Makala

WANGARI: Umakinifu wahitajika katika sheria zijazo za mihadarati

December 9th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MARY WANGARI

TUME ya Umoja wa Mataifa kuhusu Mihadarati mapema wiki jana iliondoa bangi kwenye orodha ya mihadarati hatari zaidi katika hatua ambayo bilashaka ilivutia mijadala nchini na kimataifa.

UN iliondoa bangi kutoka Kitengo IV cha mihadarati inayodhibitiwa, ambacho kimetengewa dawa za kulevya ambazo ni hatari zaidi kama vile heroini.

Hatua hiyo ilijiri huku Mswada Unaofanyiwa Marekebisho kuhusu Mihadarati na Dawa za Kusisimua 2020, ukigonga vichwa vya habari na kuibua hisia za kila aina.

Ukweli ni kuwa, matumizi ya dawa za kulevya bado ni kero kubwa nchini Kenya ambalo limeathiri mno sekta ya kukabiliana na uhalifu, kijamii na kiuchumi.

Si ajabu kwamba Kenya imeorodheshwa miongoni mwa mataifa sugu yanayohusika na uzalishaji, usafirishaji na ulanguzi wa mihadarati na madawa ya kusisimua.

Ndiposa Mswada huu umejiri wakati mwafaka zaidi na umuhimu wake katika kudhibiti ulanguzi na matumizi ya mihadarati hauwezi ukapuuzwa.

Kwa muda sasa, kumekuwa na hisia kuwa sheria iliyopo, ambayo ilibuniwa 1994 kuhusu mihadarati si faafu katika kupiga vita matumizi ya dawa za kulevya.

Kuna hisia kuwa sheria hiyo badala ya kulenga mashirika ya mabwenyenye yanayoendesha biashara ya ulanguzi wa dawa za kulevya, inawalenga watumiaji wake hivyo kuwa na ubaguzi.

Takwimu tayari zinaashiria nyakati ngumu zijazo endapo kero la mihadarati halitashughulikiwa vilivyo kupitia mikakati kabambe ya kisheria na kisera.

Kenya iliandikisha historia kwa sababu zote mbaya baada ya tani 1.5 za heroini kunaswa humu nchini mnamo 2018 na kufanya taifa hili kuorodheshwa miongoni mwa mataifa yaliyonasa kiwango kikubwa zaidi cha heroni kulingana na Ripoti ya Ulimwengu kuhusu Mihadarati 2019.

Kando na takwimu hizo za kuhofisha, ni bayana kwamba madhara ya mihadarati katika jamii hasa miongoni mwa vijana hayawezi kupuuzwa.

Hatua ya kufanyia marekebisho sheria kuhusu dawa za kulevya itachangia pakubwa kuziba mapengo yaliyopo ambayo yamefanya kuwa vigumu kuwanasa na kuwashtaki walanguzi wa mihadarati.

Kuanzia faini wanazotozwa wahalifu kuhusiana na mihadarati, vifungo wanavyohukumiwa na zaidi adhabu zinazotolewa dhidi ya maafisa wa polisi wanaopatikana na hatia ya ulanguzi wa mihadarati, ni baadhi tu ya masuala nyeti yanayopaswa kuangaziwa katika sheria inayorekebishwa.

Ni muhimu pia kuhakikisha kwamba sheria na sera zinazobuniwa zinaendana na wakati na majira yaliyopo hasa ikizingatiwa kwamba mashirika na watu wanaojihusisha na biashara ya mihadarati vilevile wanajitahidi kubuni mbinu mpya na kutia makali walizo nazo.

Japo serikali na wadau husika wamejitahidi kupambana na kero la mihadarati nchini juhudi zaidi zinahitajika.

Kubuniwa kwa mikakati madhubuti itakayowezesha wadau husika kumakinika na kuwa hatua moja mbele zaidi kila wakati kutasaidia pakubwa kuziba mianya inayotumiwa na walanguzi wa mihadarati.

[email protected]