Michezo

Lukaku afunga na kusaidia Inter kuangusha Bologna ligini

December 7th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MASHIRIKA

ROMELU Lukaku aliendeleza ubabe wake wa kufunga mabao msimu huu baada ya kucheka na nyavu za Bologna mara moja na kuongoza Inter Milan kusajili ushindi wa 3-1 katika Ligi Kuu ya Italia (Serie A) mnamo Disemba 5, 2020.

Ushindi huo wa Inter wanaonolewa na kocha Antonio Conte uliwasaidia kuendeleza presha dhidi ya viongozi wa jedwali, AC Milan ambao kwa sasa wanaselelea kileleni kwa alama 23 japo wana mchuano mmoja zaidi wa kusakata ili kufikia idadi ya mechi ambazo zimepigwa na wapinzani wao wakuu – Inter na Juventus.

Inter kwa sasa wanashikilia nafasi ya pili kwa alama 21, moja zaidi kuliko nambari tatu, Juventus ambao ni mabingwa watetezi.

Lukaku aliwafungulia Inter ukurasa wa mabao katika dakika ya 16 na kufikisha magoli ambayo kwa sasa anajivunia kapuni mwake hadi 17 kutokana na mechi 18 ambazo amechezea Inter na timu ya taifa ya Ubelgiji hadi kufikia sasa msimu huu.

Achraf Hakimi alichuma nafuu kutokana na masihara ya Marcelo Brozovic katika dakika ya 45 na kufungia Inter bao la pili kabla ya Emanuel Vignato kurejesha Bologna mchezoni katika dakika ya 67 alipopachika wavuni bao la pekee kwa kikosi hicho kilichokuwa kikichezea ugenini uwanjani San Siro.

Hata hivyo, Hakimi alifungia Inter bao la tatu katika dakika ya 69 na kuhakikisha kwamba wanatia kapuni alama tatu muhimu zinazowafanya kuwa miongoni mwa wagombezi halisi wa taji la Serie A msimu huu wa 2020-21.

MATOKEO YA SERIE A (Disemba 5, 2020):

Juventus 2-1 Torino

Inter Milan 3-1 Bologna

Spezia 1-2 Lazio