• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 5:50 AM
KINA CHA FIKIRA: Punguza mzigo wa maisha badala ya kujiongezea mzigo

KINA CHA FIKIRA: Punguza mzigo wa maisha badala ya kujiongezea mzigo

Na WALLAH BIN WALLAH

MAISHA ni mzigo mzito kote ulimwenguni!

Kila mtu analia kwamba maisha ni magumu! Wapo wanaolia waziwazi hadi kilio chao kinasikika! Wengine wanalia chini kwa chini kisirisiri wasemavyo Waswahili, “Wanalia chini ya maji!” Lakini kilio ni kilio tu hata ukililia chini ya maji au juu ya maji! Na kilio si dawa!

Dawa ya kukabiliana na tatizo la uzito wa maisha ni kuupunguza mzigo wenyewe kwa kuongeza nguvu kazi! Watu wafanye kazi kwa bidii kuongeza mapato na kupunguza matumizi.

Huwezi kupata nafuu maishani endapo mapato yako ni madogo au mshahara wako ni mwembamba huku mahitaji ni mengi na makubwa zaidi ya mapato yako au zaidi ya mshahara wako!

Bana matumizi kwa kuvisamehe vitu vingine unavyoweza kuishi bila ya kuwa navyo maishani ili uishi kulingana na uwezo wako na mapato yako! Bana matumizi! Punguza mzigo wa maisha badala ya kujiongezea mzigo wa maisha!

Mzee Gungunyani na Mzee Guruguza waliishi kijijini Gubigubi. Walipendana na kuelewana sana kwa mambo mengi. Leo tunapoongea, Mzee Guruguza aliaga dunia miaka mingi iliyopita na akasahaulika! Labda Mzee Gungunyani tu ndiye bado anamkumbuka kwa umbali kutokana na ukuruba waliokuwa nao pale kijijini Gubigubi!

Siku moja Mzee Gungunyani aliondoka kwa miguu akidemadema kuenda kumtembelea mjukuu wake Dungodungo katika kijiji kilichokuwa upande wa pili wa msitu! Njia ilipitia msituni! Jua lilikuwa kali! Alipofika katikati ya msitu, alimwona mzee mkongwe akikusanya kuni na kuziweka pamoja akazifunga kwa kamba! Mzee huyo akanyanyua tita la kuni kujitwika kichwani!

Alipohisi ulikuwa mzigo mwepesi kwake, aliutua chini! Akaingia kichakani kukusanya kuni zaidi akaongezea akafunga! Alipojaribu kuubeba mzigo, ukawa mzito zaidi! Yule mzee akaufungua na kuingia msituni. Akaleta kuni nyingi zaidi akaongezea! Akafunga mpaka mzigo wa kuni ukawa mkubwa na mzito zaidi kiasi kwamba mzee yule hakumudu kuunyanyua angalau sentimita moja kutoka chini autie kichwani!

Muda wote huo Mzee Gungunyani alisimama akimwangalia tu mzee yule akiendelea kuongeza kuni juu ya kuni ambazo hawezi kuzibeba badala ya kupunguza ili mzigo uwe mwepesi aubebe aende nao!

Hapo ndipo Mzee Gungunyani alipotambua na kujua kwamba aliyekuwa akifunga na kufungua kuongeza kuni alikuwa rafiki yake mpendwa hayati Mzee Guruguza! Mzee Gungunyani alishtuka akajiuliza, “Hii maana yake nini?? Badala ya kupunguza mzigo, rafiki yangu anaongeza mzigo!? Halafu ametoka wapi mtu huyu marehemu?”

Ndugu wapenzi, hivyo ndivyo watu wengi walivyo! Badala ya kupunguza mizigo mizito waliyo nayo, wanajiongezea! Watabeba vipi? Punguza mzigo wa maisha badala ya kujiongezea mzigo maishani!

[email protected]

You can share this post!

GWIJI WA WIKI: Geoffrey Mung’ou

Dkt Mogusu atawagusa?