Habari

'Tuheshimiane', Uhuru aonya Wafadhili

December 5th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na WANDERI KAMAU

RAIS Uhuru Kenyatta jana Ijumaa aliyaonya mataifa ya Magharibi dhidi ya ‘kuingilia’ uhuru wa Kenya, akisema Kenya ni nchi huru na yenye uwezo wa kutatua matatizo yake.

Akionekana kukasirishwa na hatua ambazo mataifa hayo yamekuwa yakichukua, kama utoaji tahadhari za usafiri katika baadhi ya nchi duniani, Rais Kenyatta alisema kuwa Kenya ni nchi inayofahamu inakoelelea.

Akihutubu jana kwenye uzinduzi wa ujenzi wa jengo la G47 Ugatuzi Tower jijini Nairobi, litakaloendesha shughuli mbalimbali za serikali za kaunti, Rais Kenyatta alisema kuwa nchi hizo zinafaa kushughulikia matatizo yazo, badala ya kuingilia masuala ya ndani ya mataifa mengine.

Kenya imekuwa ikijipata kama mhasiriwa wa tahadhari za usafiri ambazo zimekuwa zikitolewa na nchi za Magharibi, hasa Amerika na Uingereza. Baadhi ya masuala ambayo nchi hizo zimekuwa zikirejelea ni mchipuko wa virusi vya corona na ugaidi.

Tayari Amerika imewashauri raia wake kutosafiri Tanzania, baada ya taifa hilo kutoweka wazi hali ya maambukizi ya virusi ilivyo.

“Hatutaruhusu yeyote kuingilia masuala ya nchi yetu. Kenya ni nchi ya Wakenya milioni 50 na inafahamu inakotaka kuelekea. Hata nyinyi (nchi hizo) mna matatizo yenu mnayofaa kuyashughulikia. Hatutaruhusu hilo hata kidogo, ila nasema kwa nia njema,” akasema Rais.

Kauli yake inajiri huku Kenya ikielekea kwa Shirika la Kifedha Duniani (IMF) na Benki ya Dunia kuomba mikopo zaidi ili kufadhili bajeti yake.

Mapema mwezi uliopita, Kenya ilituma ombi la kupata mkopo wa pili kutoka kwa shirika hilo, baada ya kupokea mkopo wa Sh79.3 bilioni mnamo Mei kuisaidia kukabili athari za janga la virusi vya corona.

Ripoti zilieleza kuwa Kenya ilichukua hatua hiyo baada ya kiwango cha ushuru kilichokusanywa kushuka kwa Sh40 bilioni, kinyume na ilivyotarajiwa.

Kwa mujibu wa wadadisi wa masuala ya kiuchumi, hatua ya Kenya kurejea kwa mashirika hayo mawili inaashiria hali ya hatari nchini, kwani huwa yanatoa masharti makali kwa nchi husika kabla ya kuzipa mikopo yake.

Masharti hayo, maarufu kama Structural Adjustment Programs (SAPs) ndiyo yanatajwa kuathiri Kenya sana kiuchumi katika miaka ya tisini, kwani ililazimika kutekeleza maagizo yote ya taasisi hizo kabla ya kupokea mkopo yake.

Ingawa serikali haijakuwa ikieleza wazi kuhusu kiwango cha deni ambacho Kenya inadaiwa na mataifa ya nje, takwimu kutoka Wizara ya Fedha mnamo Agosti zilionyesha limefikia Sh7.1 trilioni.

Uhalisia mchungu kuhusu mwelekeo wa Kenya kiuchumi ulidhihirika Jumatano, baada ya Waziri wa Fedha, Bw Ukur Yatani kusema Wakenya wanapaswa kujitayarisha kwa “hali ngumu katika siku zijazo”

Kwenye kikao na Bunge la Kitaifa, Bw Yatani alisema kuwa jukumu kuu la Serikali kwa sasa ni kuzuia uchumi wa Kenya kusambaratika.

“Jukumu kuu tulilo nalo kwa sasa ni kuhakikisha tumetekeleza bajeti na kuhakikisha uchumi wa nchi hausambaratiki. Huwa tunachukua mikopo kwa sababu kiwango cha ushuru tunachokusanya hakitoshi ama hakipo kabisa. Nitakuwa nikidanganya ikiwa nitasema tuko sawa kifedha nchini. Tuko katika hali ambayo haijawahi kushuhudiwa awali. Hali ya uchumi na kupungua kwa kiwango cha ushuru ni ya kuzua hofu,” akasema.