MUTUA: Tusidanganyane, Kenya ya sasa ni bora kuliko ya BBI
Na DOUGLAS MUTUA
KATIKA mojawapo ya hotuba zake za kupinga mabadiliko ya Katiba yanayopigiwa upatu kupitia ripoti ya Muafaka wa Maridhiano (BBI), mwanaharakati Boniface Mwangi amefoka vikali akanichekesha.
Akizungumza chini ya mwavuli wa vuguvugu la Linda Katiba, mwanaharakati huyo ambaye pia ni mwanahabari amewahimiza Wakenya wasikubali nchi yao iwe kama za majirani.
Aliwashauri wanahabari wasiufanye mjadala kuhusu BBI kuonekana kama ushindani kati ya Naibu Rais William Ruto na Waziri Mkuu wa zamani, Raila Odinga.
Kisa na maana? Eti kufanya hivyo ni kuushusha hadhi mjadala wenyewe na hivyo kukubali Kenya iwe ‘kama mataifa ya Tanzania, Uganda, Zimbabwe na mengine yaliyofeli’.
Nilicheka kidogo kwa maana Bw Mwangi alionekana kufuata nyayo za mpinzani wake wa kisiasa na Mbunge wa Starehe, Bw Charles Njagua, kuyadharau mataifa jirani.
Nadhani hujasahau kwamba miaka kadhaa iliyopita Bw Njagua almaarufu Jaguar alizua mtafaruku alipoorodhesha Waganda na Watanzania miongoni mwa watu wasiopaswa kufanya biashara ndogondogo nchini.
Tofauti kati ya mitizamo ya Bw Njagua na Bw Mwangi ni kwamba Njagua alipigania visivyo maslahi ya watu waliomchagua ilhali Bw Mwangi analenga kuupandisha hadhi mjadala wa kitaifa.
Nilisema, na ningali ninasema, kwamba Kenya ni nchi inayozingatia sera za uchumi huru na hivyo basi hatupaswi hata kufikiria kuwafukuza majirani zetu wanaotafuta riziki ya halali.
Mtazamo wa Bw Mwangi, ingawa nina hakika utawauma sana wananchi wa mataifa aliyotaja, ni wa kupongezwa na kuonewa fahari.
Kenya ndilo taifa lenye nguvu zaidi na la kidemokrasia kuyazidi yote Afrika Mashariki na Kati. Bila shaka majirani zetu wana maoni tofauti. Si hoja. Huo ni mjdala wa siku nyingine.
Kati ya mambo ambayo nimeonea fahari nikizungumza na watu wa mataifa mengine tangu nihamie Marekani ni ujasiri wa Wakenya kutetea haki zao bila kuomba msamaha.
Nimemsifia Bw Mwangi na wanaharakati wenzake waliowaingiza nguruwe maeneo ya Bunge, wakamwaga damu huko na kuwaachia wanyama hao kuiramba ili kupinga nia ya wabunge kujiongezea mishahara.
Nimemsifia mwanaharakati Okiyah Omtatah Okoiti na wenzake, pamoja na Chama cha Wanasheria cha Kenya (LSK) ambao hawasiti kuishtaki serikali ikibidi.
Kwa jumla, nimeusifia ukaidi wa Wakenya, nikaringa kwamba nchi yangu ni miongoni mwa chache sana Afrika ambazo hazijawahi kutawaliwa na majeshi kwa kuwa itabidi watuue sote tukimwagika barabarani!
Hayo majisifu yote ni ya hadi juzi tu, kwa bahati mbaya. Sina hakika leo ninaweza kuwatizama watu nyusoni na kuwasifia upekee wa nchi yangu tena.
Kenya imebadilika pakubwa. Waliokuwa wakombozi wamegeuka washirika wa serikali, sikwambii wamekaa kimya nchi ikitafunwa mithili ya ubao mkavu unavyoutafunwa na mchwa.
Mambo yakiendelea hivi, hatutawacheka Wasomali, Watanzania, Waganda, Wazimbabwe na wengine ambao huisoma demokrasia kwenye vitabu na magazeti tu.
Rais Uhuru Kenyatta, ambaye anapaswa kuwa akifunganya virago ili kuondoka Ikulu mwaka wa 2022, anajaribu kunata mamlakani, labda kwa cheo tofauti. Hilo ndilo lengo kuu la BBI, tusidanganyane!
La kusikitisha ni kwamba anahimizwa na kushangiliwa na Bw Odinga na wafuasi wake, watu ambao wameteseka zaidi nchini kila demokrasia inapoingia doa.
Bw Odinga na watu wake wanatumaini kwamba Bw Kenyatta atamuunga mkono Bw Odinga ili awe rais hapo 2022, kitu ambacho kwao kinatamanisha ila ni chambo cha kuvulia samaki.
Ikiwa Katiba itabadilishwa inavyopendekezwa na ripoti ya BBI, amini usiamini, Bw Kenyatta na wasiri wake hawatamruhusu Bw Odinga kuwa rais!
Urais unaopendekezwa na BBI una mamlaka kuliko aliyokuwa nayo marehemu Daniel Moi, dikteta aliyetukalia mguu wa kausha kwa miaka 24.
Hayo, nakuapia Jalali, hata akishuka malaika, Bw Kenyatta hawezi kukubali Bw Odinga awe nayo.
Kumbuka Bw Kenyatta anatuhumiwa kumuibia kura Bw Odinga mara mbili. Anaogopa kuadhibiwa akiondoka mamlakani.
Angekuwa mkweli, Bw Kenyatta angeiacha Katiba ilivyo, amuunge mkono Bw Odinga ili awe rais akistaafu. Kenya ya sasa ni bora kuliko ya baada ya BBI. Usidanganyike!