.

Mchuano dhidi ya Sevilla ulimshuhudia pia kocha Frank Lampard akimwajibishwa chipukizi Billy Gilmour, 19, kwa mara ya kwanza msimu huu. Kiungo huyo alitokea benchi katika kipindi cha pili.

Sevilla ambao pia waliingia ugani wakiwa tayari wamejikatia tiketi ya hatua ya 16-bora, walikosa huduma za wanasoka wengi wa kikosi cha kwanza na walitegemea maarifa ya kipa Alfonso Pastor katikati ya michuma baada ya mlinda-lango chaguo la kwanza, Tomas Vaclik kupata jeraha mazoezini.

Ilikuwa mara ya kwanza kwa Pastor, 20, kuchezeshwa na Sevilla walionyanyua ubingwa wa Europa League katika msimu wa 2019-20.

Hadi alipoowadhalilisha Sevilla, Giroud alikuwa amepangwa katika kikosi cha kwanza cha Chelsea mara moja pekee msimu huu kwenye mchuano wa EFL ulioshuhudia Tottenham Hotspur wakiwaangusha uwanjani Stamford Bridge.

Giroud aliingia uwanjani kuongoza safu ya mbele ya Chelsea dhidi ya Sevilla akijivunia kufunga bao la ushindi katika dakika za mwisho kwenye mechi ya awali ya UEFA iliyowakutanisha na Rennes ya Ufaransa mnamo Novemba 24, 2020.

Uhakika wa Giroud kuunga kikosi cha kwanza cha Chelsea msimu huu ulishuka baada ya waajiri wake kumsajili fowadi Timo Werner ambaye amekuwa akishirikiana vizuri zaidi na Tammy Abraham kwenye safu ya mbele ya kikosi cha Lampard.

“Giroud ni mwanasoka wa haiba kubwa na mvamizi tegemeo katika mechi muhimu. Angalia rekodi yake ya ufungaji katika timu ya taifa na kwenye kivumbi cha UEFA,” akatanguliza Lampard.

“Fomu yake inazidi kuimarika kila uchao. Anajitahidi mazoezini na ni mfano bora kwa chipukizi wetu hasa ikizingatiwa ukubwa wa kiwango cha kuhisika kwa ushawishi wake kila anaposhuka dimbani,” akasema Lampard kumhusu fowadi huyo wa zamani wa Arsenal.

Mwishoni mwa mchuano huo, Lampard alikiri kwamba hakutarajia kibarua chao dhidi ya Sevilla kiwe chepesi kiasi hicho hasa ikizingatiwa kwamba miamba hao wa Uhispania waliwalazimishia sare tasa katika mechi ya mkondo wa kwanza mnamo Oktoba 2020 uwanjani Stamford Bridge. Chelsea walitawazwa mabingwa wa taji la UEFA kwa mara ya mwisho mnamo 2012.

Mbali na Havertz na Pulisic, wanasoka wengine walioridhisha pakubwa kambini mwa Chelsea dhidi ya Sevilla ni Callum Hudson-Odoi na Antonio Rudiger.

Chelsea kwa sasa wanajiandaa kuwa wenyeji wa limbukeni wa EPL, Leeds United mnamo Disemba 5, 2020 kabla ya kukamilisha kampeni zao za makundi kwenye UEFA mnamo Disemba 8, 2020 dhidi ya Krasnodar ya Urusi uwanjani Stamford Bridge.

Kwa upande wao, Sevilla wameratibiwa kucheza na Real Madrid kwenye mechi ya La Liga mnamo Disemba 5 kabla ya kuvaana na Rennes katika mchuano wa mwisho wa Kundi E katika UEFA.

You can share this post!

Nahodha wa Harambee Starlets atua kambini mwa Thika Queens...

Manchester United katika hatari ya kuaga kipute cha UEFA...