AC Milan wacharaza Sampdoria na kufungua pengo la alama tano kileleni mwa jedwali la Serie A
Na MASHIRIKA
AC Milan walifungua mwanya wa alama tano kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Italia (Serie A) mnamo Disemba 6, 2020 baada ya kupepeta Sampdoria 2-1 na kuendeleza rekodi ya kutoshindwa kwao ligini hadi kufikia sasa muhula huu.
Franck Kessie aliwaweka Milan kifua mbele kunako dakika ya 45 kupitia penalti baada ya Jakub Jankto wa Sampdoria kuunawa mpira ulioelekezwa langoni na Theo Hernandez kwa kichwa.
Samu Castillejo alitokea benchi na kufanya mambo kuwa 2-0 kwa upande wa Milan katika dakika ya 77. Licha ya bao hilo kuwapa Milan motisha zaidi ya kuvamia wenyeji wao, Sampdoria walifutiwa machozi na Albin Ekdal katika dakika ya 82.
Ushindi wa Milan ambao ulikuwa wao wa nane mfululizo ligini. Ni ufanisi ambao unaendeleza rekodi ya kutopigwa kwa Milan katika jumla ya mechi 10 mfululizo – rekodi ya muda mrefu zaidi mwanzoni mwa msimu wa kivumbi cha Serie A tangu 2003-04 chini ya kocha Carlo Ancelotti ambaye kwa sasa anadhibiti mikoba ya Everton katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).
Inter Milan ya kocha Antonio Conte sasa inajivunia alama 26 na iko nyuma ya AC Milan ambao chini ya mkufunzi Stefano Pioli, hawajawahi kushinda taji la Serie A tangu 2020-11. Ni pengo la pointi tano ndilo linalotamalaki kati ya vikosi hivyo vya kwanza kwenye msimamo wa jedwali la Serie A.
Napoli ambao wanafunga orodha ya tatu-bora, wanajivunia pointi 20 sawa na mabingwa watetezi Juventus ambao wanatiwa makali na mkufunzi Andrea Pirlo.
MATOKEO YA SERIE A (Disemba 6, 2020):
Sampdoria 1-2 AC Milan
Verona 1-1 Cagliari
Parma 0-0 Benevento
AS Roma 0-0 Sassuolo
Crotone 0-4 Napoli
Udinese na Atalanta (mechi iliahirishwa)