SERIE B: Balotelli apata hifadhi ya soka baada ya kusajiliwa na kikosi cha AC Monza kwa mkataba mfupi
Na MASHIRIKA
FOWADI wa zamani wa Manchester City na Liverpool, Mario Balotelli amejiunga rasmi na kikosi cha AC Monza kinachoshiriki Ligi ya Daraja la Pili (Serie B) nchini Italia kwa mkataba mfupi utakaotamatika rasmi mwishoni mwa msimu huu wa 2020-21.
Balotelli, 30, hajakuwa na klabu tangu aagane na Brescia mwishoni mwa msimu wa 2019-20. Hadi alipopata hifadhi kambini mwa Monza, Balotelli alikuwa akishiriki mazoezi kambini mwa Franciacorta inayoshiriki Ligi ya Daraja la Nne (Serie D) nchini Italia tangu Novemba 2020.
Monza wanajivunia pia huduma za kiungo wa zamani wa Tottenham Hotspur, Kevin Prince-Boateng. Kikosi hicho kwa sasa kinashikilia nafasi ya tisa kwenye msimamo wa jedwali la Serie B.
Balotelli amewahi pia kuvalia jezi za klabu za Inter na AC Milan katika Ligi Kuu ya Italia (Serie A).
Akiwa Inter alifunga mabao 28 kutokana na mechi 86 na kusaidia kikosi hicho kutwaa taji la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) na kutia kibindoni mataji matatu ya Serie A, Kombe la Coppa Italia na Italian Super Cup.
Alinyanyua pia taji la EPL na Kombe la FA akivalia jezi za Man-City aliowafungia jumla ya mabao 30 kutokana na michuano 80.