Neymar atamani tena kucheza pamoja na Messi
Na MASHIRIKA
HUENDA Lionel Messi akashawishika sasa kutua kambini mwa Paris Saint-Germain (PSG) na kutupilia mbali ofa ya kujiunga na Manchester City baada ya kuagana na Barcelona mwishoni mwa msimu huu.
Hii ni baada ya nyota Neymar Jr kufichua kwamba kubwa zaidi katika maazimio yake kwa sasa kitaaluma ni kucheza tena na Messi katika kikosi kimoja.
“Ninachotamani zaidi ni kucheza na Messi pamoja, niweze kushirikiana naye pamoja uwanjani kwa mara nyingine,” akasema fowadi huyo wa zamani wa Barcelona mwishoni mwa mechi ya Klabu Bingwa Ulaya iliyowashuhudia PSG wakipiga Manchester United 3-1 mnamo Disemba 2, 2020 uwanjani Old Trafford.
“Anaweza kucheza katika nafasi yangu kwa sasa kambini mwa PSG ambayo ni ya mvamizi mkuu, nami nicheze pembezoni mwa uwanja au nyuma yake. Sina tatizo lolote na hilo. Ningependa hilo lifanyike kuanzia msimu ujao na naona ni kitu cha lazima kufanyika,” akasema Neymar ambaye ni raia wa Brazil.
Neymar anaitoa kauli hiyo siku chache baada ya rais mshikilizi wa Barcelona, Carlos Tusquets kusema kwamba ingalikuwa nafuu zaidi kwa kikosi hicho kumkubalia Messi kuondoka ugani Camp Nou mwishoni mwa msimu huu wa 2019-20 jinsi alivyotaka.
Messi, 33, aliwasilishia Barcelona barua ya kutaka wamwachilie aondoke Camp Nou mwishoni mwa msimu uliopita. Hata hivyo, fowadi huyo raia wa Argentina alizuiwa na La Liga kuondoka baada ya shirikisho hilo la soka ya Uhispania kusisitiza kwamba wanunuzi wa Messi wangelazimika kuweka mezani Sh89 bilioni ili kumtwaa rasmi.
Hata hivyo, mkataba wa sasa kati ya Messi na Barcelona unatarajiwa kutamatika rasmi mwishoni mwa msimu huu ambapo atakuwa huru kuteua pa kuelekea. Awali, alihusishwa pakubwa na Man-City waliokuwa radhi kumsajili ili aungane na kocha wake wa zamani Pep Guardiola.
Josep Maria Bartomeu alijiuzulu kama rais wa Barcelona mnamo Oktoba na nafasi yake ikatwaliwa na Tusquets ambaye kwa sasa ni kaimu rais hadi uchaguzi mkuu utakapoandaliwa mnamo Januari 2021.
“Nikizungumza kwa mtazamo wa kiuchumi, Barcelona wangalichuma nafuu kubwa kifedha iwapo wangalimtia Messi mnadani mwishoni mwa 2019-20. Hatua hiyo ingaliwaweka Barcelona katika nafasi ya kupunguza gharama ya matumizi ya fedha,” akasema katika mahojiano yake na kituo cha redio cha RAC1 nchini Uhispania.
Ili kujinasia huduma za Messi katika juhudi za kutimiza masharti mapya ya Neymar, itawajuzu PSG kuwauza wanasoka Angel Di Maria, 32, na Kylian Mbappe, 21.
Hata hivyo, gazeti la Mundo Deportivo nchini Uhispania limeshikilia kwamba ni kinaya kikubwa kwa Neymar kutamani tena kuungana na Messi ikizingatiwa kwamba kuondoka kwake Barcelona kulichochewa na haja ya kutaka kuwa huru baada ya kusisitiza kwamba alichoka kuwa kivuli cha Messi ugani Camp Nou.
Neymar aliagana rasmi na Barcelona mnamo 2017 na kutua PSG kwa Sh26 bilioni licha ya vinara wa Barcelona kutokuwa radhi kumuuza. Kubwa zaidi alichosema wakati huo ni kwamba alikuwa na maazimio ya kujiunga na kikosi kitakachomfanya mwanasoka tegemeo ili ajinyanyulie mataji ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) na Ballon d’Or ambalo hutolewa kwa mwanasoka bora zaidi duniani kila mwaka.
Hata hivyo, Neymar hajafanikiwa katika maazimio yake hayo kufikia sasa na aliwahi kufunguka mwishoni mwa msimu wa 2018-19 na kukiri kwamba angetamani kurejea Barcelona.
“Kwa msingi wa kiuchumi, haiwezekani kwa PSG kumudu gharama ya kuwadumisha Di Maria, Messi, Neymar na Mbappe katika kikosi kimoja. Kwa kuwa Di Maria yuko katika mwaka wa mwisho wa kandarasi yake na PSG, huenda kikosi hicho kikalazimika kumuuza na kumtia Mbappe mnadani ili kumudu usajili wa Messi,” ikasema sehemu ya taarifa ya Mundo Deportivo.
Mbappe kwa sasa anawaniwa pakubwa na miamba wa soka ya Uhispania na bara Ulaya, Real Madrid.
Ingawa hivyo, Joan Laporta na Victor Font ambao ni washindani wawili wakuu katika vita vya kuwania urais wa Barcelona, wamesisitiza kuwa maazimio yao ni kumdumisha Messi uwanjani Camp Nou.
Neymar angali na mwaka mmoja na nusu kwenye mkataba wake wa sasa na PSG na kumshawishi kubanduka katika kikosi cha miamba hao wa Ufaransa na kuungana na Messi ama Barcelona, Man-City, Juventus, Inter Milan au Chelsea ni kibarua kigumu zaidi.