Aguero arejea kwa matao ya juu na kuongoza Man-City kuzamisha Marseille kwenye UEFA
Na MASHIRIKA
KOCHA Pep Guardiola anaamini kwamba fowadi Sergio Aguero hatawahi kupoteza makali yake ya kufunga mabao baada ya kurejea kutoka mkekani alikokuwa akiuguza jeraha la goti na kufunga dhidi ya Olympique Marseille ya Ufaransa mnamo Disemba 9, 2020.
Bao lililofungwa na Aguero katika dakika ya 77, liliwezesha Man-City kupepeta Marseille 3-0 uwanjani Etihad na kufuzu kwa hatua ya 16-bora ya UEFA.
Hadi aliposhuka dimbani dhidi ya Marseille, Aguero alikuwa amekosa kuchezeshwa na waajiri katika mechi tatu mfululizo.
Sajili mpya Ferran Torres aliwaweka Man-City uongozini katika dakika ya 48 kabla ya Aguero kucheka na nyavu za wageni wao kunako dakika ya 77. Alvaro Gonzalez alijifunga mwishoni mwa kipindi cha pili na kuwapa Man-City bao la tatu lililowapa vijana wa Guardiola alama zote tatu kwenye mchuano huo wa Kundi C.
Aguero, 32, alikuwa akichezea Man-City kwa mara ya tano pekee kwenye mapambano yote ya msimu huu ambao umemshuhudia akitatizwa sana na jeraha la goti.
“Licha ya kuwa mwepesi wa kupata majeraha tangu afanyiwe upasuaji wa goti mwishoni mwa msimu wa 2019-20, Aguero bado ni tegemeo kubwa katika safu ya mbele ya Man-City. Alishiriki vipindi vinne pekee vya mazoezi kabla ya kuwajibishwa dhidi ya Marseille. Ni sogora aliye na uwezo mkubwa na alidhihirisha hivyo kwa kufunga bao chini ya kipindi cha dakika 25 pekee za kuwa uwanjani,” akasema Guardiola.
Ingawa hivyo, Guardiola alionya kwamba huenda akalazimika kutomchezesha Aguero dhidi ya Manchester United katika gozi kali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ambalo litawakutanisha uwanjani Old Trafford mnamo Disemba 12, 2020.
Bao la Aguero lilikuwa lake la 41 katika soka ya UEFA na kwa sasa amemfikia nyota wa Paris Saint-Germain (PSG), Neymar Jr. Lionel Messi wa Barcelona anaongoza orodha ya wafungaji bora wa UEFA kutoka Amerika ya Kusini kwa mabao 118.
Mbali na Man-City waliojizolea alama 16, kikosi kingine kilichofuzu kwa hatua ya mwondoano ya UEFA kutoka Kundi C, ni FC Porto kilichojikusanyia pointi 13. Olympiakos iliridhika na nafasi ya tatu kwa alama tatu sawa na Marseille waliovuta mkia kwa uchache wa mabao.