RIZIKI: Kutoka uchuuzi wa maji, njugu hadi mmiliki wa kinyozi
Na SAMMY WAWERU
BAADA ya kufanya mtihani wa kitaifa kidato cha nne, KCSE 2006 Justin Kimani hakuwa na budi ila kutafuta vibarua ili kusaka riziki na kukimu mahitaji mengine muhimu ya kimsingi.
Anasema asingeweza kujiunga na taasisi ya elimu ya juu, kukata kiu cha masomo, kwa sababu wazazi wake hawakuwa na uwezo vile kifedha.
Matamanio yake maishani, yalikuwa kuwa mhasibu, taaluma ambayo ingemlazimu kusomea uhasibu, ndiposa aweze kulenga shabaha ya ndoto zake.
Isitoshe, alimezea kozi hiyo kwani pia alikuwa na malengo kuwekeza katika sekta ya biashara.
Alilazimika kutia nanga maazimio hayo kwa muda, kwa ajili ya ukosefu wa fedha kujiendeleza kimasomo. “Katika shule ya upili, ilikuwa ni kwa neema ya Mungu nikasoma hadi kidato cha nne. Wazazi wangu ni wakulima wadogo, ambapo mapato yao yalikuwa ya chini,” anasema.
“Ninawashukuru kwa dhati kufuatia jitihada zao kunisomesha hadi shule ya upili, walijinyima mengi,” Kimani, 33, anaelezea.
Kutafuta njia mbadala kujiendeleza kimaisha, pia kuliwawezesha wazazi wake kusomesha ndugu zake wazawa, waliomfuata.
Kulingana na Kimani, ambaye ni mzaliwa wa Murang’a, alifanya vibarua vya hapa na pale, vikiwemo vya kulimia watu mashamba na ujenzi wa majengo.
Mwaka wa 2010, alikita kambi Nairobi, kupitia mwaliko wa mmoja wa wanafamilia.
“Mwaliko huo ulinuwia kuona ikiwa nitaweza kupata ajira, ninauridhia kufikia leo,” anasema.
Baada ya kusaka kazi kwa muda bila mafanikio, Kimani anasema alipata wazo, wazo la kufanya uchuuzi.
Anafichua kwamba alichuuza maji ya chupa za plastiki na njugu karanga jijini Nairobi na viunga vyake.
Ni gange ambayo haikuwa rahisi, ikizingatiwa kuwa alikuwa mgeni jijini. Kukamatwa na maafisa wa halmashauri ya jiji, maarufu kama Kanju, ni kati ya changamoto alizopitia.
“Ilifika kiwango kukamatwa kukawa ratiba, muhimu zaidi ikawa kuwapa heshima na kutii amri. Nilikuwa nawabembeleza hadi wananionea huruma,” anafafanua, akikiri ni kibarua kuwashawishi.
Katika pilkapilka hizo za kujiendeleza kimaisha, Kimani anasema kinyozi ambapo alikuwa akinyolewa Githurai, aliridhishwa na huduma alizopata na kuvutiwa na kazi ya kunyoa.
Anasema mhudumu wake naye alikuwa mkarimu, na mkwasi wa utu. Wakati wa ziada, Kimani alikuwa anamtembelea kujifunza namna ya kunyoa, bila kutozwa ada yoyote.
Anasimulia kuwa, haikuchukua muda mrefu kuelewa shughuli za kinyozi. “Miezi sita baadaye, nilikuwa nanyoa sambamba,” anasema.
Kulingana na barobaro huyu, alitengea uchuuzi muda wake na pia kunyoa muda wake, lengo likiwa kutafuta mtaji.
Kimani anaambia Taifa Leo kwamba alijinyima mengi, ili kuweka akiba, hata ingawa haikuwa rahisi.
Ili kuafikia malengo na ndoto maishani, mtu hana budi ila kujituma, kutia bidii katika kazi anayofanya na muhimu zaidi ni kuweka akiba, licha ya kidogo au kikubwa anachopata.
“Kuna njia nyingi za kuweka akiba. Unaweza kujiunga na Chama cha Ushirika (Sacco), ufungue akaunti kwenye benki, makundi ya kijamii ya hazina (vyama), na pia kwenye simu kufuatia kuibuka kwa apu za kampuni za mawasiliano zinazotoa huduma za kutuma, kupokea na kuweka pesa,” anashauri Jack Kamau, mtaalamu wa masuala ya fedha na kiuchumi.
Kufikia mwaka wa 2015, Justin Kimani anasema alikuwa ameweka kibindoni akiba ya Sh50, 000, fedha ambazo alizitumia kufungua kinyozi chake.
Mtaji huo, aliutumia kununua mashine mbili za kunyoa, kukodi chumba eneo la Zimmerman, Nairobi, kutengeneza fanicha, na vifaa vingine muhimu katika shughuli za kinyozi. Vilevile, alitafuta leseni.
Utangulizi hata hivyo haukuwa rahisi, nyakati zingine akisema kiwango cha wateja kilikuwa cha chini mno. Hakufa moyo, kauli atafutaye hachoki akichoka keshapata, ikimtia motisha.
Licha ya kuwa pandashuka hazikosi katika gange yoyote ile, Kimani anasema kazi yake imeimarika. Ana vibarua wawili.
Sawa na biashara zingine zilivyoathirika kufuatia mkurupuko wa janga la virusi vya corona nchini, Kimani anasema kabla ya Rais Uhuru Kenyatta kulegeza kamba sheria na mikakati iliyowekwa kusaidia kuzuia maenezi zaidi ya Covid-19, mambo yalikuwa magumu.
Anasema, mapato yalishuka kutoka Sh1, 500 kwa siku, hadi chini ya Sh500. Hilo hasa lilichangiwa na hofu ya watu, walipotahadharishwa kuepuka huduma zinazotolewa kupitia mtagusano kama vile ususi na kinyozi.
“Sasa kazi imeanza kuamka,” Kimani anasema. Mjasirimali huyo ameweka sheria, wanaohudumiwa sharti waingie na maski.
Pia anatilia maanani mikakati mingine iliyopendekezwa na Wizara ya Afya kudhibiti msambao wa corona, kama vile umbali kati ya mtu na mwenzake na kunawa mikono kabla ya kuhudumiwa.
Ndoto zake, ili kuimarisha biashara yake, anatazamia kusomea kozi inayohusiana na masuala ya biashara na pia kufungua vinyozi vingine Nairobi.